Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Tabasamu Hamisi Hussein Mwagao

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sengerema

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii ya Maliasili na Utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Wizara hii kufanya kazi kwa uzuri sana ya kupongezwa, lakini nina masikitiko makubwa sana kutokana katika Wizara hii. Wizara hii inayo wataalam ambao watalaam hawa ili wawe watalaam waliandika maandiko sasa tunashangaa katika hiki Chuo chao cha Mwika kuna tatizo la wafugaji na hawa wasimamizi wa wanyamapori watu wa TAWA. Hawa ng’ombe kisheria wanaitwa ni wanyama na tembo, simba na wenyewe ni wanyama kwa lugha nzuri ya Kiswahili wanaitwa hayawani. Kwa hiyo ng’ombe anaitwa hayawani pia na ndio maana wanachungwa hawana akili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa ni kwamba tunasikitika sana, maliasili maana yake katika Kamusi ni kitu ambacho sisi tumekikuta kama urithi, ambacho kinakuwa ni sehemu yetu. Kwa hiyo ng’ombe ni maliasili katika nchi hii. Tunashangaa ng’ombe wakienda kwao, wale wametoka tu porini kuja kukaa na binadamu wakafugwa. Sasa wakirudi kwao wanakuwa ni adui, wanapigwa faini wakati tembo wakija kwa binadamu hatujaona Sheria ya Maliasili inasema, wanapigwa faini kiasi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo tunawaomba watu wa Wizara ya Sheria na Katiba watutengenezee sheria ya tembo akitoka katika eneo lake akaja kwa binadamu faini yake itakuwa ni bilioni moja, milioni mia tano ili wananchi tujue. Haiwezekani sheria ikawa ya upande mmoja, hakiwezekani kitu kama hicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachotaka kukwambia ni kwamba, hakuna kitu kibaya zaidi kwa wananchi wanachoona kwamba wanatungiwa sheria wao, wakati wale wanyama wengine hawatungiwi sheria, kwa sababu hawa ng’ombe sisi tuliwakuta, tumewakuta kama maliasili na wakakubali kuishi na binadamu wafugwe, ni kama vile sasa hivi ukija ukaenda Thailand, ukienda India, hawa tembo wanavalishwa mpaka mashada, wanatembea barabarani na ndio maana utalii wao umekuwa kwa sababu ya jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukienda India, nyani, tembo wanavishwa mashada, sasa sisi inakuwaje ng’ombe wanaenda kwao, linakuwa ni tatizo, kwa sababu hawa ng’ombe walitoka porini wakaja kuishi na binadamu, ni sawasawa na nyumbu akichukuliwa anakuja kuishi na binadamun wakapata mafunzon wanakuwa ni jamii katika sehemu yetu.

Sasa ifikie, sheria wanazozitunga za kuwazuia wananchi kuingia katika maeneo hayo na wao watunge sheria hao wanyama wasije katika maeneo yetu, tuwe balanced, vinginevyo kwamba ng’ombe akipita hata barabarani amekosea mchungaji amesinzia, linakuwa ni tatizo... (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Tabasamu.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Ndio.

NAIBU SPIKA: Sheria ni kwa ajili ya binadamu, sio kwa mnyama. (Makofi)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa nini hawa…

NAIBU SPIKA: Subiri kwanza Mheshimiwa. Kama ulivyosema, vizuri mwenyewe kwamba hana huo uelewa.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Ndio.

NAIBU SPIKA: Hawezi kutungiwa sheria kwa ajili yake yeye mnyama, yaani kwamba mnyama akivuka hapa atafanywa hivi, sheria ni kwa ajili ya binadamu, kwa ajili ya mahusiano ya binadamu. (Makofi)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru. Sasa hawa ng’ombe wametungiwaje sheria sasa wakivuka mipaka tayari sisi inakuwa ni tatizo kwetu. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Mimi najaribu kukuweka vizuri kwa sababu ukisema wameenda kwao, basi maliasili wapo sahihi kuwazuia wale ng’ombe wabaki kule. Najaribu kukuweka vizuri ili mchango wako uupeleke kule unakotaka uende. Ukisema ng’ombe wamerudi kwao kwa namna hiyo, maana yake Maliasili wapo sahihi kuwazuia wale ng’ombe kutoka tena, maana si wamerudi kwao, kwa mchango wako yaani, ndio unamaanisha hivyo.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, sasa…

NAIBU SPIKA: Sasa sijui kama ndio lengo lako, maana yake binadamu hawezi kwenda kumchukua tembo akaja naye nyumbani. Kwa hiyo hata hawa ng’ombe wakishaenda kule wabaki huko, si ndio kwao wamesharudi. Ndio mchango wako unachomaanisha ndio maana nakuongoza vizuri uende kule ulikotaka kusema. Ukisema wamerudi kwao maana yake Maliasili wapo sahihi kuwazuia, maana unafuata wa nini wakati wapo nyumbani. (Makofi)

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa uelewa huo, lakini ninachotaka kukwambia ni kwamba wale ng’ombe ni hayawani, hii sheria wanatakiwa watungiwe binadamu sio ng’ombe. Kwa hiyo anayetakiwa kukamatwa pale ni binadamu ndio akapigwa faini sio ng’ombe. Sasa hawa watu wa TAWA, watu wa Maliasili ninachotaka kuwaomba sana wakae tuje na mjadala wa kitaifa tukae watu wa Sheria na Katiba, watu wa Wanyamapori, watu wa Wizara ya Ardhi na sisi Wafugaji, kwa sababu hapa Wabunge sisi hapa Wabunge wote hakuna Mbunge anayetoka kwenye jimbo lake hakuna mifugo na hakuna Mbunge anayetoka katika jimbo lake ambapo hakuna eneo la game reserve au forest reserve. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wakati sheria hizi zinatungwa za kuweka haya maeneo ya forest reserve na game reserve, wakati huo nchi yetu ilikuwa na watu milioni kumi na mbili na hawa watu milioni kumi na mbili mwaka 1960 ni taarifa zilizopikwa, kwa sababu wakati huo kulikuwa hakuna simu, hakuna barabara, hakuna chochote, walipataje orodha ya watu kwamba Tanzania kuna watu milioni kumi na mbili na yalikuwa ni mapori. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa kwa hatua hiyo, sasa hivi nchi yetu, nchi haikui, ipo palepale ila wananchi wanaongezeka katika nchi yao na wanyama wanaongezeka, tuje na mjadala wa kitaifa kwa ajili ya hili jambo. Leo mifugo yetu, ukiichukua idadi ya mifugo iliyokuwepo mwaka 1960 na mifugo iliyopo leo vitu haviendani.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakupa mfano Geita Mjini kuna eneo la game reserve la kilometa mbili, inawezekana wapi na Geita ni Manispaa? Kuna Kwimba mita mia 600 kutoka Ngudu Mjini unaambiwa kwamba ni game reserve, mita 600, haviwezekani vitu kama hivyo na hiyo ukiangalia ramani ni ya mwaka 1953. Sasa leo tunajitawala, hatuwezi hata sisi wenyewe kutengeneza ramani zetu, tunatumia ramani za Mwingereza, ramani za Mjerumani! Waheshimiwa Wabunge hili ni jambo ambalo tuiombe Serikali, tupitie haya maeneo yote ziletwe hizi sheria, afadhali hii Burigi tumeisikia ni ya mwaka jana, sijui hii Selous ilikuwa ni mwaka gani, na hii Serengeti ilikuwa ni mwaka gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa hatua hii, hii mipaka imeingiliana na tunaomba mjadala wa kitaifa twende tukaokoe wafugaji wetu. Hawa ng’ombe wataisha kwa kupigwa risasi huko na hawa ndugu zetu. Bahati mbaya sana wanaowapiga risasi ni watoto wa wafugaji, watoto wa wakulima, tunawashangaa sisi hawa watoto wa maskini wenzetu wanaenda kututia umaskini wazazi wao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la kwangu lingine nataka kuishauri Wizara ya Maliasili na Utalii, watengeneze Zoo za kila Makao Makuu ya Mikoa, wasitegemee watalii kutoka nje, leo kuna ugonjwa wa Covid, sasa hivi hatupati watalii, tungekuwa tuna watalii wa ndani hapa hapa, Jumapili hii leo mimi nilikuwa naweza kwenda Kongwa na familia yangu tukaangalie wanyama.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Ahsante sana kengele imeshagonga Mheshimiwa Tabasam.

MHE. TABASAM H. MWAGAO: Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)