Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Rose Cyprian Tweve

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote nakushukuru sana na kumpongeza Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kaka yangu Mheshimiwa Mwigulu kwa namna ambavyo amewasilisha bajeti hii hapa Bungeni ili nasi sasa tuweze kutoa mapendekezo na maoni yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kipekee kabisa nachukua fursa hii kumpongeza Rais wetu, mama yetu Mheshimiwa Samia Suhulu Hassan kwa namna ambavyo amesisimama imara kuendelea kuliongoza na kulisimamia Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ni miongoni mwa nchi chache ambazo zilifanikiwa kupiga hatua kubwa ya kupanda kiuchumi ingawa tulipitia changamoto kubwa sana kidunia, lakini tuliweza kufika uchumi wa kati. Sasa ni jambo jema na hii haina guarantee kuwa tutaendelea kuwepo hapo, tunaweza kushuka au kupanda zaidi. Ni matamanio yangu na Watanzania wengine kuwa tutaweza kupiga hatua kubwa zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama Taifa tuna jukumu kubwa la kuhakikisha tunawekeza ili uchumi wowote uweze kupiga hatua, lazima tuwekeze na eneo kubwa ambalo ningependa kuweka msisitizo ni kuhakikisha tunawekeza kwenye rasilimali watu.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais yetu Samia Suluhu Hassan alipokuwa akiongea hapa tarehe 8 mwezi wa Sita alisisitiza sana umuhimu wa kuhakikisha tunaendelea kuwekeza kwenye rasilimali watu na akaenda mbali zaidi kuisihi sekta binafsi kuhakikisha wanaendelea kuchangia ile 4% ya gross pay kuendelea kuboresha na kukuza ujuzi hasa wa vijana wetu. Hii hiko kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwaka 2006 Bunge lako Tukufu lilipitisha Sheria ya Mafunzo ya Elimu ya Ufundi Stadi kuhakikisha hawa wenzetu sekta binafsi waendelee kuchangia vipaji vya vijana wetu hapa nchini. Hapa ndipo ambapo kidogo pana changamoto. Namwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha twende sasa na mahitaji na mabadiliko ambayo nchi hii inataka.

Mheshimiwa Naibu Spika, sheria hii kile Kifungu cha 15 kinasema two third ya yale makusanyo yaende Serikali Kuu na one third ilikuwa inaelekeza kuwa iende kuboresha miundombinu tu ya hivi vyuo vya ufundi na siyo kufadhili elimu yetu. Hapa ndipo ambapo pamekuja na changamoto. Sasa namwomba Mheshimiwa Waziri, kwa sababu hii pesa ambayo inakusanywa ililenga kuhakikisha inaendeleza ufundi na ujuzi wa vijana wetu. Tuje na mapendekezo kama ambavyo amefanya marekebisho ya sheria na tozo mbalimbali, it is a high time tupitie sheria hii, tulete hapa tufanye mabadiliko ili tuendane na uhitaji na kuendelea kukuza uchumi wa Taifa hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, as of today tuna vijana zaidi ya 357 ambao wako vyuo na kama 201,000 ni vijana wa elimu ya vyuo vikuu na vijana 157,000 wako kwenye vyuo vya ufundi, sasa Mheshimiwa Waziri wa Fedha ulipokuja kuwasilisha bajeti hapa, tumeonyesha kabisa nia njema ya kuhakikisha kupeleka fund kwenye vyuo vikuu. Tulipopitisha bajeti iliyopita tumeongeza kutoka shilingi bilioni 464 mpaka shilingi bilioni 500 ambayo itaenda kwenye vyuo vikuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa na sheria hii ilivyo hapa sasa hivi, ambayo hiyo two third bado inakwenda Serikali Kuu, nilikuwa nakuomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha tulete mabadiliko ya sheria hapa ili tutengeneze mfuko maalum kwa sababu Tanzania ya Viwanda sasa hivi inahitaji vijana ambao watakuwa na ujuzi na ubunifu ili tuweze kupiga hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili sasa kwa sababu hawa wenzetu wa vyuo vikuu wana mfuko huu wa bodi ambao unawasaidia. Hawa vijana wafundi nao tuwatengenezee mfuko wa mikopo wa vyuo vya ufundi kwa sababu kianzio kipo. Kutoka kwenye hii ongezeko ambalo wenzetu wanalilipa, tuanzishe huu mkopo ili hawa vijana waweze kuutumia. (Makofi)

Mheshimwia Naibu Spika, wenzetu Rwanda wamepiga hatua kubwa sana. Vyuo vyao vya Ufundi wamevi-brand. Mtoto anapotoka pale, kama anajifunza ufundi, anatoka na cherehani; kama anataka kwenda makenika anakuwa na tool box yake ambayo tayari itamwezesha yeye kuanza kufanya kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri wa Fedha, kama wenzetu wameweza kufanikiwa, nina uhakika tukiwekeza huko sisi Tanzania tutakuwa na uwezo wa kupiga hatua kubwa sana. Siyo tu kukua kwa asilimia sita au saba, tunaweza tukaenda hata double digit kama tukiweka nguvu kuhakikisha hawa vijana wetu wa Kitanzania wanaendelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba sasa ninukuu maneno ya mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan alipokuwa anahitimisha hotuba yake ambayo aliifanya hapa Dodoma ile tarehe 8 mwezi wa sita. Aliongea kwa kusisitiza sana kuwa kwa heshima zote anaomba sisi kama Watanzania tumuunge mkono na tumsaidie. Kwa bajeti hii ambayo umeileta Mheshimiwa Waziri wa Fedha inaonyesha nia njema ya Mheshimiwa Rais wetu, mama yetu Samia Suluhu Hassan kutaka Watanzania tufikie yale malengo ambayo tumejiwekea.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge na Watanzania twende tukamuunge mkono Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kuhakikisha tunalifikisha Taifa letu pale tunapotakiwa lifike.

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. ROSE C. TWEVE: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)