Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Neema William Mgaya

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia bajeti hii. Kwanza kabisa nianze kwa kumpongeza Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuonyesha upendo mkubwa kwa Watanzania, ukisoma mapendekezo ya bajeti hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha upendo kwa makundi mbalimbali ya wananchi wa Tanzania kwa kupunguza tozo kandamizi mbalimbali katika makundi mbalimbali wakiwemo wakulima, wafanyabiashara, kama bodaboda, kwa kupunguza tozo ya faini kutoka shilingi 30,000 mpaka shilingi 10,000.

Mheshimiwa Naibu Spika, kipee kabisa nampongeza Rais, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa aliyoifanya jana kwa maelekezo mazuri na maamuzi mazuri aliyoyatoa kuhusiana na mradi mkubwa wa Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Naibu Spika, mradi wa Liganga na Mchuchuma kuna takribani tani milioni 128 za chuma pamoja na madini mengine. Mradi huu ukianza kutekelezwa utakwenda kutupatia malighafi ya chuma ambayo itatumika kutengezea nondo kwenye viwanda vyetu vya nondo, mabati, viwanda vya vifaa vya kutengeneza madaraja na viwanda vya vifaa vya kutengeneza reli. Kwa mradi huu, utatachochea uanzishwaji wa viwanda vingi vinavyotumia malighafi ya chuma. Sina shaka SGR aliyokwenda kuifungua kuanzia Mwanza huenda ikatumia malighafi ya chuma inayotokana na Liganga na Mchuchuma kama tutatekeleza vizuri kufuatana na Mheshimiwa Raisi alivyosema.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile nampongeza Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu kwa sababu ameona kwamba mradi huu wa Liganga na Mchuchuma tutakwenda kuokoa takribani shilingi bilioni 640 ndani ya mwaka mmoja kwa muda wa miaka 30 ya uhai wa mradi huu wa Liganga na Mchuchuma. Hivyo natoa pongezi nyingi sana kwa mama. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile hiyo ni sambamba na kuzalisha ajira 35,000. Hii pesa tutakayoenda kuokoa ni shilingi bilioni 640 kila mwaka ndani ya miaka 30. Itasaidia miradi ya maendeleo ndani ya nchi yetu. Wale watakaokwenda kuajiriwa, hao watu 35,000 watatusaidia pia katika kulipa kodi na kuendelea kupata mapato na kuweza kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri pamoja na timu yao nzuri ya Wizara ya Fedha. Naunga mkono pendekezo waliloleta la kutatua changamoto ya fedha ambazo zilikuwa zikirudi Hazina kila mwisho wa mwezi wa Sita na kuzifanya fedha zile sasa ziwe zinaenda kwenye akaunti ya amana ili ziweze kuendelea kutekeleza miradi ambayo ilikuwa haijamalizika. Hii itasaidia kuchochea kumalizika kwa miradi mapema na vilevile kwa ufanisi mkubwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimekuwa nikuzungumza mara kwa mara umuhimu wa zao la parachichi ndani ya Bunge hili la Tanzania. Kwa sababu Parachichi sasa hivi ni green gold, ni zao ambalo linakua kwa haraka. Takribani mikoa 12 ikiwemo na Mkoa wangu wa Njombe tunalima zao hili la parachichi. Tunawashukuru sisi wakulima wa hot culture, wa mbogamboga, kwa pamoja na maua.

Mheshimiwa Naibu Spika, ndani ya mbogamboga tunakuta hili zao la parachichi. Tunawashukuru kwa kutoa kodi ya vyumba vya ubaridi (cold room). Tunawashukuru sana, kwani hii itatusaidia sisi wakulima wa mazao ya mbogamboga pamoja na maua hususan wakulima wetu sisi ambao wanalima parachichi kuhifadhi mazao yale, kwa sababu mazao haya ya mbogamboga pamoja na maua, biashara yake kubwa ni kwa ajili ya kusafirisha nje ya nchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa kutoa kodi ina maana sasa wakulima wataenda kutengeneza vyumba hivi vya ubaridi kwa wingi na kuweza kuhifadhi mazao hay ana kuweza kuyasafirisha nje ya nchi yakiwa na ubora na itasababisha kuongeza pato la Tanzania. Kwa sababu bidhaa zetu zitakuwa zinafika kwa mlaji zikiwa bora. Vilevile itawajengea imani kwa mazao ya mbogamboga na maua yanayotoka Tanzania na kuweza kuongeza wateja wengi ambao watakuwa wananunua mazao kutoka nchini kwetu Tanzania na kuweza kuongeza pato la Taifa.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimalizie kwa kusema, hakuna kitu kilichokuwa kinaniudhi na kilichokuwa kinanikosesha raha na kilikuwa kinaniuma sana kama kutoza kodi mara mbili (double taxation). Wale wafanyabiashara wa Zanzibar ambao walikuwa wanakuja kununua bidhaa huku Tanzania Bara kwa kweli tulikuwa hatuwatendei haki. Isitoshe sisi Watanzania Bara na Tanzania Zanzibar, tuna mahusiano, tumeoleana, kwa hiyo, tuna undugu. Unaweza ukaenda kwa mkwe wako; kwa mfano, kama mimi, naweza nikafika Tunguu kule Zanzibar kwa wakwe zangu wakaniambia tunakupa TV hii umpelekee mjukuu wetu. Nafika pale custom tena nalipishwa ushuru kweli! Hapana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono asilimia mia moja, tozo hii ya kulipa mara mbili mbili kwa kweli mmewatendea haki Wazanzibar. Wazanzibar ni ndugu zetu, ni jamaa zetu, ni marafiki zetu, ni wakwe zetu; Zanzibar na Tanzania Bara ni Tanzania moja. Kwa hiyo, kwa kuondoa tozo hizi mbili mbili itatusaidia kuendelea kuujenga Muungano wetu wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru. Naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)