Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Mrisho Mashaka Gambo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arusha Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nami namshukuru Mungu kwa kupata nafasi niweze kuchangia bajeti hii ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nitumie fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa na kazi nzuri sana aliyoifanya hasa kuchukua maoni mengi ya Wabunge na kuyaingiza kwenye Mpango wa Serikali, nampongeza pia Waziri wa Fedha kaka yangu Mwigulu Nchemba pamoja na Naibu Waziri wa Fedha Mheshimiwa Injinia Masauni kwa kazi kubwa na nzuri sana ambayo wanaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo nitajikita kwenye mambo mawili la kwanza ni kuhusu utalii. Sekta ya Utalii imesahaulika sana. Bajeti hii imeangalia mambo mengi sana, lakini nataka nikuhakikishie haijatoa ahueni yeyote kabisa kwenye sekta ya utalii. Wizara ya Maliasili na Utalii ni kana kwamba vile haijui dunia imetoka wapi, ipo wapi na inakwenda wapi.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia taarifa zilizopo kutokana na changamoto za Corona duniani tunaambiwa kwamba uchumi umekuwa na mdororo hadi kufikia asilimia 3.3 ambayo ni hasi kutoka asilimia 2.8 ya mwaka 2019. Lakini tunaambiwa kwamba Pato la Taifa limeshuka kutoka asilimia 7 mpaka asilimia 4.8 mwaka 2019/2020. Tunaambiwa pia mchango wa utalii umeshuka kutoka asilimia tuliyoizoea 17.5 mpaka asilimia 10.7 kwenye Pato la Taifa. Tunaambiwa pia mapato yamepungua na taarifa imetolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii kutoka bilioni 584 mpaka bilioni 89 ambayo ni sawasawa na asilimia 15 ya malengo yaliyowekwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia mapato ya mwaka 2019/2020 yalikuwa bilioni 252 kipindi kama hiki leo bilioni 44.8 kwa taarifa zao wenyewe Wizara ya Maliasili na Utalii. Tunaambiwa pia idadi ya utalii imepungua kutoka mwaka 2019/2020 walikuwa milioni moja elfu hamsini na mbili mia tisa arobaini na tatu (1,529,443) na sasa hivi ni watalii laki nne na kumi na nne na thelathini (414,030).

Mheshimiwa Naibu Spika, tunafahamu kwamba changamoto kubwa zimejitokeza hasa kwenye ajira, ukienda Arusha hoteli nyingi zimeathirika, Tour Operators wameathirika, waongoza utalii wameathirika, karibu sekta zote madereva, wahudumu wa hoteli, wapagazi wale, wapiga mahema, wapishi, staff wa maofisini wapo hoi kwa sababu hakuna wageni. Tunajua, Waziri anajua, Waziri wa Fedha anajua, Waziri wa Utalii anajua, lakini mambo yanavyokwenda kana kwamba wapo dunia nyingine tofauti na sisi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kinachonishangaza pamoja na matatizo yote haya solution waliyokuja nayo Wizara ya Maliasili na Utalii na Serikali yetu hii ni kuongeza tozo. Utaona tumeongeza dola 10 kipindi cha high season kwenye hifadhi ya Serengeti na hifadhi ya Nyerere, lakini tumeleta tozo nyingine mpya inaitwa land base rent kwa watu ambao wanakuwa na seasonal camp dola 2,000, ukiwa na permanent tented camp dola 20,000, ukiwa na lodge dola 50,000 ndani ya hifadhi, Serengeti mle ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati mtalii anapokuja Tanzania akifika airport pale analipa VISA, akitoka pale anapanda gari ya utalii anachangia mafuta pamoja na masuala mengine, akienda kwenye hoteli akilala analipa ambapo Serikali inapata fedha, akienda kwenye park analipa park fee, akitoka pale akilala ndani ya hifadhi analipa kitu kinaitwa concession fee ambayo kila siku anayolala ndani ya hifadhi analipa dola 50 bila VAT.

Mheshimiwa Naibu Spika, leo wamekuja wenzetu maliasili na utalii na tozo nyingine, eti ukitengeneza seasonal camp umechukua hema lako umeliweka mle ndani ya hifadhi dola 2000, ukichukua hema lako kama ni kwa muda fulani, permanent dola 20,000, umejenga lodge ume-invest wanakupiga dola 50 hasa ile concession fee ni ya nini? kwa hiyo, unaona kabisa Wizara ya Maliasili na Utalii wasipoangaliwa hawa wanakwenda kuiua kabisa sekta hii wanakuwa ni Corona namba mbili katika nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nina ushauri kwenye jambo hili Serikali ikaliangalie jambo hili vizuri hizi tozo zisitishwe, kwa sababu kwanza hazijaanza kutozwa, zitaanza kutozwa kuanzia tarehe Moja mwezi wa Saba mwaka huu inamaana bajeti hii ikipita. Tunavyozungumza leo hata wakisitisha Serikali haijapata hasara yoyote kwa sababu mambo haya ni mapendekezo yote wamekuja nayo Wizara ya Maliasili na Utalii. Ndiyo maana nilisema kwenye mchango wangu uliopita tunazo hifadhi 22, hifadhi ambazo zinazalisha ni tano peke yake, hifadhi 17 hazina uwezo wa kuzalisha kiasi cha kujiendesha, badala ya Wizara ya Maliasili na Utalii kuja na mpango mbadala kila siku wanafikiria kuongeza tozo Serengeti, kuongeza Nyerere na masuala mengine, ukiwauliza ni kwa sababu gani wanasema tunataka tuzuie congestion! eti tukiongeza tozo watalii wataogopa kwenda hifadhini kwa hiyo hifadhi zitabaki salama, halafu leo wanakuja na maelezo hapa tunataka tuongeze watalii kutoka idadi ya sasa mpaka milioni tano, unashindwa kujua hata haya mambo wanayo yazungumza wanayatoa wapi? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili jambo ni very serious naiomba sana Serikali kwa sababu tunaye Rais msikivu, Rais ambaye ameamua kuleta ahueni kwenye sekta binafsi, Rais ambaye anafahamu hawa sekta binafsi, kuna hotel pale Karatu, walikuwa zamani kabla ya utalii hotel ya dola 200 leo mtu ameshusha mpaka dola 100 ili kuweza kuvutia wageni waje, Serikali hii inakwenda kuongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nadhani hili jambo ni vizuri Bunge lako Tukufu na Serikali yetu waende wakaliangalie watu wa Maliasili na Utalii wakumbushwe kwamba kazi yao wao ni kuangalia interest za Serikali pia kuangalia na interest za wawekezaji kwa maana ya sekta binafsi, lakini siyo kuangalia Serikali peke yake.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni kuhusu wenzetu hawa wa bureau de change, tumepata shida kubwa sana Mkoa wa Arusha, tumeteseka na ma-task force kila siku yanashindana kuja tu pale, baadaye wamekuja na mambo haya ya bureau, na watu wa bureau hawa kuna mchezo wanaucheza ambao sijui hawa watu wa Serikali kuna watu wao wanataka wafanye hii biashara? Maana ukiangalia mwaka 2015 mtaji wa mtu wa bureau ulikuwa milioni 40, wakaja mwaka 2015 hadi kufika mwaka 2017 wakaongeza ikaja milioni 100, kufika 2018 Mei wakapeleka milioni 300, baadaye wakaona sasa kila wakiongeza wale wanafanya biashara, kila wakiongeza wanafanya biashara, baadaye wakaamua kuvamia na kwenda kuwapora! Wakapora pesa zao, wakapora magari yao, wakapora hati zao za nyumba, wakapora viwanja wamewaacha hoi taabani.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mrisho Gambo kengele imegonga.

MHE. MRISHO M. GAMBO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana lakini ombi letu kwamba warudishiwe leseni, warudishiwe fedha zao, gharama zipungue na assessment za kienyeji zile zifutwe ili watu wafanye biashara Serikali ipate kodi na fedha zake.(Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. (Makofi)