Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Hawa Mchafu Chakoma

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali. Napenda kumpongeza Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, kwa kuapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nipende kuipongeza Serikali yake kwa kuja na bajeti nzuri ambayo ina mguso kwa Watanzania wote. Katika bajeti ya kwanza kabisa ya Rais Samia Suluhu Hassain imefanikiwa kugusa makundi yote katika jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikianza na kundi la wakulima; zipo tozo pamoja na ushuru ambazo zimeondolewa katika mapendekezo haya ya bajeti. Nia, lengo na kusudi ni kuwawezesha wakulima wetu waweze kulima kilimo chenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ukisoma mapendekezo ya bajeti, unakuta kuna lengo ama dhamira ya kuongeza tija kwa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi. Sambamba na hilo pia wanakusudia kutafuta masoko kwa ajili ya mazao hayo ya wakulima yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiangalizia kundi lingine ambalo ni kundi muhimu sana, ni kundi la wafanyakazi ama watumishi. Tutakubaliana sote hapa Serikali inapata kodi yake ya uhakika katika vyanzo vyake vyote vya kodi, kodi ya uhakika inatoka kwenye kundi la wafanyakazi. Ni kodi ambayo haina kuvutana mashati, ni kodi ambayo haina kuifukuzia, yaani ipo inapatikana kiurahisi kabisa. Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais Samia kwa kuona umuhimu wa kupunguza kodi ya pay as you earn kwa watumishi wa Taifa hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwa muda mrefu sana takribani miaka mitano ama miaka sita, watumishi wa Taifa hili wamekuwa wakinungunika juu ya masuala mazima ya kupanda daraja ama ya kupanda vyeo. Namshukuru sana Mheshimiwa Rais Samia katika bajeti yake ya kwanza kabisa kukusudia kutenga bilioni 449 kwa ajili ya kupandisha vyeo watumishi 92,619.

Mheshimiwa Naibu Spika, tutakubaliana ni haki ya msingi ya watumishi kupanda madaraja ama kupanda vyeo na unapokuwa unawapandisha vyeo watumishi tafsiri yake ni kwamba …

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Getere natumaini unataka kutoa taarifa na siyo kuchangia, Mheshimiwa Getere.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli nataka kutoa taarifa kumpa mzungumzaji anayeongea. Alipozungumza ile malipo ya pay as you earn, nataka kujua tu anapoendelea kwenye mchango wake majibu yake yaje yapatikane kwamba asilimia iliyotolewa ni ipi, kuna watu wa kundi la kwanza ambao wanamshahara wa 270 mpaka 540 ambao wana asilimia 9.0, wanakwenda
mpaka asilimia 10...

NAIBU SPIKA: Sasa hebu ngoja tuelewane hiyo ni taarifa au unamuuliza swali? Kwa sababu yeye hana uwezo wa kukujibu wewe.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Naibu Spika, nataka kuchangia tu, watakavyompa majibu watuambie kwamba...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Hawa Mchafu, endelea na mchango wako.

Waheshimiwa Wabunge, Mbunge akiwa anaenda na mchango wake hivi, ukimkatisha njia yaani ile namna anavyoenda unamchelewesha. Kwa hiyo usimame kutoa taarifa kama hasa unataka kuongeza kwenye jambo ambalo unaona yeye hajamaliza vizuri pengine hoja yake. Sasa yuko katikati ya jambo, wewe umeingia hapo hata point yake hajamaliza bado.

Mheshimiwa Hawa Mchafu.

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Naendelea kwa kusema kwamba tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa kutenga hizo bilioni 449 kwa ajili ya kupandisha vyeo watumishi wa Taifa hili. Nilikuwa nasisitiza kwa kusema kwamba mtumishi yoyote ambaye ana haki anastahili kupanda cheo, unapompandisha cheo unampa moraly na ari ya kufanya kazi kwa ufanisi, jambo ambalo litaenda kuchochea na kuchagiza kodi iweze kupatikana zaidi kwa mustakabali wa maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi ambalo Rais Mheshimiwa Samia amelifanya na limenigusa kwa namna moja ama nyingine nilikuwa mtumishi wa Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii. Kwenye Bunge lililopita nilikuwa nikiwakilisha wafanyakazi. Rais, Mheshimiwa Samia amefanya jambo kubwa sana kudhamiria kulipa madeni ya hifadhi ya jamii.

Mheshimiwa Naibu Spika, hiki alichokuja nacho hapa ni mwarobaini wa kuhakikisha tunatenga fedha za bajeti na zinaenda kutumika katika utaratibu wa hati fungani ili kwenda kulipa madeni ya hifadhi ya jamii. Hii nini maana yake? Ni kwamba hifadhi ya jamii ilikuwa na madeni ya muda mrefu sana na madeni ambayo yalikuwa yakienda yakikua katika mifuko yetu ile mitano.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kama Serikali imeamua na kudhamiria kufanya hivyo, wakitenga fedha kwenye bajeti na kupeleka kwenye hati fungani na baadaye kulipa kulipa madeni kwa Mfuko tuliokuwa nao sasa wa PSSSF, tafsiri yake ule Mfuko unaenda kukuwa, Mfuko ule unaenda kuwa na ukomavu, sasa kile kilio cha wastaafu kinaenda kumaliza na mapendekezo haya. Ile kauli mbiu ya Mfuko wa LAPF iliyokuwa ikisema mstaafu wa leo analipwa kesho, kwa huu mwarobaini aliokuja nao mama Samia ndiyo inaenda kutekelezeka kwa vitendo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo hili lilikuwa likipigiwa kelele sana na ndugu yangu Ester Bulaya pamoja na Mheshimiwa Halima Mdee kwenye Bunge lililoisha na Bunge hili. Hivyo nitawaomba sana mapendekezo haya yakipita tutakapofika kupiga kura siyo dhambi wakapiga kura ya ndiyo kumpongeza Rais Mheshimiwa Samia Suluhu Hassain kwa sababu ametii kiu yao ya muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nitaomba sana Mheshimiwa Mwigulu akija atufafanulie jambo moja, kulikuwa na watumishi waliokuwa wanafanya kazi Serikali Kuu ambao kimsingi walistaafu kabla ya mwaka 1999, watumishi wale Serikali ilisema walipwe mafao yao na Mfuko wa PSSSF. Sasa wale walilipwa lakini lile deni halikulipwa ambalo linajulikana kama pre-1999 na muda wote ulikuwa tukijadili madeni ya hifadhi ya jamii pre-1999 tulikuwa tunaijadili separate. Kwa hiyo nataka kujua kwenye hii dhamira waliyoileta ya kutaka kutenga hii hati fungani kulipa madeni ya hifadhi ya jamii na pre- 1999 iko included. Kama watakuwa wamefanya hivyo Mheshimiwa mama Samia atakuwa amemaliza kabisa kilio cha Trade Union, cha wafanyakazi, cha watumishi, pamoja na wastaafu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kundi lingine ambalo linaguswa katika bajeti hii ni kundi la vijana na akinamama. Bajeti inakusudia kwenda kuboresha uwezeshaji wa wananchi kiuchumi. Tunaposema kuwawezesha wananchi kiuchumi ni kundi linalokusudiwa hapa ni akinamama pamoja na vijana na juzi alivyotuita wanawake wa Taifa hili alizungumza ana dhamira ya kuhakikisha anataka kuhakikisha haya majukwaa ya uwezeshaji wananchi kiuchumi. Kwa maana hiyo hapa wanawake watanufaika na vijana watanufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kundi lingine ambalo linanufaika kwenye bajeti hii ni kundi la wafanyabiashara, kundi la wawekezaji hususani wenye viwanda, ukiangalia bajeti kwamba Mheshimiwa Waziri anakusudia kuondoa sharti la kuweka dhamana la asilimia 15 ya ziada ya ushuru wa forodha iliyorejeshwa kwenye sukari ya matumizi ya viwandani.

Mheshimiwa Naibu Spika, hili ni jambo kubwa sana, wakati tupo hapa Bunge lako linaendelea walikuja wadau wa viwanda chini ya mwavuli wa CTI. Katika mambo waliyokuwa wanayalalamikia, liko hili la kuondoa hii tozo asilimia 15, lakini lipo lile la kuondoa ama kupunguza tozo ya mabango ambayo kimsingi nadhani imependekezwa ishuke kutoka asilimia 15 mpaka asilimia 10, if I am not mistaken. Napenda sana kuipongeza Serikali na kama hivyo ndivyo basi kazi imebaki kwao wenzetu wenye viwanda kuhakikisha wanaongeza uzalishaji, wanaongeza ajira, lakini pia wanalipa kodi stahiki kwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba nimwonyeshe Mheshimiwa Waziri Sehemu ambayo kimsingi hajatolea jicho, pale tunaweza tukapata mapato ama tukapata kodi. Tukizungumzia uvuvi wa wa Bahari Kuu, tukizungumzia kule deep sea, sisi kama nchi hatuna meli itakayoweza kwenda kuvua kule, lakini sisi kama nchi hatuna bandari ya uvuvi kwa utaratibu meli kubwa kutoka nje zinalipa tozo kidogo kwa Wizara wanapewa kibali wanaenda wanavua. Wanavua tones and tones za samaki ambazo zinapatikana katika eneo la Jamhuri ya Muungano, ambayo ni bidhaa ya Jamhuri ya Muungano.

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi bidhaa ile inayopatikana katika mipaka ya bahari ya Jamhuri ya Muungano haikatwi kodi. Kwa hiyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri, TRA waone namna bora ya kufanya makadirio ili tuweze kutoza kodi zile tozo tunazotoza ili kuwapa kibali wakavue, ni maduhuli tu yale madogo madogo, lakini tuweke utaratibu wa kisheria ili tuweze kutoza kodi hao samaki wanaoweza kwenda kuuzwa huko duniani.

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, ukiangalia katika ukurasa wa 41(e) cha hotuba ya Mheshimiwa Waziri anasema anakusudia kuongeza ushuru wa forodha kutoka asilimia 25 mpaka 35 kwenye bidhaa ya marumaru. Bidhaa za marumaru…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. HAWA M. CHAKOMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nimalizie kidogo. Kwa bidhaa hizo za marumaru zinazotoka nje, Mheshimiwa Waziri kuongeza tozo ni sahihi kabisa, kwa sababu anakusudia kulinda viwanda vyetu vya ndani. Tunapozungumzia suala zima la viwanda, mkoa unaoongoza kwa viwanda ni Mkoa wa Pwani; na ukizungumzia masuala mazima ya viwanda vya tyles, unavikuta Mkuranga, Mkiu, Chalinze, Bagamoyo na Kisarawe. Kwa kufanya hivyo, atavilinda viwanda hivi, wataweza kuzalisha, kulipa kodi na kutoa ajira kwa Watanzania.

NAIBU SPIKA: Ahsante sana.

MHE. HAWA M. CHAKOMA Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)