Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Neema Kichiki Lugangira

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana.

Mheshimiwa Naibu Spika, nami napenda niungane na Wabunge wenzangu kuipongeza sana Serikali kwa bajeti nzuri na bajeti ya kimkakati ambayo inakwenda kuinua wananchi wote hususan wananchi wa chini. Kipekee kabisa napenda kumpongeza sana Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kasi ambayo amekuja nayo na nia yake ya dhati ya kuhakikisha kwamba maendeleo yanawafikia Watanzania wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo mimi napenda nichangie kwenye eneo la vyanzo vipya vya mapato, hapa nitaanza na eneo langu la kwanza ambalo linahusu huduma ya sekta hii ya ki-digital kwa mujibu wa takwimu za TCRA Tanzania ina jumla wa watumiaji wa Internet Milioni 29 lakini vile vile ina jumla ya watumiaji wa huduma za kupokea fedha kwa njia za mtandao wa simu Milioni 32 hivyo hii sekta ya ki-digital ni sekta kubwa na ninaipongeza sana Serikali kwa kutambua hilo na hata kuunda Wizara mpya ambayo ina dhamana ya masuala mazima ya TEHAMA.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ningependa kumshauri Waziri na Serikali kwa ujumla ifanye mapitio ya Sheria ya Kodi ya Mapato ya mwaka 2004 pamoja na Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani ya mwaka 2014 ili sheria hizi mbili ziweze kuwa na vifungu vitakavyowezesha utozwaji wa kodi kwenye biashara ya sekta hii, napendekeza Serikali ije na kodi ya huduma za ki-digital kwa maana ya digital service tax nasema hivi kwa sababu hivi sasa kuna huduma nyingi zinafanywa na sekta hii ambazo chanzo chake ni ardhi ya Tanzania.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kwakuwa chanzo chake ni ardhi ya Tanzania basi Serikali inayo fursa ya kutoza kodi aina ya digital service tax nitatoa mfano mdogo, matangazo ya biashara yanayofanywa kupitia online platforms yaani mitandao ya kijamii kama Facebooks, Instagram, Twitter Google nayo yanaweza kuwa ni fursa ya kutozwa kodi, vilevile yapo masoko ya kimtandao ambayo yanakutanisha wanunuzi na wateja kama Amazon, E-bay, Alibaba, Kikuu na kadhalika, nako kunaweza kukawa kuna fursa ya kutoza kodi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia zipo biashara za kukodi usafiri na hoteli kama vile wengi tunatumia Uber, Boat, Airbnb booking.com nayo ni fursa ya Serikali ya kutoza kodi, lakini pia lipo eneo hili la michezo ya kubahatisha yaani online betting. Nimeona Serikali imependekeza kushusha ile gaming tax on winning kutoka asilimia 20 kwenda asilimia 15 lakini kiuhalisia wengi wanapenda kutumia online betting kwa sababu unapocheza online betting hakuna kodi ambayo unalipia kwa hiyo nayo hiyo ni fursa ya Serikali kutoza kodi.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile napenda kuikumbusha Serikali kwamba hivi sasa tunao kakribani Watanzania Millioni 5.9 ambao wanatumia mitandao hii ya kijamii. Hivyo kwa mantiki hiyo, ninaiomba sana Serikali iiangalie sekta hii kwa jicho la kipekee na ije na utaratibu wa kutoza kodi ambayo inaweza ikaenda kwa jina la digital service tax ili kuhakikisha kwamba Tanzania tunanufaika na sekta hii ambayo inakua, ambayo inaendana na digital economy na hata Waziri mwenye dhamana ya Wizara hii ya masuala ya TEHAMA aliahidi kwamba ataandaa sera ya digital economy, kwa hiyo kwa ujumla wake nadhani tutapata fursa ya kupata vyanzo vipya vya mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo langu la pili napenda kuongelea nishati ya jua, nafahamu kwenye Bunge lililopita Bunge la 11 Bunge lako Tukufu mlipitisha kuweka msamaha wa kodi wa ongezeko la thamani kwenye vifaa vya nishati ya jua (solar) lakini kwenye mapendekezo ya Mheshimiwa Waziri, amependekezwa kwamba afute msamaha huu, na hii inaendana na ile unpredictability ya sera zetu, nasema hivi kwa sababu Serikali imefanya jitihada kubwa sana ya kuhakikisha kwamba umeme unafika mpaka vijijini, lakini mpaka sasa tunavyoongea kuna vijiji takribani 2000 bado havina umeme na hata vijiji ambavyo vina umeme, umeme umefika kwenye centre sio kaya zote zenye umeme na sio vitongoji vyote kwa hiyo bado wananchi wetu wanategemea kwa kiasi kikubwa umeme unaotokana na solar nishati hii ya jua. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kule vijijini ukienda wanategemea solar kwa ajili ya Zahanati, wanafunzi wanategemea solar kwa ajili ya kusomea, wananchi kule wanategemea solar kwa ajili ya kupata habari, wanategemea solar kwa ajili ya kuchaji simu zao. Mheshimiwa Waziri hili pendekezo la kuondoa ule msamaha wa kodi kitakachokuja kutokea ni kwamba gharama ya kupata vile vifaa vya solar itaongezeka kwa takribani asilimia 27 mpaka asilimia 35 na ambaye atakwenda kuumia kwenye gharama hii ni yule mtumiaji mwananchi wa kijijini ambaye Serikali ya Awamu ya Sita, Serikali ya Mama Samia Suluhu Hassan Rais wetu anataka kuhakikisha kila mwananchi popote pale alipo aweze kupata maendeleo na maendeleo ya kiuchumi chachu mojawapo kubwa ni nishati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mimi ninaiomba sana Serikali kwa unyenyekevu mkubwa wauache huu msamaha wa kodi kwenye eneo hili uendelee kubaki pale pale kwasababu kuiondoa kuifuta ni kumuumiza mwananchi wa chini ambaye Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ndiye anayemtetea na ndiye anaye mpigania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo langu la mwisho ni eneo la lishe napenda tu kusema kwamba, nadhani wakati umefika sasa Serikali iweke jitihada kubwa zaidi na uwekezaji kwenye kinga badala ya tiba, nasema hivi kwasababu kwa taarifa za Serikali kama tutaendelea Tanzania kuwa na hali ya ukosefu wa lishe bora tuliyonayo kwa kipindi cha miaka 10 yaani tangu 2014 mpaka 2025 Taifa letu litapoteza mapato mengi sana kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kila mwaka tutakuwa tunapoteza Trilioni mbili kwasababu ya kuwa na hali ya udumavu tuliyonayo, kila mwaka tutapoteza Bilioni 230 kwa sababu ya upungufu wa damu kwa wanawake wajawazito, kila mwaka tutapoteza Billioni 15 kwa sababu ya upungufu wa madini joto, lakini kama hiyo haitoshi napenda niongezee kwamba tutakapokuja kwenye yale magonjwa yasiyoambukiza, ambayo yanamahusiano na lishe kama kisukari, moyo, pressure, figo, Inni na aina mbalimbali za cancer kwa taarifa za Serikali inasema kwamba kila mwaka Tanzania inatumia bilioni 457 kugharamia magonjwa haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na magonjwa haya yanapelekea hata mfuko wetu wa Bima ya Taifa upo taabani sasa basi, na kama hiyo haitoshi hivi sasa Tanzania inakadiriwa kila mwaka asilimia 2.65 ya pato ghafi la taifa yaani GDP linapotea tu kwasababu ya udumavu. Sasa kama kila mwaka udumavu tu unachangia pato ghafi letu la Taifa lipungue kwa asilimia 2.65, mimi nadhani wakati umefika na Mheshimiwa Waziri pamoja na wachumi wabobezi kabisa ambao tunao ndani ya Wizara watakubaliana nami kwamba wakati umefika Serikali iweke jitihada kwenye kinga badala ya tiba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ningependa kupendekeza yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, nafahamu kwamba sera ya chakula na lishe imeshakamilika imebaki tu kupitishwa na sera hii ipo kwenye Ofisi ya Waziri Mkuu naomba sera hii kwa heshima zote na unyenyekevu ifanyiwe kazi, lakini pia napenda kupendekeza Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango ione namna ya kuja na kodi ndogo kwenye vyakula ambavyo vina sukari nyingi, mafuta mengi na chumvi nyingi, hii itamlinda mlaji lakini pia itaipatia Serikali pato zuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naunga mkono ….

NAIBU SPIKA: Hebu ngoja kwanza umesema kwenye chakula chenye sukari nyingi, mafuta mengi wachaji kodi ndogo.

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, nchi za wenzetu walichofanya hasa nchi za Bara la Ulaya ili kupunguza kasi ya magonjwa yasiyo ambukiza wametambulisha kodi kwa mfano wenyewe wanaiita sugar tax kwa hiyo kama juisi ambazo zimewekwa kiwango kingi sana cha sukari basi inatozwa.

NAIBU SPIKA: Sasa umetumia neno kodi kidogo hapo ndiyo tumepata changamoto.

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, kodi kubwa.

NAIBU SPIKA: Haya ahsante.

MHE. NEEMA K. LUGANGIRA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana nashukuru. (Makofi)