Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Naomba nianze kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Rais mama Samia Suluhu kwa kazi kubwa na nzuri ambayo ameifanya Kanda ya Ziwa katika siku hizi tatu alizotembelea huko. Tunampongeza sana na kumshukuru sana kwa kazi kubwa aliyoifanya pale kwenye kivuko ambako tunajenga daraja. Kwa mtu ambaye hajawahi kufika anaweza kufikiri tunazungumzia daraja la mita 200, lile ni daraja lenye takriban kilometa 3 na pointi, lakini umuhimu wa daraja hilo ni pale unapokuwa una mgonjwa unampeleka Bugando kwenye hospitali ya Rufaa na ziwa limeziba water hyacinth unachukua masaa matatu unasubiri ferry. Umuhimu wa daraja hilo ni pale unapowahi ndege na ferry haziwezi kupita majani yameziba na umuhimu wa daraja hilo ni pale unapokimbizana na uhai wa mtu unataka kuvuka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba tumhakikishie Mheshimiwa Rais, wananchi wa Kanda ya Ziwa wanamshukuru sana na kumpongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa ambayo wameyasema weznangu. Kwanza nianze na msamaha wa kodi kwenye nyasi bandia. Mheshimiwa Waziri, nikupongeze sana kwa jambo hilo lakini nikuombe, nchi hii ina Majiji sita tu, unaposema umetoa msamaha wa kodi wa nyasi bandia kwenye majiji sita, maana yake unataka kupandisha michezo kwenye majiji sita na tayari majiji haya yana loopholes nyingi na uwezo mkubwa wa kujiendesha na kuendesha viwanja vyake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningetamani kusikia kutoka kwako unategemea kupata hasara ya shilingi ngapi iwapo utaruhusu Makao Makuu ya mikoa yote Tanzania watapata viwanja vyenye nyasi bandia. Maana mpaka ninapozungumza leo kila nikiangalia kwenye viwanja tulivyonavyo Tanzania…

MHE. FESTO R. T. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Costantine kuna taarifa. Taarifa tafadhali.

T A A R I F A

MHE. FESTO R. T. SANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kumuunga mkono mzungumzaji anayezungumza kwenye suala la nyasi bandia. Nataka kumpa Taarifa kwamba, kati ya hayo Majiji sita anayoyazungumzia, Dar es Salaam tayari wana viwanja, Mwanza tayari wana viwanja kwa hiyo kuna Majiji manne tu ndiyo ambayo hayana viwanja. Kwa hiyo, unachokizungumza ni kitu sahihi na sisi kama wadau wa michezo tunakuunga mkono. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Constantine, Taarifa hiyo.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea hiyo taarifa. Hapa ninachotaka kumwambia Mheshimiwa Waziri ni kwamba, kwa mfano tukisema kwenye mwaka wa fedha ulioisha ni wangapi walioingizia pesa kwa kulipa kodi kwa kuleta nyasi bandia? Na unatarajia utakapofuta sasa hiyo misamaha Mikoa mingine utakuwa umeingia hasara kiasi gani? Mimi nikiangalia Mikoa ni miwili na walioweka nyasi bandia ni walewale na inawezekana kuna mwaka mzima utaisha hakuna nyasi bandia. Kwa hiyo, unachokifanya Mheshimiwa ni kuifanya nchi nzima iwe na mwamko wa michezo kuliko mikoa ambayo tayari imeendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri mimi ninaunga mkono kabisa kodi ambayo umeileta kwenye LUKU ninaiunga mkono. Nadhani ni sahihi hata kama kiwanja kina apartment sita na apartment zote zikawa na LUKU yake n azote zikadaiwa kodi ni sahihi. Nataka nitoe mfano, sasa hivi ukiwa na low density umejenga apartment nane na kama zinatofautiana, unapokwenda kulipa TRA unalipa property tax ya kila apartment, sasa kwa nini unashindwa kulipa huo mchango ambao umeupendekeza, kodi ambayo imependekezwa kwenye kila apartment? Nafikiri ni sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili litaepusha sana kwanza makadirio ya hovyo hovyo yaliyokuwepo mwanzo ambayo Mheshimiwa wa Awamu ya Tano aliyaondoa, lakini uhakika wa ukusanyaji wa pesa yenyewe. Duniani kote maendeleo yanakuja kwa watu kulipa kodi na watu lazima walipe kodi ndiyo waone maendeleo yanakuja. Hatuwezi kupiga kelele hapa kila siku tunataka maendeleo wakati hatutaki kulipa kodi, lazima tulipe kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninataka kulisema hapa na kumshauri Mheshimiwa Waziri, bado pesa nyingi sana inapotea. Mimi nina uhakika TRA wanakusanya kama siyo asilimia moja ya tatu ya kodi basi ni nusu ya kodi. Mlifanya mpango mzuri sana pale bandarini kwamba, kodi za magari zinajulikana, kabla hujaagiza gari unajua kodi yako hii hapa, jambo ambalo unatakiwa ulibuni na kulifanya huku mtaani ni kuondoa utamaduni wa mtu anajaza zile audited accounts halafu tunaanza mjadala miezi mitatu, miezi minne, miezi mingapi, matokeo yake tunakuja kuishia kwenye kuelewana nikutoe ngapi ili tuweze ku- balance tunapoteza kodi nyingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuangalie upya namna tunavyoweza kufanya ili kuwafanya walipa kodi anapomaliza kulipa kodi zile instalments makadirio yake yaje genuine na anapolipa awe amemalizana na Serikali, kila mtu atalipa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jingine tupitie upya orodha ya wamachinga. Machinga tumewapa vile vibali wengine wana maduka, wengine wanauza uji, mwingine anauza mchicha, tupitie upya tu-define tunafikiria machinga mwenye kibali ni mtu wa namna gani? Ili kundi fulani ambalo tunafikiri limevuka kwenye hiyo level tulitoe. Tutakuwa tumeongeza malipo ya kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya ushauri huo niende sasa kwenye idara moja ya uvuvi. Nimeangalia kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri anapendekeza kufuta kodi ya solar power. Hivi sasa kule kwetu Kanda ya Ziwa, solar panels ndiyo zinazo-charge taa za kuvulia dagaa, lakini nimeangalia sasa amefanya double standard, wakati amependekeza kufuta msamaha wa kodi amependekeza kuongeza withholding tax kwa mazao yote ya uvuvi yanayopelekwa kiwandani. Mheshimiwa Waziri this is too wrong.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ngoja niseme, samaki ambao mvuvi anawapeleka kwenye kiwanda production cost yake ni very expensive, unapomkata asilimia mbili utahamasisha smuggling. Nataka nikwambie mvuvi kwenye mtumbwi mmoja ana-invest about 20 million, siku moja ili aende ziwani anahitaji mafuta lita 30. Kuna wakati anapata kilo 10 tu na hizo kilo 10 ndiyo anazokusanya kwenye boti zifike tani mbili ziende zikauzwe, wewe unafikiri zote ni faida, huyu sio mkandarasi, utakapoingiza kiwandani ukakata 2% withholding tax kwa mvuvi utakuwa umekata mtaji tangu kwenye nyavu, kwenye mafuta na kwenye operation cost, sina uhakika kama watu wako wamelielewa vizuri suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukimuona mtu yuko pale Mwanza ana boti la tani 10 la samaki amekusanya samaki hao wiki mbili na amekusanya kwa wavuvi wanaopeleka kilo 20, kilo 25 ambao kila siku wanatumia lita 30 za mafuta na ana boti investment yake ni milioni 20. Sasa unaposema unaenda kukata withholding tax kwa samaki aliowapeleka kiwandani maana yake nini, unakata mtaji. Mimi nikuombe Mheshimiwa Waziri hili practically tunakwenda kufilisi watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliishauri hapa Serikali mwaka 2017, ilikuwa inafanya operations nyingi kwa wavuvi na matokeo yake wavuvi wote wakubwa ziwani wamekwisha, wale waliokuwa wanakopesha wavuvi hawawakopeshi tena. Na tuliwaambia kwamba, mnafurahi mnakusanya pesa ya faini, lakini watu wanafilisika.

Sasa leo watu wamerudi kwenye kuvua wanavua illegal, matokeo yake sasa ni nini, hakuna tena mvuvi anakopeshwa nyavu, hakuna mvuvi ana mtaji. Sasa hivi mtakapoleta hii kodi watu watapeleka samaki Uganda na Kenya. Nakuomba Mheshimiwa Waziri liangalie vizuri sana jambo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba Mheshimiwa Waziri unisaidie kupata ufafanuzi, kwenye ukurasa wa 34 umesema, nimeona kuna mambo mawili kama hapa yana- contradict, unazungumzia kuweka kiwango cha kutoza kodi kwa wachimbaji wadogo, kwenye (a) umesema kutoza kodi wachimbaji wadogo wa madini kwa kiwango cha asilimia tatu kwenye thamani ya mauzo ya madini, lakini nimeona tena kwenye sehemu ya nne unasema kutoza kodi kwa yule ambaye amenunua madini kwa wachimbaji wadogo ili kuhakikisha kwamba, anawalipia kodi sasa sijaelewa. Kwa sababu, huyu ulishamtoza kodi huku chini, huku tena unakuja kumtoza kodi huku. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukumbuke pia huyu anayeuza madini hiyo siyo faida, hawa wanaochimba mashimo anachimba miezi mitatu anakwenda mita 100 hajaingiza hata 100. Shimo linamgharimu milioni 50, siku akianza kuzalisha mifuko 10, mifuko 10 anaitoa kwa one week, akiifikisha juu umeshachukua asilimia tatu, lakini bado unasema utahakikisha kwamba kuweka wajibu wa mchimbaji mdogo wa madini kama muajiri wa kukata kodi mapato ya ajira kutoka kwa wafanyakazi wake pale tu madini yanapokuwa yamepatikana na kuuzwa kwa masoko ya madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, madini yametoka wapi? Yametoka kwa wachimbaji wadogo, umeshawakata kodi, huyu mchimbaji mdogo akienda kuuza unamkata kodi, tunapambana sana suala hili linafanana na kwenye samaki. Wenye viwanda wanalalamikia royality, umekwishaenda kukata asilmia mbili, umeshamkata mchimbaji mdogo, unamkata na huyo, Mheshimiwa hii si double taxation? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikuombe Mheshimiwa litazame vizuri. Tukiamua kumkata yule mdogo kule chini basi tu-track source yake iko wapi ili kusudi hawa waliopo wabaki huku chini

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Constantine Kanyasu.

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)