Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Kwagilwa Reuben Nhamanilo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa hii adhimu nipate kuchangia katika bajeti ya nchi yetu kwa mwaka huu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nianze kwa kuunga hoja mkono hoja zote mbili zilizowasilishwa ya kwanza ya Waziri wa Fedha na ile yetu ya Kamati ya Bajeti. Nimpongeze sana sana Mheshimiwa Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa kutuletea bajeti yenye maono makubwa kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii imebeba mahitaji ya Watanzania, bajeti hii imebeba matumaini ya Watanzania, bajeti hii imebeba maoni ya Wabunge, bajeti hii imebeba Ilani ya Uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi, lakini bajeti hii imebeba dira ya Taifa letu, bajeti hii imebeba maono ya Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan. Nasema hivyo kwa sababu bajeti hii inakwenda kutupelekea barabara zetu zote mijiji na vijijini Mheshimiwa Rais kupitia bajeti iliyowasilishwa hapa anatengua Sheria ya Usalama barabarani ili tuweze kupata Bilioni 322 kwa ajili ya barabara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Rais amebeba maono makubwa kwa Taifa letu kwasababu kupitia bajeti hii tunapeleka maji safi na salama kwa nchi nzima, kupitia hiyo ameamua kutengua Sheria ya Posta na Mawasiliano Sura Na. 306 ili tuweze kukusanya Trilioni 1.3 kwa ajili ya kuyafanya haya. Mama yetu amebeba maono makubwa kupitia bajeti hii kwa sababu anakwenda kufanya jambo ambalo limeshindikana kwa miaka mingi bima ya afya kwa kila Mtanzania, Mheshimiwa Rais anakwenda kutekeleza miradi yote ya kimkakati ikiwemo mradi maarufu ambao mimi huwa ninasimama hapa kuuongelea kila mara mradi wa SGR unakwenda kutekelezwa kupitia bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bajeti hii inakwenda kututengenezea miundombinu ya elimu, kwenye hili upande wa elimu ya juu kupitia bajeti hii watoto wote wa Kitanzania ambao walikuwa wameshapata udahili kwenye vyuo na wakakosa nafasi ya kusoma kwa sababu ya fedha, bajeti hii inakwenda kuwarudisha katika vyuo. Kwa hiyo, bajeti hii ni ya Watanzania na bajeti hii ni ya kwetu na tunakwenda kuijenga nchi yetu kwa kujifunga mikanda wenyewe kama ambavyo Waziri wa Fedha alituambia hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Serikali ukiacha maeneo haya mapya ambayo yametengua sheria nne na yakatupatia Trilioni mbili, TRA ina department Nne ukiangalia hizi department kuna moja ya muhimu sana inaitwa department ya customs na excise hii inakusanya asilimia 38 ya mapato yote ambayo TRA inakusanya yanatoka kwenye hii department hii inatafsiri kwamba kwa lengo tulilojiwekea la kukusanya mapato ya ndani Trilioni 26 ina maana kwamba Trilioni 8.4 zitakusanywa na department ya customs na exercise duty. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaitaja hii department kwa sababu ndiyo inayohudumia bandari yetu, na ndio inayohudumia viwanja vyetu vya ndege lakini ndio inayohudumia mipaka yetu, Mheshimiwa Waziri wa Fedha twendeni tukafanya mapinduzi kwenye Bandari yetu. Haiwezekani eti bandari yetu ya nchi haina vifaa vya kisasa vya kupakua mizigo na kupakia mizigo. Twendeni tukanunue vifaa hivyo ili mizigo mingi ipite kwenye bandari yetu. Hali ilivyo hivi sasa Bandari yetu inapitisha tani Milioni 17 kwa mwaka, kiwango hiki ni kidogo sana ukilinganisha na bandari ambazo tunashindana nazo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukafanya mapinduzi kwenye bandari kwa kununua vifaa vilevile tutafanya mapinduzi kwenye bandari kwa kuziangalia vizuri sheria tunazozitunga kwenye Jumuiya yetu ya Afrika Mashariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge sikilizeni niwaambie Sheria hizi za Afrika Mashariki Tanzania trading yetu kubwa ya kibiashara tunafanya na SADC tuna trade kidogo sana na East Africa, wenzetu wamekuwa wajanja sana wana tu-fix kwenye sheria hizi hasa hasa zile zinazohusu usafirishaji wa mizigo kutoka bandarini kwenda kwenye nchi tunazozihudumia. Kwa hiyo, tujipange vizuri kwenda kusimamia eneo hilo ili bandari yetu ipitishe mizigo mingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile baada ya kupitisha bajeti hapa wenzetu wa Serikali tunawapa kazi ya kwenda kuitekeleza bajeti, siku zote hapa tumekuwa tukitaja suala la monitoring and evaluation, budget circle yetu ilivyo, ina sheria hapa Bungeni kupitia Sheria yetu ya Bajeti, inaangazia draft ya budget, inaangazia approval ya bajeti ndiyo tunachokifanya hapa sasa hivi tupo kwenye hiyo stage ya approval, vilevile inapoingia stage ya execution kwenye stage ya bajeti ndipo ambapo Sheria yetu inakosa nguvu, inakosa nguvu. Kwa hiyo, tunaiomba Serikali ikalete policy ya monitoring and evaluation ili tutunge sheria na hili hapa limekuwa likizungumzwa na kukosewa kosewa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hatuhitaji kutengeneza independent board yeyote hapa, Bunge ndiyo jukumu lake hili yaani tunachotakiwa sasa sisi ni kuendelea kusimamia Serikali kwa maana ya monitoring and evaluation kipindi tutakapokuwa tumeitunga sheria hiyo ya monitoring and evaluation ili tuweze kuisimamia Serikali vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho niipongeze sana Serikali, nimpongeze sana Mama yangu Samia Suluhu Hassan Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa sababu mimi ni shahidi tosha kwamba bajeti aliyoileta hapa imezingatia maoni yote ya Wabunge yakiwemo maoni ambayo tumeshauri hapa ya ku-finance miradi mikubwa kwa kutumia infrastructure bond, ipo hapa imetajwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, niipongeze sana Serikali nimpongeze sana mama yangu Samia Suluhu Hassan Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano, kwa sababu mimi ni shahidi tosha kwamba bajeti aliyoileta hapa imezingatia maoni yote ya Wabunge yakiwemo maoni ambayo tumeyashauri hapa yaku-finance miradi mikubwa kwa kutumia infrastructure bond, ipo hapa imetajwa. Bajeti pia imechukua maoni yetu Wabunge ya kufanya credit rating ya nchi yetu, ipo hapa imekaa. Mheshimiwa Waziri nikupongeze sana, ondoa mashaka hautakuwa unpopular, utakuwa ni popular finance Minister kwa sababu umeyabeba maono ya Mheshimiwa Rais ukatuletea hapa kwa kadri ambavyo alielekeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kuyasema hayo nikushukuru sana ahsante sana kwa fursa.