Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Ramadhan Suleiman Ramadhan

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chake Chake

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kunipa fursa hii ya kuchangia kwenye hoja ya bajeti iliyoko Mezani. Nichukue fursa hii kumpongeza na mimi kama wenzangu Waziri wa Fedha kutokana na uwasilishwaji wake mzuri wa bajeti hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitaalamu sio mchumi ni Mwanasheria. Kwenye sheria za uwakala kwa kitaalamu tunaziita Law of Agency, kuna usemi wa kilatini unaosema kuifasi pa alyum fas perse. Tunapompongeza Mheshimiwa Waziri tunampongeza yeye pamoja na timu yake yote walioandaa bajeti hii. Tunampongeza yeye pamoja na Baraza lote la Mawaziri kwa sababu, alichokileta ndani ya Bunge hili sio mawazo yake peke yake, ni yake yaliyochangayika na Mawaziri wenzake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunapolipongeza Baraza la Mawaziri tunampongeza Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri ambaye ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Mama Samia. Kwa hiyo, kilicholetwa mbele yetu ni maamuzi ya Serikali n ani maamuzi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa tanznaia. Mnafanya kazi nzuri kama Serikali, Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye bajeti hii Mheshimiwa Waziri ameleta mapendekezo 15 ya kufanya marekebisho kwenye Sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Sura ya 148, kuanzia page ya 28 mpaka ya 31, mapendekezo 15. Moja ya mapendekezo hayo amekuja kuomba kufanyiwe marekebisho ya sheria ili kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye vyumba vya ubaridi, cold rooms. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninavyoitazama bajeti hii ni kwamba, kwa asilimia 90 imesikiliza vilio vya Wabunge. Haya ndio ambayo yalikuwa yakipigiwa kelele kila siku na Waheshimiwa Wabunge humu ndani kwa hiyo, ni bajeti ambayo imesikiliza na kuliheshimisha Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani hiki kilio kimeliliwa sana humu na Dada yangu Mheshimiwa Neema Kichiki, mama lishe. Kwamba, inaenda kuongeza thamani ya mazao yetu ya mbogamboga kwenye sekta yake ya lishe ambayo itaenda kusaidia wakulima wanaolima mbogamboga na mauwa kuongeza thamani ya mazao yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia ameleta mapendekezo ya kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye madini precious metals Wabunge wa kanda Mungu aliwajalia madini, hasa Kanda za Ziwa, Geita na kwingine, Mheshimiwa Musukuma, wamelia sana. Wakati wa uchangiaji wa jumla tuliyasema haya sana ambayo hiyo inaenda kuongeza thamani kwenye viwanda vyetu vya uchenjuaji wa madini ambapo jana Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alizindua kiwanda kimoja, inaenda kuongeza fedha za kigeni, inaenda kuongeza ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ameleta mapendekezo ya kusamehe kodi kwenye ongezeko la thamani kwenye huduma ya bima ya mifugo. Wabunge Kaka yangu Mheshimiwa Nicholaus Ngasa, wamelia sana kuhusu hili, ndio ambalo Mheshimiwa Waziri kalichukua kalileta ndani ya bajeti kwa sababu, lilikuwa kilio cha Wabunge. Ameleta mapendekezo ya kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye nyasi bandia; rafiki yangu hapo Mheshimiwa Sanga amelipigia kelele hili, kwa hivyo limechukuliwa likaja likawekwa kwenye bajeti kwamba, linataka utekelezaji. Maana yake ukiiondoa hii inaenda kukuza yale mawazo ya Mheshimiwa Sanga ya kukuza mpira wetu na kuleta viwanja vya kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ameleta mapendekezo ya kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye kadi za kutengenezea National ID. Haya yamepigiwa kelele sana, upatikanaji wa National ID umekuwa tatizo, labda kutokana na gharama za uzalishaji kwa hiyo, Waziri akaleta mapendekezo, ili tupunguze huko hizi ID zipatikane kwa wingi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ameleta mapendekezo ya kusamehe Kodi ya Ongezeko la Thamani kwenye simu janja, haya aliyasema kaka yangu Mheshimiwa Jerry. Tunataka kutoka asilimia 40 ya matumizi ya mitandao tunaelekea asilimia 86, hatuwezi kufika kwenye hiyo target kama gharama za simu janja, moderm na vishkwambi viko juu. Ndio hayo ambayo Serikali wameyaleta kwetu kwa sababu, hicho ndio kimekuwa kilio chetu cha muda mrefu; dada yangu Mheshimiwa Judith Kapinga haya kayasema sana kwa hiyo, yamechukuliwa mawazo yake yameletwa kwenye bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kaleta mapendekezo ya kufuta msamaha wa kodi ya ongezeko la thamani kwenye mikebe inayotumika kuhifadhia maziwa. Hapa yamesemwa hatusafirishi maziwa nje ni kwa sababu, kulikuwa kuna gharama za uhifadhi wa maziwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la Zanzibar ambalo ndiyo limenikuna kweli kweli Waziri ameleta mapendekezo ya kuondosha au kurudisha utaratibu wa VAT kwa bidhaa inazonunuliwa Tanzania Bara na zinazotumika Zanzibar. Wafanyabiashara katika Jimbo langu la Chakechake na Wazanzibar kwa ujumla wafanyabiashara wakubwa kama hardware’s kwa asilimia 80 sasa hivi wanaagiza bidhaa kutoka Tanzania Bara hawaendi tena China, hawaendi tena India, hawaendi tena nchi nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nondo tunanunua Tanzania Bara, saruji tunanunua Tanzania Bara, wire za umeme tunanunua Tanzania Bara, tunanunua Tanzania Bara gypsum board, gypsum powders, bodi za kujengea, misumari, wires na tumekuwa tukililia hili kwa muda mrefu jirani yangu haya Mheshimiwa Abdul-Hafar wakati wa mchango wake alilisemea hili kwa sana kwamba kumekuwa na ukiritimba wafanyabiashara wanaotoka Zanzibar wakija wakinunua bidhaa zao Bara na kuzirejesha Zanzibar na hiki ndiyo kilio ambacho Mheshimiwa Waziri amekileta na Serikali ya Mama Samia wamelisikia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lango ni kutaka kuondosha hiyo migongano, watu ambao walikuwa hawapendi muungano wetu walikuwa wanatumia mwaya wa kutubomoa sehemu hii, ya kuonesha hii ni nchi moja mbona mnanyanyaswa mkifika Bara. Sasa haya ndio yanakwenda kuondoka maana yake sasa unaondosha VAT kwa sababu VAT inalipwa na yule mtumiaji wa mwisho mlaji.

Kwa hiyo ukiweka VAT akija Bara analipa halafu akifika Zanzibar analipa mara mbili, anafanya double maana yake anaiongeza thamani bidhaa yake ili apate kufikia ile VAT aliyoitoa mara mbili na bidhaa inapanda bei kwa hivyo haya yanakuja kuondosha tatizo na kupunguza bei na kuwasaidiwa wananchi wetu walioko kwenye maeneo yetu na wafanyabiashara kufanya biasahra bila kusumbuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili tatizo lilikuwa linatokea pia kwenye umeme tumesema sana kwenye TANESCO walipokuwa wanatuuzia umeme ZEC kwenda Zanzibar walikuwa wanatutoza VAT na ndiyo hayo madeni ambayo yalikuwa yanalalamikiwa na ikishafika umeme Zanzibar kwenda kwa mlaji mimi ili uingie kwenye nyumba yangu nalipa tena VAT, kwa hiyo mapendekezo haya yakishafanyiwa kazi maana yake yanaenda kuondoa hizo double VAT kwa sisi watumiaji wa mwisho wa umeme maana yake hii inaenda kurahisisha maisha ya wananchi watu. Kwa hiyo, nilivyoisoma bajeti hii kuanzia page ya mwanzo mpaka ya mwisho ya 121 hakuna kitu ambacho kilikuwa kinanipa furaha wakati nasoma kama nikiona haya yamesemwa na Mheshimiwa Waziri. Maana yake ndiyo yalikuwa vilio vya Waheshimiwa Wabunge. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa niaba ya wananchi wa Chakechake, naunga mkono hoja bajeti hii imetuheshimisha sana Bunge, Mungu aibariki sana Tanzania na Mheshimiwa Rais wetu. (Makofi)