Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Kenneth Ernest Nollo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bahi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. KENNETH E. NOLLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nianze kwa kuipongeza na kuishukuru Serikali kwa utaratibu iliyochukua wa kutoa fedha shilingi 500,000,000 kwa kila jimbo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utaratibu huu nauona una tija zaidi tofauti na ilivyozoeleka. Kwa upande wa Jimbo langu la Bahi, shilingi 500,000,000 hizi zimenisaidia kutatua changamoto kubwa ya barabara inayotoka kwenye Kata ya Chifutuka ambayo iko kilometa 90 kutoka kwenye Makao Makuu ya Wilaya na wakati mwingine imekuwa inajifunga haipiti. Lakini kwa 500,000,000 hizi tulizozipata tunaenda kutatua kwa kiasi kikubwa tatizo hili la barabara na hatimaye kuweza kuleta maendeleo ya wananchi kupitia kata ile. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nataka niipongeze sana Serikali. Bajeti hii ina ahueni kubwa katika kuleta maendeleo lakini pamoja na hilo, tunakuja kwenye matumizi ya bajeti. Bajeti yetu imekuwa mara nyingi haifiki asilimia 70 katika matumizi hususan katika miradi ya maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali hasa Wizara wa Fedha aelewe na atambue hili kwamba bajeti yetu iwe ni rural centered development. Iangalie zaidi katika kutatua shida zaidi za wananchi waliopo vijijini na kwa kweli tuna shida kubwa sana vijijini. Tuna shida ya zahanati, kwa mfano Jimbo langu la Bahi sina zahanati 16, sina ambulance, hata ambulance zinazokuja ugawaji wake bado haueleweki. Ukigawanywa kama hivi tulivyopewa 500, 500 italeta ahueni. Kwa hiyo, nadhani hii model iliyotumika ya 500,000,000 tuiangalie katika bajeti iweze kutumika katika maeneo mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya bajeti kupitishwa imekuwa tunasubiria kudra za Hazina ndiyo ziweze kutupatia katika maeneo yetu. Wakati mwingine unasikia upande fulani wamepewa, huku kwako hujapewa, kigezo hakieleweki. Ili twende sawa sawa, kuwe na equal distribution, ni lazima tuone namna gani. Kama tunaamua kutoa milioni 600 kwa ajili ya kumalizia maboma kwenye majimbo yote, ziende kote. Namna hii tunaweza tukaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niishie pale kwenye conclusion ya Waziri wa fedha kuhusu kadi ya njano na kadi nyekundu. Maneno yale yana busara kubwa ya kuonesha namna gani kiongozi wetu wa Taifa hili alivyosheheni uzoefu wa kuweza kuliongoza Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini sio hivyo tu ni kwamba Mheshimiwa Samia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi. Chama hiki kina utajiri wa rejea katika uongozi. Ni chama ambacho kimepita katika vipindi vingi tangu kuanza mapambano ya uhuru lakini baada ya nchi yetu kupata uhuru. Lakini, hata hivyo vile vile kupambana na mifumo mbalimbali ili kujiletea maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Chama chetu cha Mapinduzi kimekuwa kinafanya reform kila wakati. Iwe katika kipindi kile sasa tunaanza kuimarisha viwanda Watanzania tuweze kujitegemea. Lakini hata hivyo, tuwe tumekuwa tunaangalia tunaenda na sera gani, tunajibadilisha kila mara kutokana na matakwa ya jamii yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuliwahi kutoa Sera za CCM katika miaka ya 90. Lengo letu lilikuwa ni namna gani sasa tunaanza kwenda katika mageuzi ambayo yanatokea katika Dunia na sisi tuweze kuendana na namna Dunia inavyoenda. Kwa hiyo, nataka niwahakikishie Watanzania, Mheshimiwa Samia anarejea kubwa ya uongozi na ninataka niwaambie hakuna shaka ya kuwa na wasiwasi kwamba Mheshimiwa Samia hatalivusha Taifa hili. Atafanya vizuri zaidi kwa sababu ana msingi mkubwa ambao msingi umetengenezwa na Chama cha Mapinduzi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, imetokea kasumba ya baadhi ya Mwenyekiti wa chama kimoja kuonesha kwamba kama ana kauli ya kuweza kulazimisha kila anachotaka yeye. Nataka tu niseme kama nilivyosema Samia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi. Mwenyekiti huyu ambaye kidogo anataka kujipa ahueni kwamba eti anataka kuja 25 ashike dola alianza tangu enzi za Mzee Mkapa, Mzee Mkapa akaondoka yeye bado ni Mwenyekiti, akaja Mzee Kikwete yeye bado Mwenyekiti, amekuja Hayati Magufuli yeye bado Mwenyekiti. Sasa mtu ambaye amekosa pumzi kabisa amechoka hoi bina taaban anataka kuja kupambana na Mwenyekiti ambaye ni mpya kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia Mwenyekiti wetu ni Mwenyekiti ambaye ameonesha, Rais wetu ameonesha ni mtu anayejua hata Dunia inavyoenda. Ninyi mmeshuhudia hata mitazamo yake, juzi amesema kwamba sasa Taifa letu liangalie kuna mageuzi makubwa sana ya kidijitali yanatokea. Sasa hatuwezi kubabaishwa na Mwenyekiti huyu ambaye ni Mwenyekiti wa enzi na enzi, amekosa mvuto, amepauka na anajinasibu anasema wao ni makamanda. Kwanza nataka niwaambie, sisi tulikomboa nchi nyingi za Afrika katika kupigania uhuru. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wameanza kuvaa makombati hayo wanayoyavaa sisi tunawaona. Sisi tulishapigania uhuru na chama chetu kina heshima kubwa katika Bara la Afrika na ninataka niseme Mheshimiwa Samia sio wa kufanyiwa mashinikizo, yuko kwenye chama imara, anajiamini na nataka niseme tunaendelea kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru ahsante sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)