Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Dr. Advocate Damas Daniel Ndumbaro

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Songea Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII: Mheshimiwa Naibu Spika, nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupa sisi wote uhai na afya na kutuwezesha kuendelea kuwatumikia Watanzania kupitia Bunge lako Tukufu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru wewe binafsi kwa kuendesha mjadala huu vizuri kabisa. Pia nimshukuru Mwenyekiti wa Kamati, Makamu Mwenyekiti wa Kamati pamoja na Kamati nzima ya Maliasili na Utalii kwa hotuba yao na ushauri wao. Katika hotuba yao wametoa mapendekezo 14 ambayo Wizara imeyapokea kwa mikono miwili na tunaahidi kwamba mapendekezo hayo tutakwenda kuyatekeleza kwa kushirikiana nao.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nitumie fursa hii pia kuwashukuru Wabunge 78 ambao wamechangia hoja ya Wizara ya Maliasili na Utalii, lakini pia Wabunge 16 ambao wamechangia kwa maandishi. Hoja zao, michango yao na maelekezo yao tumeyapokea na kuahidi kwamba ushauri wote walioutoa tutautumia ili kuboresha utendaji wa Wizara hii na hatimaye kuleta tija kwa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niruhusu niongelee mambo machache sana ambayo Waheshimiwa Wabunge wameyaelezea.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la kwanza ni migogoro iliyopo kati ya wahifadhi na wananchi. Imetamkwa hapa kwamba wananchi kadhaa wamefariki, lakini niseme pia na wahifadhi 12 wamefariki. Roho hizi za Watanzania ni nyingi sana, sina mamlaka hayo lakini ningekuwa nayo ningekuomba Bunge lako Tukufu lisimame angalau kwa sekunde 15 kuwakumbuka Watanzania hawa ambao wamefariki.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Rais mama Samia haipendi kuona mwananchi wake yeyote anakufa kwa sababu yoyote ile. Sisi kama Wizara ya Maliasili na Utalii hatufurahishwi na jambo hilo.

Mheshimiwa Naibu Spika, Waheshimiwa Wabunge, mmesema hapa kwamba wananchi wengi wamefariki kutokana na migogoro kati ya wahifadhi na wananchi, lakini nami nimesema hapa askari 12 wameuawa pia katika migogoro hiyo. Tufike sehemu tuseme sasa inatosha. Tutafute ufumbuzi wa suala hili na ufumbuzi ni wa kwetu wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, moja, sisi kama Wabunge tuelimishe wananchi wetu kwamba maeneo ya uhifadhi tusiingie kufanya shughuli nyingine, lakini hata tutapokamatwa na hao askari tusilete resistance ambayo inasababisha mapigano na baadaye kupoteza maisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi kama Wizara tumeanza kuchukua hatua; hivi ninavyoongea askari wetu 61 tumewafukuza kazi. Hivi ninavyoongea askari 40 wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi. Moja kati ya kazi za kwanza ambazo mimi na Naibu Waziri tulifanya ni kwenda Ifakara kufukuza kazi askari watatu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mkakati wetu ni rahisi sana; tukipata malalamiko yenye ushahidi usiokuwa na shaka, sisi tunaitisha parade na tunamfukuza huyo askari kwa aibu na fedheha. Kwa sababu hatupendi askari ambaye amepata mafunzo anakiuka miiko ya kazi yake. Tunachohitaji ni ushirikiano toka kwa wananchi, ushirikiano toka kwa Waheshimiwa Wabunge na sisi kama Wizara tunahakikisha tukipata ushirikiano huo suala hili limekwisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuwashauri wananchi wetu, chanzo cha migogoro hii mpaka kuuana wakati mwingine ni rushwa; askari wetu wanaomba rushwa ili waingie kulima, askari wetu wanaomba rushwa ili waruhusu wafugaji waingie. Sasa ile pesa ya rushwa ikiisha anataka aongezewe rushwa, ndipo mgogoro unapoanza. Wananchi tukatae kutoa rushwa kutoka mwanzo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namba yangu mimi na namba ya Mheshimiwa Naibu Waziri na namba ya Katibu Mkuu ziko wazi kwa mtu yeyote kupokea malalamiko yoyote yenye Ushahidi ili tuweze kuchukua hatua. Ninaamini suala hili sasa linakwenda kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhakikisha kwamba nidhamu ya askari wetu hawa inakaa vizuri, kwa sababu hivi sasa bado zile Kanuni za Jeshi Usu hazijasainiwa. Niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba nitasaini kanuni hizo Jumatatu ili kuanzia tarehe Mosi, Julai, askari atakayekiuka miiko yake ya kazi haendi kwenye mahakama za kawaida, anakwenda kwenye mahakama za Kijeshi na anafukuzwa kazi mara moja. Kwa hiyo hii tunaamini italeta sana ufumbuzi kwenye hoja hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, limeongelewa suala la vitalu hapa na ushauri mwingi umetolewa. Naomba niseme tumepokea ushauri huo wote. Hata hivyo, niongeze kitu kidogo tu, kwamba Wizara hii imekuwa na desturi ya kubadilisha Mawaziri kila baada ya miezi 18 na chanzo kikubwa cha Mawaziri kubadilishwa ni mfumo wa zamani wa ugawaji wa vitalu ambao ulikuwa umegubikwa na wingu kubwa la sintofahamu, rushwa na upendeleo.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo mpya uliowekwa wa kielektroniki umekuja kutibu matatizo hayo. Jambo lolote jipya haliwezi kuwa perfect a hundred percent, litakuwa na dosari hapa na pale. Tusichukue dosari hizo kubomoa mfumo huu mpya ambao una uwazi, una ushirikishwaji, unaleta wadau wapya kwenye sekta hii na unaondoa rushwa. Turekebishe matatizo hayo taratibu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mfumo huu ambao umeshaanza kutumika katika minada minne tumeweza kuuza vitalu 12, lakini vitalu hivyo 12 ambavyo vimeuzwa vimetuletea fedha ambayo inatusaidia sasa kwenda kujenga madarasa. Inatusaidia sasa kwenda kujenga hospitali, inatusaidia sasa kwenda kujenga barabara na la muhimu zaidi tunasaidia kwenye ujirani mwema kati ya uhifadhi na wananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Festo hapa amesema kule Kitulo anataka ujirani mwema; fedha inatoka hapa. Nimhakikishie Mheshimiwa Festo kwamba hilo jambo litakaa vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli pia performance ya vitalu imeshuka. Ilianza kushuka kabla mfumo huu haujaingia. Kilichosababisha kushuka kwanza ilikuwa ni katika nchi za wenzetu ambako watalii wengi ndio wanatoka, hasa Marekani, walianza kuweka zuio ili hizi trophies zisiende. Walivyozuia kutokana na harakati za wapigania haki za Wanyama, tukajikuta kwamba soko la trophies kule Marekani likashuka, likishuka na uwindaji wao unashuka.

Mheshimiwa Naibu Spika, bahati nzuri Marekani walifungua, lakini baada ya Marekani kufungua hivi juzi European Union nao wametoa azimio la kuzuia trophies zisiingie huko. Sasa siyo jambo letu sisi peke yetu, tumeungana na nchi nyingine zote za SADC tunafanya mchakato ili kuondoa zuio hilo. Haya pamoja na ugonjwa wa Covid-19 ndiyo yamechagia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa utalii wa uwindaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeona Serikali yetu imeanza kuchukua hatua stahiki kabisa na hatua madhubuti kupambana na ugonjwa huu wa Covid-19. Tunaamini tutakavyoweza kuweka sawa suala la Covid-19 na kuondoa hili zuio la kutoka European Union na kuboresha mfumo huu wa uwindaji wa vitalu wa kielektroniki tutaweza kupandisha tena performance ya uwindaji wa kitalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa muda huu mfupi mimi na Mheshimiwa Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara tumeshakutana na wawindaji na vyama vyao mara tatu. Tuliitisha mkutano Morogoro, siku nzima tumeshinda nao, asubuhi mpaka jioni. Tumeongea nao tumepata maoni na maoni yao ni muhimu sana katika kuboresha utendaji wa Wizara. Tunaomba tuwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba hili nalo tunakwenda kuliweka sawa kabisa, na tutaboresha kuondoa sintofahamu yoyote ile.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja mahususi kabisa kutoka kwa Mheshimiwa Olelekaita, Mbunge, wakili msomi. Hoja yake iko kwenye mawanda mawili; moja, alisema kwamba sheria hiyo haipo; pili, akasema sheria hiyo ni ya uonevu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikubaliane naye labda kwenye hiyo hoja ya pili, lakini ya kwanza sheria ipo. Sheria ya Wanyamapori, Kifungu cha 116 kinasema; Sheria ya TANAPA Kifungu cha 28 na Sheria ya TFS Kifungu cha 95, ila tunahitaji kuwa na mjadala wa eneo hilo ili tuweze kuliboresha zaidi, ili kuondoa kelele na malalamiko kutoka kwa Watanzania hao wafugaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kazi hiyo ni kazi ya Bunge hili Tukufu, ndiyo kazi yake kushughulikia sheria kama hizi, kuzirekebisha, kuzitunga na ndiyo maana sisi tuko humu ndani kwa ajili ya kazi hiyo. Kwa hiyo Mheshimiwa Olelekaita, wakili msomi, ambaye mimi huwa nawasiliana naye sana, karibu sana tuje tuongee hili. Naamini pia tutaliweka sahihi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna suala la wanyama wakali na waharibifu sambamba na kifuta jasho. Juzi hapa tulifanya semina kwa Waheshimiwa Wabunge ambao wanatoka kwenye maeneo hayo kwa lengo la kuwapa uelewa nini chanzo cha tatizo hili.

Niseme, nashukuru sana mjadala wa leo unaonesha kwamba Waheshimiwa Wabunge wengi wametambua chanzo ni nini. Baada ya kutambua chanzo ni nini sasa, tujielekeze tutawezaje kuondoa changamoto hiyo.

Mheshimiwa Naibu Spika, njia ya kuondoa changamoto hii ni moja tu; turudi kwenye mpango bora wa matumizi ya ardhi. Vijiji, halmashauri na Wizara; haya maeneo tuyaainishe. Wakati mwingine wananchi wanaingia kwa sababu hawajui; ameshajenga, ameshalima ndiyo anajua kwamba hii ni shoroba.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni wakati kuanzia kwenye vijiji, kuanzia kwenye halmashauri na nasema halmashauri kwa sababu sisi wote humu ni Madiwani. Kwa hiyo kwenye halmashauri zetu tukatoe kipaumbele kwenye kitengo cha maliasili katika halmashauri. Kwa sababu kila halmashauri ina kitengo cha maliasili, lakini hatukipi umuhimu unaostahiki. Imesemwa hapa wana mabunduki ya zamani, hawana risasi, hawana usafiri, lakini wako chini ya halmashauri.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kama Wabunge, ambao pia kama Waheshimiwa Madiwani, tulichukue jambo hili kwa umakini mkubwa sana. tutakavyorudi kwenye Mabaraza yetu ya Madiwani tujiulize ni kwa kiasi gani tunaweza kuimarisha kitengo cha maliasili ili kupunguza kadhia hizi ambazo zinajitokeza. Tukishazipunguza sasa ndipo tutaweka mchakato zaidi wa kuweza kuangalia kwamba zile chache zinazoweza kuwezekana tuweze kufanya vipi katika jambo zima la kifuta jasho na kifuta machozi.

Mheshimiwa Naibu Spika, nimshukuru sana Mheshimiwa Lukuvi kwa ufafanuzi mzuri ambao ameutoa. Yeye ni Mbunge mzoefu na ni Senior Minister. Jambo hili la migogoro ya mipaka alilifanyia kazi vizuri sana, yeye ndio aliongoza Kamati ile ya Mawaziri nane; amefanya kazi nzuri iliyotukuka, kilichobaki ni utekelezaji wake tu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nisingependa kurudia aliyoyasema, lakini niongeze jambo moja. Katika zile hekta ambazo zimefutwa, kuna hekta mahususi 29,000 kwa ajili ya wafugaji. Tutakwenda kuzigawa hekta hizo ili wafugaji waweze kupunguza kadhia yao. Najua haitaondoa kabisa tatizo lao, lakini tutaweza kupunguza. Ili tatizo liondoke kabisa tunapanga uelimishaji zaidi.

Mheshimiwa Naibu Spika, na Mheshimiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mheshimiwa Ndaki, ameshaiomba Wizara ya Maliasili na Utalii tufanye mkutano wa Kitaifa wa pamoja wa Maliasili pamoja na Mifugo. Mkutano huo unakuja kuanzia sasa mpaka Oktoba tutakuwa tumeshaufanya.

Mheshimiwa Naibu Spika, imeongelewa hapa kuwa watu wameshinda kesi lakini mifugo yao haijulikani ilipo, hawajakabidhiwa. Nchi hii inaongozwa na utawala wa sheria na sheria inatafsiriwa mahakamani. Mtu akienda mahakamani ameshinda kesi lazima apate kile alichokishinda mahakamani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwaahidi Waheshimiwa Wabunge na niliahidi Bunge lako Tukufu kwamba, tutafuatilia kesi zote hizi ili haki za wale walioshinda kesi mahakamani zisipotee. Tumelichukua jambo hilo kwa umakini wa hali ya juu na niwaahidi tutakwenda kutekeleza. Kama ambavyo tumekuwa tukipokea maombi ya Wabunge na kutekeleza kwa haraka na hili tutalitekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hata kesho nimealikwa kutembelea kwenye majimbo la Wabunge wawili na nakwenda baada ya bajeti hii. Hiyo yote ni kuonesha kwamba pamoja na kwamba Wizara hii ni muhimu sana katika uchumi, lakini pia ina umuhimu katika mustakabali na maslahi ya wananchi wa kawaida.

Mheshimiwa Naibu Spika, limeongelewa suala la WMAs na wewe unalifahamu vizuri sana kwa sababu ulikuwa consultant wakati hili jambo linaanzishwa. Kwenye hilo kwa sababu ulikuwa ndio mwanzilishi wa hili, niwaombe Waheshimiwa Wabunge wakupigie makofi kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuna WMAs 38 lakini ambazo zinafanya kazi ni 22 tu, hizi 16 zimekufa. Labda niseme WMAs ni nini; WMA ni kifupi cha Wildlife Management Area, kwamba Serikali hii ya Chama Cha Mapinduzi iliona ni bora na ni vyema kukabidhi madaraka ya kusimamia wanyamapori kwenye maeneo ya vijiji kwa wananchi kupitia Serikali za vijiji. Vijiji kwa mkusanyiko kadhaa vinatengeneza kitu kinaitwa authorized association. Wakitimiza masharti yyale wanapata usajili, wakipata usajili wanafanya uhifadhi na uwekezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, zipo ambazo zinafanya vizuri sana kama ile ya Ikona. Imeonesha wanataka kufikia mapato ya shilingi bilioni 2.6 kwa mwaka. Sasa angalia, hiyo ni WMA moja inapata fedha hiyo, lakini wengine wameingia kwenye migogoro ya uongozi, wameshindwa kuhifadhi na ukishindwa kuhifadhi wanyama wanatoweka na wawekezaji wanakimbia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo hizi 16 ambazo wameshindwa kufanya majukumu yao, wanyama wametoweka na hali imekuwa ni ngumu, ndizo ambazo tumesema Wizara tunaziangalia kwa jicho la kipekee.

Mheshimiwa Naibu Spika, tumepanga pia ku-build capacity na kuendelea kuwa karibu na hizi WMAs kwenye utendaji. Kuwashauri zaidi kwa sababu kuna wengine wameingia kwenye mikataba ya kiunyonyaji ambayo haiwasaidii. Tunarudisha kwenye mfumo sasa tuweke mikataba mizuri ili hizi zote 22 ziweze kufanya vizuri na hatimaye zile 16 tuzirudishe kwenye mstari stahiki.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna hoja mahususi pia zimetolewa na Waheshimiwa Wabunge. Moja, tumepokea maombi mengi sana ya kuhusu vibali vya kuvuna kwa wananchi ambao walilima katika maeneo ya hifadhi kimakosa, walikuwa wamezuiwa. Kama nilivyosema wakati wa kulima kuna kuwa na makubaliano na wakati wa kuvuna wanataka kuwe na makubaliano mengine.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kupitia Bunge lako hili Tukufu naomba Wizara itoe maelekezo, hayo makubaliano ya rushwa hatuyataki. Naagiza leo wananchi wote ambao walilima katika maeneo ya uhifadhi, waruhusiwe kuvuna kwa kibali maalum. Maelekezo haya ni kwa nchi nzima, kwa hiyo Waheshimiwa Wabunge hakuna haja ya kuja kuomba tena jambo hili tumelitolea maelekezo mahsusi kwa nchi nzima. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kibali mahsusi kwa mamlaka ile husika kwa sababu unapoingia kwenda kuvuna unaingia eneo la hifadhi kwa hiyo unapewa kibali. Baada ya kibali hicho tunawaomba Waheshimiwa Wabunge watusaidie, wasirudi tena kulima kwenye maeneo hayo, ili mwakani tusilijadili hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Asenga aliongelea kwamba pale Mang’ula kuna kona moja kali sana ambayo inasabababisha ajali, Watanzania wanafariki na ikiinyooshwa ile kona inakula eneo la hifadhi la mita 50. Kubadilisha mpaka wa hifadhi ni Mamlaka ya Mheshimiwa Rais, lakini naomba nijivishe kilemba cha ukoka, niagize pale mkandarasi anyooshe zile mita hamsini, nitaenda kumwomba msamaha Mheshimiwa Rais kwamba nimeingilia mamlaka yake na abariki maamuzi hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mkandarasi yule anyooshe pale ili tupunguze ajali kwa Watanzania ambao wanafariki. Bahati nzuri kona ile naifahamu kwa kuwa nimesoma Ifakara, lakini nimeoa kule, naenda kusalimia wakwe kila siku na naona madhara ya kona ile. Kwa hiyo hili nalo naomba, watendaji wa Wizara wamenisikia utekelezaji wake huo uanze leo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imegawa namba 14 hotlines kwa ajili ya kupokea malalamiko ya wananchi kutokana na wanyama wakali, hiyo yote ni kusaidia kupunguza kero hii. Namba hizo ni za bure, ukipiga wala huchajiwi, tunaomba kupitia Bunge lako Tukufu, tuwaambie watanzania wote, ambao wana matatizo ya kukabiliana na wanyama wakali, watumie namba hizo kutoa taarifa ili askari wetu nao waweze kufika kwenye eneo husika kwa haraka kabisa, tutaendelea kuzisema namba hizo kwa wananchi mbalimbali.

Mheshimiwa Naibu Spika, imeongelewa hapo hoja mahsusi ya miundombinu ya Burigi - Chato, mimi nimetembelea, nimefika nimejionea tunahitaji kuboresha miundombinu ya Burigi - Chato na bajeti hii ndiyo imebeba fedha za kuboresha miundombinu ya Burigi - Chato kwa hiyo Mheshimiwa Dkt. Oscar ukiipitisha bajeti hii tume-solve tatizo la Burigi - Chato, tushikamane twende kumaliza tatizo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na ufafanuzi ambao nimeutoa kwa hoja zote ambazo zimewakilishwa na Wabunge hapa, pia hoja ambazo Wabunge wamezitoa kimaandishi na sisi tutazijibu pia kimaandishi na kuzileta kwako.

Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana wewe, niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao na maelekezo yao, niwaombe sana sasa tupitishe bajeti hii ili twende kwenye utekelezaji.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki.