Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Janejelly Ntate James

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. JANEJELLY J. NTATE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye kitu muhimu ambayo ni Bajeti ya Serikali. Kwanza nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri Dkt. Mwigulu, mzee wa Yanga na Mheshimiwa Naibu Waziri, Mheshimiwa Masauni, mzee wa kimyakimya na timu ya wataalam wote wa Wizara ya Fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakika bajeti hii imeonyesha Wizara ya Fedha ina wachumi waliobobea. Wamekuja na bajeti ambayo imegusa kila kundi la Mtanzania. Ukiangalia vijana wameguswa, wazee wameguswa, wafanyabiashara wameguswa na akinamama wameguswa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mama Samia Suluhu. Usiposhukuru kidogo hata kikubwa huwezi kushukuru, kwa masuala ambayo amefanya kwa watumishi wa Tanzania. Mimi nijikite kwenye hotuba aya ya 44, maslahi ya watumishi. Akiwa kwenye Mei Mosi alisema, atapunguza Pay As You Earn, itabakia tarakimu moja ambayo ni nane na amefanya hivyo. Alisema atafuta tozo asilimia sita kwa mikopo ya vyuo vikuu, amefanya hivyo.

Vilevile ametoa bilioni 449, kwa ajili ya kupandisha madaraja ya watumishi, si kazi ndogo hii. Mpaka sasa ripoti za leo watumishi 78 wameshapandishwa madaraja, kati ya watumishi 92,619 ambao wanatakiwa kupandishwa. Kwenye hili ni lazima nitoe ushauri kidogo kwa Serikali, kwenye upandishaji wa vyeo. Mheshimiwa Waziri wa Fedha na Mheshimiwa Waziri wa Utumishi watatusaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye upandishwaji wa vyeo, kuna kasoro kidogo imetokea. Tunakumbuka 2016 watumishi walipandishwa madaraja, lakini muda kidogo yakafutwa, wakanyang’anywa zile barua za kupandishwa vyeo. Sasa, zoezi hili lilivyoanza, imekuwa ni adhabu kwao, wanahesabika walipandishwa 2017. Kwa hiyo, hawana sifa ya kupandishwa vyeo sasa hivi na watumishi wengine wameshakaa miaka 10, lakini barua waliyonyang’anya ilikuwa ni Serikali yetu Tukufu. Kwa hiyo, tuombe hilo wajaribu kurekebisha kidogo, hawa watumishi wafikiriwe, ambao walikuwa mwaka 2016 wako kwenye haki ya kupandishwa vyeo, lakini walipandishwa halafu wakanyang’anywa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuje kwenye michango ya Mifuko. Niishukuru sana Serikali, wamekuja na muarobaini wa kwenda kuponya wastaafu wetu. Wanapoamua kwamba makato watabaki nayo na watayapeleka kwenye Mifuko. Hata hivyo, niwaombe Serikali yangu Tukufu na Waziri wa Fedha, fedha hizi wakishabaki nazo ziende kwa wakati. Tusije tukasababisha malipo mengine ya penalty kwa kuzichelewesha na tusije tukasababisha wastaafu wetu kuchelewa kupata maslahi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna madeni ya wafanyakazi yanayosababishwa na upandishwaji wa madaraja. Kuna watumishi ambao walipandishwa mwaka na 2018 na 2016, bado hawajalipwa tofauti yao, kati ya mshahara wa zamani na mshahara mpya, yamekuwa ni madeni sugu. Tuombe hili nalo Wizara ya Fedha, maana ndio wahakiki wa madeni, basi wakawalipe watumishi hawa wafaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Mfuko unaitwa Mikopo ya Usafiri kwa Watumishi wa Serikali, mikopo ambayo haina riba. Mfuko huu uko chini ya Mheshimiwa Waziri wa Fedha. Tuiombe Serikali yetu wakae watafute namna ya kuuongezea fedha huu Mfuko, ili watumishi wote sasa waweze kufaidi matunda ya Mfuko huu. Fedha imekuwa haitoshi kwa hiyo, wengine wanasikia historia tu kwamba kuna mikopo ya magari yawawezeshe kuja kazini na kurudi nyumbani, lakini hawajawahi kupata mkopo huu. Ni kwa sababu, Mfuko umepewa fedha kidogo. Kwa hiyo, tuombe hapo fedha iongezwe kwenye huo Mfuko ili watumishi waweze kufaidi matunda ambayo wamewawekea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niongelee suala la Madiwani ambao watalipwa moja kwa moja kutoka Serikali kuu. Kwenye halmashauri kama tunasema hawa Madiwani watalipwa na Mfuko wa Serikali kuu, tuangalie na wale watumishi ambao walikuwa wanalipwa moja kwa moja kutoka kwenye halmashauri. Watumishi hawa wamekuwa wanakopwa sana, lakini walivyolishughulikia kama Serikali, manispaa za mjini ndio waliwahi kuhamisha watumishi wao wakalipwa na Serikali kuu, lakini wa pembezoni mpaka sasa hivi, wanalipwa kutoka kwenye vyanzo vya mapato vya halmashauri. Hasara wanayopata, hawawezi kupewa bima ya afya, hawawezi kuwa kwenye pension watumishi hawa. Sasa nao tuwasaidie waweze kufaidi matunda ya Serikali yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nije kwenye malipo ya Watendaji wa Serikali za Mitaa. Tumeamua kuwalipa Madiwani, Watendaji wa Serikali za Mitaa, lakini tumesahau Wenyeviti wetu wa Vijiji na Serikali za Mitaa. Hawa ndio huanza na wananchi wetu from zero, lakini Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa au Mwenyekiti analipwa shilingi 30,000 kwenye Manispaa zingine, pengine shilingi10,000 yaani haina standard. Hata hiyo yenyewe kulipwa inaweza ikapita miezi sita, hajawahi kulipwa. Suala hili linawaondolea heshima na uimara wa kufanya kazi na wanakuwa wana wasiwasi wa kufanya kazi. Kwa hiyo tuombe Serikali hawa watu nao iwaangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nimshukuru sana Mheshimiwa Mwigulu, Tunamwamini, kwamba bajeti hii tukiipitisha, itaenda kwa wakati kwenye manispaa, kwenye mikoa yetu na kwenye majimbo yetu ili ikafanye kazi kama ilivyopitishwa. Tuna uhakika huu upandishaji wa watumishi, fedha zitabaki watapandishwa wenye haki za kupandishwa, lakini wakiangalia ile kasoro ambayo tumeisema ya 2016. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga hoja mkono mia kwa mia. Ahsante sana. (Makofi)