Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Jafari Chege Wambura

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Rorya

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. JAFARI W. CHEGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi. Nami niungane na wenzangu kwanza kabla sijaenda mbele zaidi, kumshukuru na kupongeza kazi kubwa aliyoifanya na Rais wetu wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi wamesimama hasa wazoefu, wengi wamekuwa wakisema hii ni bajeti ya kumi; wengine ni bajeti ya tano kwa kadri ya muda wa miaka aliyokaa ndani ya Bunge. Sisi Wabunge ambao ni awamu yetu ya kwanza tunasema hii ni bajeti yetu ya kwanza. Kipekee kabisa tunakwenda tarehe 29 kwenye Majimbo yetu tukiwa tumetosheka na tumeshiba sawa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mambo ambayo kimsingi pamoja na miaka yote hii ya nyuma hayakuwa yakifanyika, sisi ndani ya Bunge hili kwa mara ya kwanza tunakwenda kwa wananchi wetu tukiamini na tukiyaona yamefanyika, angalau tunaweza tukasema nini Mheshimiwa Rais wetu ametutendea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumshukuru sana na pia kuwapongeza Mawaziri wote; Waziri Mwigulu Nchemba na Naibu wake pamoja na Wizara nzima, kwa namna ya kipekee walivyokaa humu ndani na kusikiliza maoni ya Wabunge. Leo hii ukiangalia upande wa TARURA, ni historia, haijawahi kutokea kutengwa fedha zaidi ya shilingi milioni 500 kurudi kwenye Majimbo, halafu Mbunge ukashirikishwa namna ya utendaji wa fedha ile. Haijawahi kutokea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi tangu nimeingia hapa na nimekuwa nikilia sana juu ya daraja langu la mto Mori, na nimekuwa nikisema lile daraja linaunganisha tarafa tatu kati ya tarafa nne ndani ya Jimbo, hata tarafa ya nne nayo inaingia. Leo hii ninavyochangia hapa, nakwenda tarehe 29 ndani ya Jimbo nimepewa zaidi ya shilingi milioni 950, kwa ajili ya utekelezaji wa daraja lile. Nikiongeza na shilingi milioni 500 maana yake nina 1.4 billion, ambayo inakwenda kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ndani ya Jimbo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nasema inawezekana ikawa ni bajeti ya kwanza kwa awamu hii, lakini kwetu sisi Wabunge wa mara ya kwanza kiukweli imetutendea haki na imetunyanyua sana. Pia amekwenda maeneo mengi; maeneo ya maji imegusa, maeneo ya afya imegusa, kiukweli sina namna ya kusema zaidi ya kuwapongeza Mawaziri na Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, cha muhimu ambacho nataka nichangie leo ni kumwomba Mheshimiwa Waziri, mimi napenda sana kushauri kuliko kusifia, kwa sababu naamini nikishauri vizuri ndiyo ataendelea kufanya kazi sawa sawa na ataendelea kuwepo kwenye Wizara hii na mwishoni atatengeneza historia ndani ya nchi hii ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naomba niende ndani ya vipengele vya kumshauri ili aendelee kufanya kazi vizuri kuliko kumsifia zaidi. Naamini ameshafanya mengi mazuri, Wabunge wameshamsifia na anastahili sifa hizo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kwanza ili kuhakikisha fedha zote za miradi ya maendeleo, tengeneza historia kuhakikisha fedha zote zilizotengwa zinakwenda kwenye majimbo na kwenye Halmashauri. Ukifanya hivi utakuwa umetengeneza historia ya miaka yote ambayo tunasema zinakwenda asilimia 10 na asilimia kadhaa kwenye bajeti za kisekta. Peleka fedha zote kwenye miradi ya kimaendeleo. Amini ninachokwambia Mheshimiwa Waziri, tukirudi hapa mwakani utakuwa umetengeneza historia nzuri sana, kwa sababu miradi mingi itakwenda kutekelezwa na mwishoni wewe ndiye utakayepata sifa hizi kwa wananchi wetu ndani ya maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, napenda sana kuchangia kwenye Property Tax (Kodi ya Majengo). Nishawahi kusema nachangia kama mdau. Ningependa nichangie maeneo matatu na ninaamini kwamba Mheshimiwa Waziri utalichukua hili, utakuja kulitolea ufafanuzi. Unakuta kwenye kiwanja kimoja, mimi mmiliki wa nyumba nimejenga nyumba tatu kwenye kile kiwanja au nyumba nne ndani ya kiwanja; nimeweka Luku moja peke yake. Maana yake mwishoni nikilipa Luku, nalipia nyumba moja. Sheria inavyosema, ni kila property; nyumba iliyopo kwenye kiwanja kimoja, kama ni property Na. 5 zile nyumba tatu zote kwa sasa zinalipia kodi ya jengo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ikiwa Luku ni moja kwenye eneo lile, lazima angalau utakapokuja Mheshimiwa Waziri utuambie, zile nyumba mbili zinazosalia katika tatu kwenye kiwanja kimoja, ni mpango gani mkakati uliopagwa ili angalau zote ziwe accommodated kwenye Luku moja ya ukusanyaji wa eneo hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, kwenye Property Tax kuna haya majengo, tuchukulie nyumba za ibada ambazo kimsingi kwenye sheria ya sasa hazikuwa zinalipa kodi. Kuna wazee wa miaka 65 na kuendelea, umri wao umezidi walikuwa hawalipo hii Property Tax. Namna gani sasa unaenda kuwa-accommodate? Kwa mfano, majengo haya ya ibada yana Luku: Je, hawatahusika kwenye Luku zao kulipia Property Tax? Nafikiri hii na yenyewe kwenye mkanganyiko Mheshimiwa Waziri utaiweka sawa sawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kuna majengo ambayo yanalipiwa na wapangaji. Mwenye nyumba amejenga, Luku inalipiwa na mpangaji: Je ni namna gani ambavyo tutawa- accommodate wale wapangaji ambao wananunua Luku kwenye majengo waliyopanga, wakati Property Tax inatakakiwa kulipiwa na mmiliki wa eneo lile (owners)? Haya mambo matatu Mheshimiwa Waziri naamini ukiyaweka sawa sawa hakuna kinachoshindikana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nichangie sana kulingana na Mahusiano ya Hali ya Uchumi na Mpango wa Maendeleo ya Taifa, Mheshimiwa Waziri tutakubaliana, ili maeneo yote kuwe kuna uchumi imara kwa wananchi, cha kwanza kabisa, lazima kuwe na stability, lazima kuwe na usalama wa wale wananchi ili kufanya biashara vizuri. Nitatolea mfano ndani ya eneo langu mimi la Rorya. Mimi shughuli zangu za kiuchumi ni tatu; moja, ni kilimo; pili ni uvuvi na tatu ni ufugaji. Kilimo sina shida kwa sababu naamini kwenye bajeti ya kisekta Waziri amenitengea fedha na nitakwenda kutekeleza hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zinabaki shughuli mbili za kiuchumi ili wananchi wale ndani ya Jimbo waweze kwendana na kasi ya mpango wa Taifa ndani wa miaka mitano. Tuchukulie mfano suala la uvuvi. Mheshimiwa Waziri mimi kule, napenda nilizungumze kwa Waziri wa Bajeti, Waziri wa Fedha na pia Waziri wa Mambo ya Ndani na ikibidi Waziri Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kuna wizi mkubwa sana unafanyika kwenye maeneo ya maziwani. Wavuvi wanapokwenda kuvua na ndiyo shughuli kubwa ya kiuchumi. Ndani ya Jimbo langu Mheshimiwa Waziri, asilimia 77 nimezungukwa na ziwa. Unaweza kuona, ili uchumi wa wananchi wangu uweze kuendelea, ni lazima wafanye shughuli ya uvuvi, lakini haufanyiki sawa sawa. Wanapokwenda kuvua, wanakutana na shughuli kubwa sana ya kupigwa na kunyang’anywa zana zao za uvuvi. Nilikuwa naomba Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani, ikibidi Waziri Mkuu atusaidie sana kwenye hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya shughuli mbili hizo nilizosema, ya tatu ni ya ufugaji. Mheshimiwa Waziri, leo ufugaji haupo stable. Kule ndani ya Jimbo langu, kila siku ndani ya Halmashauri ya Rorya isipopita siku mbili, siku tatu lazima utakuta wananchi wameibiwa mifugo; na lengo kubwa la uanzishwaji wa Halmashauri zile mbili, mpaka ikafikia sehemu ikatengenezwa Polisi ili kuhudumia maeneo haya yote mawili, haipo sawasawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo ninavyozungumza, jana wananchi toka asubuhi mpaka saa 8.00 wanazunguka kutafuta mifugo yao ambayo imeibiwa. Uanzishwaji wa kanda maalum ndani ya ile Halmashauri kwa maana ya Tarime na Rorya, ilikuwa ni kuhakikisha angalau kuna usalama kwanza wa hizi Halmashauri mbili, lakini nisikufiche ningetamani sana Mheshimiwa Waziri wa Mambo ya Ndani alichukulie serious suala hili, kwa sababu kule imekuwa ni kero kubwa sana. Leo Mheshimiwa Rais akienda au Waziri Mkuu, amini ninachokwambia, bango la kwanza atakalokutana nalo ni suala la wizi wa mfugo. Imekuwa ni suala la kihistoria, limekuwa la miaka mingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali kwa unyenyekevu mkubwa, watafute mbinu za kukomesha hili suala ili angalau wale wakazi wa Rorya ambao kimsingi wameamua kuhamasika kwenye kuingia kwenye shughuli za ufugaji, wafuge mifugo yao, kama ni ng’ombe ikiwa ni salama kabisa bila kuingiliana na huu msuguano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kwa sababu bila ya kufanyika, haya ndiyo yana mahusiano na mwingiliano wa ukuaji wa kiuchumi wa wananchi wangu. Kama utakutana na disturbance kwa maeneo haya mawili, maana yake kila mwaka watakuwa wanakwenda na bado watakuwa wanarudishwa nyuma, kwa sababu mtu anajikakamua, anaanza kufuga ng’ombe wawilia au watatu; na mwingine wale ng’ombe ndiyo anaotumia kulipa ada ya watoto wake. Mwingine wale ndiyo wanazitumia angalau akipata shida kuuza na kuingia kwenye shughuli zake za kiuchumi na kujiendesha katika maisha yake. Halafu haifiki mwisho, wale ng’ombe wanakuja kukwapuliwa, anaanza upya yule mwananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana sana, Wizara ya Mambo ya Ndani, kwa sababu nimeshafuatilia kwa muda mrefu, walichukue walione ni namna gani angalau wanalitatua ili wananchi nao waweze kujikwamua kwenye suala hilo la kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo machache, nakushukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)