Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Mussa Ramadhani Sima

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumshukuru sana Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nitumie fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Rais, mama yetu Samia Suluhu, kwa bajeti nzuri hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia nimpongeze kaka yangu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, pamoja na Naibu Waziri na timu nzima ya Wizara ya Fedha, bila kuwasahau Kamati. Nimpongeze Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti pamoja na Wanakamati wote, kwa kweli wametuonesha mwanga ni wapi tunapaswa kupita kushauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapendekezo ya bajeti hii yanatupa fursa sisi kuchangia na kuweza kuishauri vizuri Serikali. Naomba nianze na eneo la uzalishaji wa mafuta ya kula. Tarehe 13, juzi, Waziri Mkuu alikuwa mgeni rasmi pale Singida kwa wadau wa alizeti; tumefanya mkutano mzuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitumie fursa hii kumpongeza sana Waziri Mkuu; mkutano ulikuwa na tija na umeleta mafanikio makubwa sana. Yapo mapendekezo zaidi ya 16 ambayo Mheshimiwa Waziri Mkuu ameyatoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nijikite kwenye bajeti hapa. Serikali imeongeza ushuru wa forodha kwenye mafuta ghafi asilimia 25 yanayoingia, lakini kwenye mafuta masafi (semi-refined and refined) asilimia 35; ni jambo jema sana, niipongeze sana Serikali kwenye eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukumbuke huku nyuma tumekuwa tukiongeza tangu bajeti ya 2016 mpaka sasa tumeendelea kuongeza. Yawezekana lipo tatizo. Kwa nini tunaendelea kuongeza asilimia ya ushuru, kutoza ushuru wa forodha wakati huku tunajua kabisa soko la mafuta ya chakula linaendelea kudidimia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nishauri eneo hili vizuri kidogo; yawezekana kule mafuta yanapotoka wenzetu kwenye nchi zao wanapata ruzuku ya uzalishaji na wanazalisha kwa wingi, kwa hiyo kadri tutakavyokuwa tunaweka tozo hii ama kuongeza kodi hii, inawezekana ikawa haisaidii, hata tukiweka asilimia 50.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nini kifanyike; cha kwanza, tunapoangalia market price inayotoka kule sisi kwetu huku inatupa changamoto. Lakini jambo la pili kwenye eneo hili, sisi lazima tu-regulate bei ya mafuta nchini kwetu. Na tayari tunaye regulator ambaye ametuonesha anafanya kazi vizuri; EWURA wamefanya kazi nzuri kwenye eneo la maji na kwenye eneo la mafuta ya petroli na mafuta ya alizeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umefika wakati sasa tumpe na jukumu hili la mafuta ya kula ili aweze ku-regulate market price kwenye nchi yetu. Tunaweza tukatatua tatizo kubwa hapo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la pili ni Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye viwanda vyetu nchini. Mwaka 1997 mpaka 2013 kulikuwa na zero-rated. Maana yake walikuwa hawalipi hii VAT asilimia 18. Tukaanzia hapo sasa wanalipa asilimia 18.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto kubwa inayojitokeza hapa ni kwamba mwekezaji ambaye ana turnover ya milioni 100 anaondolewa ile VAT ya asilimia 18. Maana yake unampa fursa yule mtu ya kujipangia bei ya kununua mbegu, na bei ya kuuza mafuta. Utawaua wenye viwanda wengine wadogo ambao hawana turnover hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka niishauri Serikali hapa; kama tumeamua kuboresha kuhakikisha hawa wazalishaji wa mafuta ya alizeti au na mafuta mengine tuondoe VAT ya asilimia 18 kwa wawekezaji wa viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo ninapenda nishauri sana; wawekezaji wote wa viwanda hawana mashamba darasa. Wawe na mashamba darasa, lakini wawe na mikataba na wakulima wanaozalisha mbegu ya alizeti ili kuwapa fursa wakulima hawa katika uzalishaji wao, uwe ni uzalishaji wenye tija, awe anajua kabisa anaweza kupata soko wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunahitaji kuwa na Sheria ya Kilimo, hapa hatuna Sheria ya Kilimo, tuna sera. Sheria ya Kilimo inatusaidia sisi ku-control ardhi yetu ile, inatusaidia sisi kupima udongo kwamba uzalishaji ufanyike, unapimwa, tunaweza ku-control eneo hili. Sasa uzalishaji wa mafuta ya alizeti unaweza kuwa na tija kubwa sana tukizingatia maeneo hayo ambayo nimeshauri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo limejitokeza ni Sheria ya Posta na Mawasiliano ya Kielektroniki Sura 306. Hili ni jambo jema sana, lakini nataka nishauri kidogo hapa, kwamba kutakuwa na tozo ya shilingi kumi mpaka shilingi 10,000; jambo jema. Lakini wanaotozwa ni akina nani? Maana yake wanaotumia simu wote, leo ukiangalia wajasiriamali wadogo wote; mama ntilie, machinga na wengine wote, wanatumia simu kwa ajili ya kuendesha biashara zao. Na simu ndiyo zimekuwa mtaji mkubwa wa kuhakikisha wanahifadhi fedha zao. Leo wakiona kuna ongezeko lingine maana yake wataacha sasa kutumia simu, watakuwa wanatembea na fedha mfukoni, wengine watajaa kwenye mabenki, itakuwa ni changamoto. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nishauri, la kwanza, tuweke kiwango maalum cha watu ambao wanatumia miamala hii waweze kutoa tozo hii. Kama ni shilingi 300,000 au ni 500,000, kiwango maalum waanzie hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, iko fedha ambayo tunapewa tunagawiwa sisi kila mwisho wa mwezi kutoka kwenye makampuni ya simu, unashtukia tu mwisho wa mwezi umepata gawio hili. Gawio hili ukikusanya uka-accumulate fedha zote linakaribia bilioni 39.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Serikali isichukue hizi fedha ambazo ni gawio linalotoka kwenye makampuni iweze kuingiza ku-cover hili gap ambalo wanalizungumzia bilioni 39, badala ya kuwa tu tunapewa fedha ambazo sisi hatujui zinatoka wapi, hata mchanganuo wake hatujui. Kwa hiyo, hilo ni jambo ambalo ninapenda sana nilishauri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Singida Mjini pale tunayo Hospitali ya Rufaa. Ile Hospitali ya Rufaa inaendelea na ujenzi. Na ujenzi wake tayari fedha ambazo zinatakiwa kwenda kukamilisha ujenzi hazijaenda mpaka leo, zaidi ya bilioni 3.5. Na Serikali imepanga fedha za dawa, na kule kuna fedha zaidi ya milioni 700 ambazo zimeingia kwenye Mfuko wa Hazina, zinatakiwa zirudi katika uendeshaji ili wananchi waweze kupata dawa na ujenzi uweze kuendelea; mpaka sasa fedha hizo hazijaweza kwenda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka nimuombe Mheshimiwa Waziri; umefika wakati, tunahitaji fedha hizi ziende, lakini tunahitaji hizi fedha pia za ujenzi ziendelee ili Singida Mjini tuweze kutumia majengo ya Hospitali ya Mkoa wa Singida ambayo inahamia kwenda Hospitali ya Rufaa iliyoko Mandewa, yale majengo ya hospitali ya wilaya tupunguze gharama ya uendeshaji katika hospitali zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa maji katika miji 28; hili ni jambo ambalo tunahitaji lifanyike haraka sana. Lakini maji haya siku zote tuna-deal na water supply, lakini water resource hakuna. Hatuangalii vyanzo vya maji, sisi tunaangalia kusambaza maji tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo unatupangia fedha za kutosha, zaidi ya bilioni 33. Nataka niishauri Serikali; sisi tunahitaji Mradi wa Maji wa Ziwa Victoria uweze kufika kwa wakati. Hii ndiyo itakuwa sustainability ya upatikanaji wa maji kwenye maeneo yetu, badala ya kuwa tuna-drill maji ambayo hatujui yapo au hayapo na unaingiza fedha nyingi ambazo tunatupotezea mapato mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna posho hapa wamepewa watendaji wa kata. Lakini naomba sana tufikirie zaidi kuhusu wenyeviti wa vijiji na wenyeviti wa mtaa. Na hawa wala huhitaji Serikali Kuu itoe fedha, Serikali Kuu inatakiwa kutoa mwongozo kwenye Local Government.

Mheshimiwa Mwenyekiti, halmashauri zetu zitenge bajeti kwenye mapato yao ya ndani na kwa kiwango ambacho wanakubaliana. Kama ni shilingi 50,000 basi 50,000 kwa kila mwenyekiti wa kijiji ama mwenyekiti wa mtaa. Hili jambo litatoa fursa kwa hawa watendaji walioko chini kufanya kazi yao vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaiunga mkono sana bajeti hii na niwatakie kila la heri katika utekelezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja tu…

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Sima.

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, moja tu.

MWENYEKITI: Malizia.

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Madiwani; sisi manispaa tumeingia kwenye akaunti siku nyingi, suala la kuingia kwenye akaunti is not an issue. Issue ni kuongeza posho. Waziri atusaidie, atuongezee posho. Hata ukiongeza kalaki moja kwa kila Diwani utakuwa umetusaidia, ndio wanaosimamia shughuli zote hizi. Ahsante sana.