Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Charles John Mwijage

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muleba Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipatia fursa ya kuchangia Bajeti Kuu, Bajeti ya Serikali. Awali ya yote naunga mkono bajeti hii, mimi naiita bajeti ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono maoni na Mapendekezo ya Kamati ya Bunge inayoshughulikia bajeti, lakini nijitendee haki naunga mkono mchango wa Mheshimiwa Dkt. Ashatu Kachwamba alipozungumzia Idara ya Mipango. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi katika mchango wangu nitazungumzia zaidi namna ya kupata mapato. Najua waswahili wanasema kulea mimba siyo kazi, kazi ni kulea mwana, tumehangaika tupo hapa miezi yote hii tangia mwezi wa kumi, vijijini huko tunatengeneza bajeti mtoto huyu Mwigulu Nchemba ameshamtoa sasa tutengeneze mapato, mimi najikita kwenye mapato.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti yetu tumeongeza shilingi mia.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwijage kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nataka kumpa taarifa ndogo tu kwamba kulea mimba ni kazi sana na kuna kipindi hata wamama tunapata bed rest kwa miezi tisa yote ukilea mimba. Kwa hiyo kulea mimba ni kazi na kulea mwana pia ni kazi vyote kwa pamoja. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Mwijage, nadhani hiyo inamaanisha misemo mingi ya Kiswahili itabidi ibadilishwe, maana wanawake tuko kazini safari hii. Tunataka kurekebisha mambo yote ambayo kwake yeye hayajakaa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Charles Mwijage.

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, naikubali sana taarifa hiyo. Kazi ya mwenzio ambayo hujawahi kuifanya usiizungumzie. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, niizungumzie ongezeko la shilingi 100 kwenye mafuta. Ongezeko la shilingi 100 kwenye mafuta, ile tozo si hoja, hoja ni mzigo mzito sasa utakaokuwa unabebwa na kila lita ya mafuta. Kwa ongezeko la shilingi 100 petroli sasa itatozwa shilingi 892, dizeli shilingi 768 na mafuta ya taa shilingi 765. Si hoja na hiyo, hoja ni kuwa sasa mafuta haya kwa kiasi kinachotozwa italeta ushawishi na kivutio cha watu kukwepa kodi hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiweza kutoa depot malori 27 ya mafuta utaweza kukwepa shilingi bilioni moja. Kwa viwango vya Mheshimiwa Ummy Mwalimu, hizo ni sekondari mbili kabisa kabisa za Kata.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninachotaka kuzungumza, katika kuboresha mapato lazima Serikali tujiandae na tujiimarishe katika kuimarisha vitengo vyetu vya upimaji, sina wasiwasi na ways and measure, lakini lazima tujiimarishe. Tujiimarishe na kitengo kinachopewa kazi ya kuangalia kwamba mafuta hayatoki kundi moja kwenda kundi lingine pale tunapozungumzia suala la vinasaba. Lakini tunalo tatizo la miundombinu ya cha wote. Kuna miundombinu muhimu ya mafuta ambayo hakuna yeyote anayewajibika nayo, ambapo mafuta yanapotea na huwezi kumuwajibisha yeyote. Serikali inapaswa kudhibiti maeneo hayo na kumuwajibisha mmojawapo. Lazima ichukuliwa taasisi moja ya Serikali ipewe jukumu la kulinda miundombinu hiyo ambako ndipo mafuta mengi yanaweza kuwa yanapotelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jumla ya yote, nimshauri Mheshimiwa Waziri kwamba kitengo cha TRA kiimarishwe upya kwa kuongezewa watu na kupewa mafunzo ya kudhibiti sekta hii. Kwa sababu utakuja kuona kwamba, katika kuuza lita bilioni 3.14 kwa mwaka kwa kiwango cha wastani wa shilingi 700 kwa lita ni fedha nyingi tutakuwa tunazikusanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pamoja na hiyo, mimi napenda niishauri Serikali, hayo ni mafuta yatakayouzwa ndani, tunapaswa kufanya utaratibu wa kuchochea mafuta mengi yauzwe. Na hapa nazungumzia mafuta ambayo yakiuzwa humu ndani hayatatubebesha mzigo. Kwa sababu kumbuka mafuta haya unayoyatoza tozo utawajibika kutafuta dola kusudi uyanunue; lakini kuna mafuta unaweza kuyatoza pasipo kutafuta dola kusudi kuyanunua. Haya ni mafuta yanayowezesha mizigo kupita Tanzania kwenda nchi za Jirani (transits).

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu, ya sheria zetu na uendeshaji wa shughuli tumekuwa tuki-discourage transit cargo, na ndiyo maana mizigo inakwenda Durban, Beira pamoja na Mombasa. Sasa tunapaswa kuangalia udhibiti na usimamiaji wa mizigo yetu ili mingi ipite kusudi tuweze kupata mafuta ambayo tutayatoza tozo kwa ili tuweze kuongeza pato letu.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na hiyo niishauri Serikali, kwamba muangalie sasa, wakati umefika wa kuweza kuitumia Dar es Salaam kuwa trading hub. Yaani mafuta yawe traded Dar es Salaam yaweze kuuzwa nje. Lita bilioni
2.5 zinapita Dar es Salaam zikiwa transit kwenda land locked countries. Sasa tukigeuza re-export Tanzania ikiwa trading hub ina maana takriban asilimia 30 zinaweza kuwa zinauzwa kutokea hapa, na kila yanapouzwa, unapata mark-up na ile mark-up inaweza kuchangia kwenye mapato ya Serikali.

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala la uchumi wa nchi. Nimeona mapendekezo katika sekta ulivyopendekeza. Niombe sasa, kwa kila sekta tuanze kuweka vigezo KPI, kwamba kila sekta inaleta nini?

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi tunauza nje ya nchi kwenye re-export, tunauza mazao yenye thamani ya dola bilioni 2.9. Katika hiyo theluthi mbili ni dhahabu, lakini ukiangalia potential ya export ni trilioni 2.36 bila kuweka dhahabu. Sasa tunapaswa kuwekeza katika maeneo hayo kusudi tuuze zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilisema hapa kwamba katika fursa ya nyama Tanzania hatu-export chochote ilhali wenzetu Uganda na Botswana wanauza dola milioni 100, dola 135 mtawalia, Uganda anauza maziwa dola milioni 100 kwa mwaka, sisi hatupo.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna fursa ya ma- avocado ambayo yanapendwa dunia nzima, na soko la avocado linaendelea kuongezeka duniani. Hata hivyo Tanzania pamoja kuwa na nafasi ya tatu katika Afrika bado kiasi tunachosukuma kwenye soko hili soko kubwa halijaonekana.

Mheshimiwa Naibu Spika, imekuja fursa ya soya beans. Ukihesabu tani milioni 42 tunazopewa na China kuuza kule ni revenue kubwa sana kuliko mazao yote tunayo-export. Sasa, Wizara isaidie sekta hizo kusudi tuweze kutengeneza kipato kikubwa na kuweza ku-supply kwenye iInternational markets. Hiyo ni sekta ya re-export. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenye mchango wa Mheshimiwa Waziri alipozungumzia matumizi ya LUKU katika kuweza kukusanya Property Tax. Nakubaliana na wazo hilo kwa kuwa lina ubunifu ndani yake, hata hivyo kuna angalizo. kuna mtu ana nyumba ya ghorofa vyumba viwili juu kimoja chini analipa shilingi 5,000. Je, yule mwenye vyumba vitano chini kwa nini umlipishe shilingi 1,000?

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna mtu ana vyumba saba, ana wapangaji watatu kila mpangaji ana mita yake atalipa shilingi 3,000. Sasa kwa nini huyu unamlipisha shilingi 3,000 badala ya shilingi 1,000 na ni vyumba 31 vile vile? Lakini kuna mtu ni mstaafu, kama alivyosema Mwenyekiti wa Kamati, kwanini huyo unampa adhabu hiyo? Suala la msingi kuna watu wako tayari kulipa hawajapewa umeme. Kwa hiyo napendekeza Serikali iongeze fedha kwenye REA kusudi wale wanaotaka umeme wapewe umeme. Vilevile Serikali iwekeze katika huo mfumo wa LUKU; na nashauri ikiwezekana tusubiri. Huu utaratibu usije ukashindwa kama ule wa TRA ulivyoshindwa au wa local government ulivyoshindwa katika kuweza kukusanya mapato haya.

Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)