Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Nicholaus George Ngassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igunga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. NICHOLAUS G. NGASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru nami pia kunipatia nafasi ya kuongea na kutoa mchango wangu kwenye bajeti kuu ya Serikali ya mwaka 2021/2022. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza niipongeze Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mama yetu Rais Samia Suluhu Hassan kwa consistency nzuri waliyoanza nayo katika ukusanyaji wa mapato, ukijaribu kuangalia taarifa ya Msemaji Mkuu wa Serikali mwezi wa nne tulikusanya trilioni 1.34, mwezi wa tano tumekusanya trilioni 1.3 naamini na mwezi wa sita mtakwenda vizuri, hongereni sana Serikali katika ukusanyaji wa mapato. Ni mwanzo mzuri, Wizara ina vijana wawili mahiri yupo Mheshimiwa Daktari Mwigulu Nchemba yupo na Injinia Masauni ambao kwa nyakati tofauti wameshakuwa mabosi wangu wakati nipo Serikalini nawajua umahiri wao naamini watakwenda vizuri, hongereni sana pia kwa kuaminiwa.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hotuba yangu itakuwa ina pande mbili, upande wa kwanza utakuwa ni wa kitaalam na upande wa pili nitaelezea uhalisia katika yale nitakayoyachangia. Upande wa kitaalam ambao utakuwa ni upande wa nadharia reference nitafanya kwa kutumia sheria mbalimbali na miongozo mbalimbali, sasa naanza na jambo la kwanza ambalo nataka nilichangie jioni hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ni udhibiti na usimamizi wa fedha za serikali, makusanyo ni mazuri tumepanga bajeti ya trilioni 36 kwenda kukusanya na kutumia katika mwaka huu wa fedha, tunayo Sheria ya Fedha Namba 6 ya mwaka 2001 inaitwa Public Finance Act ilipofanyiwa maboresho mwaka 2010 ilizaa baadhi ya taasisi, moja ya taasisi ambazo zilizaliwa inaitwa taasisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Ndani wa Serikali - Internal Auditor General Office ndiyo taasisi ambayo kwenye Halmashauri inaleta watu wanaitwa Internal Auditors au Wakaguzi wa Ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wakaguzi wa Ndani pamoja na majukumu yao mengine yote wana majukumu makubwa matatu ambalo la kwanza ni kuangalia michakato inayoendelea kwenye Taasisi za Serikali tunasema kuangalia zile process. Jukumu la pili ni kuangalia ile assurance udhabiti wa Serikali kwamba tunakokwenda ni uhakika na jukumu la tatu ni kuangalia quality tunasema quality control.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kinachoendelea katika uhalisia katika halmashauri zetu Wakaguzi wa Ndani wamegeuka kuwa Menejimenti za Halmashauri na wenyewe badala ya kuwa wakaguzi. Ukienda kwenye SMT ambayo Mkurugenzi wa Halmashauri au kwenye Taasisi Mjumbe mmojawapo ni Mkaguzi wa Ndani ambaye anatakiwa amkague huyo Mkurugenzi wa Taasisi au Mkurugenzi wa Halmashauri ambaye ni bosi wake, hivi unaweza ukamkagua bosi wako na ukatoa taarifa ya kumkaanga ni jambo gumu sana, matokeo yake ni nini? ndiyo maana tunapokuwa kwenye vikao vya Kamati ya Fedha au Mabaraza ya Halmashauri anapotuhumiwa DT unashangaa Internal Auditor anasimama kumtetea DT, kwa utaratibu huu itakuwa ngumu kwenda.

Mheshimiwa Naibu Spika, niiombe Wizara hawa watu muwakumbushe majukumu yao, kutumia vyuo mbalimbali mlivyonavyo chini ya Wizara yenu muwajengee uwezo kama ambavyo la wiki iliyopita Mheshimiwa Hasunga alichangia mvitumie hivi vyuo, wakumbushwe majukumu yao, wao ni waangalizi wa Serikali wanawasaidia kuangalia wale ni watchdogs, lakini siyo sehemu ya operations katika Halmashauri zetu.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo jingine kuhusu Wakaguzi wa Ndani, sasa hivi tunasema tuna e-government tunaendesha mfumo wa Serikali kimtandao, unakuta una Mkaguzi wa Ndani mmoja ambaye basically ni accountant namna gani ataenda kukagua hii mifumo ya Halmashauri ya kukusanya fedha ya kieletroniki? Sasa niwaombe Wizara kama mtaomba kibali cha kuajiri tuna halmashauri 185 kuna watu wanaitwa Information System Auditors hiyo Idara ipo pale katika Ofisi ya CAG. Katika Ofisi ya AG pia muiweke muajiri watu ambao wanajua mifumo waende kukaa na kukagua mifumo ili kuwarahisishia wale Accountants katika suala la Ukaguzi wa Mapato ya Serikali na Matumizi ya Serikali, hiyo ni sehemu ya kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sehemu ya pili baada ya sheria kufanyiwa maboresho kuna kitengo kilianzishwa kinaitwa vitengo vya usimamizi vihatarishi (Risk Management Unit), hivi ni vitengo ambavyo vimetengenezwa kwa ajili ya kuangalia viashiria vya viahatarishi Serikalini katika utekelezaji wa mipango yetu kwa kila robo mwaka, naomba pia mviimarishe mwajiri watu au waliopo wapewe mafunzo wajengewe uwezo waweze kuisaidia. Vitengo hivi vinaenda sambamba na vitengo vya Ukaguzi wa Ndani na kila robo mwaka wanaandaa taarifa inapitiwa na Kamati za Uongozi na kuangalia vihatarishi vitakavyokwamisha operations za Taasisi za Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ni Halmashauri au Idara zinazojitegemea wanatoa maelekezo na kusema kwamba safari hii tuna Corona tutakwamisha kwa namna moja, mbili, tatu. Safari hii tuna mvua nyingi kwenye ujenzi wa barabara tutakwamishwa na moja, mbili, tatu. Mviangalie hivi vitengo mviimarishe mvijengee uwezo vitaweza kutusaidia sana katika kufikia malengo ya bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tunakwenda kitengo cha tatu au taasisi ya tatu ni Ofisi ya CAG, Ofisi ya CAG ipo chini yenu Wizara ya Fedha, sasa unapoongea Ofisi ya CAG ndiyo inaleta watu wanaitwa External Auditors wanapoenda kufanya ukaguzi kwenye taasisi nyingine. Hawa watu wanapofika wanafanya mnasema zile entrance meeting na ukitaka kuondoka unafanya exit meeting, lakini ukifanya uchunguzi kwa kiwango kikubwa wana - collide na Wakuu wa Taasisi katika suala la uandaaji wa hizi hati.

Mheshimiwa Naibu Spika, unakuta taasisi imepewa hati safi lakini ukifuatilia matumizi yake siyo mazuri, wanaenda wanakaa mezani wanajadiliana kabla hawajafanya exit meeting wanaacha kitu kidogo wanaongezewa pale mlungula wanaondoka ripoti inatoka safi, fanyeni uchunguzi mjiridhishe katika hili wizara. Kwa hiyo, katika upande wa udhimabiti wa fedha za Serikali na Usimamizi wa Fedha itawasaidia sana mkitumia haya maeneo matatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mchango namba mbili, eneo namba mbili nataka kuchangia Utumishi wa Umma. Wakati nachangia Mpango wa Maendeleo ya Taifa nilisema Utumishi wa Umma ni nyenzo muhimu sana katika kufanikisha mipango hii. Niwapongeze Serikali, niwapongeze Wizara ya Utumishi, TAMISEMI na nyinyi Wizara ya Fedha kwa kuja na motisha mbalimbali mlizotoa kwa watumishi wetu wa umma, hongereni sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto nyingine ambayo ninatamani niichangie kuna eneo la kuwajengea uwezo Watumishi wa Umma. Tunayo Sheria ya Utumishi wa Umma Na. 8 ya mwaka 2002, Kanuni za 2013 na Kanuni za Kudumu za 2019 hapa changamoto ipo wapi, wanapoandaa mafunzo kuna mipango ya mafunzo ya muda mrefu na mafunzo ya muda mfupi ni kichaka kingine ambacho Maafisa Utumishi wanakitumia kunyima haki za Watumishi wa Umma. Wakati mwingine mtumishi anahitaji kujisomesha, kujiendeleza na kujijengea uwezo lakini unaambiwa haupo kwenye mpango wa mafunzo, sasa huyu mtu anajisomesha kwa hela yake sasa kwa nini unamzuia? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuangalie tuweke utaratibu kama ambavyo inasema Sera ya Mafunzo ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2013 watu hawa wanapohitaji kujiendeleza kwa sababu ni lengo ni kuboresha na kuongeza ufanisi katika kazi, wapewe nafasi ya kwenda kusoma wakirudi waendelee. Kwa sababu Serikali ina fedha ndogo na uwezo wa kusomesha kila mtumishi kadri ya muda wake wa kusoma haiwezi, mtu anapotaka kwenda kujisomesha apewe ruhusa akasome kwa sababu atakaposoma ni faida kwa Serikali yetu, tuepukane na haya matusi wanayotukanwa watalaam wetu kwamba hawana uwezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mtu amekaa miaka kumi na tano hajawahi hata kupata hata refresher course unadhani atakuwa na uwezo mzuri wa kufikiria? Ndiyo maana hata huko kwenye vyombo vya ulinzi na usalama ukikaa miaka mitatu, minne unapigwa refresher course maana yake ni kwamba kuna vitu vipya hata computer zina software, unasikia tunatoka Window 7 tunaenda Window 8, tunaenda Window 9. Kwa hiyo Serikali hili mliangalie katika kuboresha hili eneo, watumishi wakiongezewa ujuzi litatusaidia sana katika kufikia haya malengo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana, naunga mkono hoja. (Makofi)