Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Haji Amour Haji

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makunduchi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. HAJI AMOUR HAJI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa ruhusa yako nami nawashukuru watu wote wa Wizara ya Utalii kwa ujumla. Mimi sitakuwa na maelezo mengi ya kuchangia hasa kwenye mambo ya Maliasili nitagusa kwenye masuala ya Utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika utalii zaidi nizungumzie mambo matatu au manne. Kwanza tufahamu wazi kwamba utalii ni biashara, utalii ni huduma, utalii ni miundombinu. Sasa wakati mwingine, wakati wa hoja hapa nilikuwa najaribu kusikiliza hoja zote hizi za Wabunge wote ambao wanaozungumza, nikaona kwamba kuna haja ya Wizara yenyewe maana yake kuwa na mdahalo maalum utakaowahusisha Wabunge pamoja na wataalam wa utalii kujadili suala la mfumo wa utalii wetu Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivi kutokana na ile michango mingi ambayo imetolewa ambapo kila mmoja kajaribu kuzungumzia upande wake hasa unaouzungumzia suala la utalii, kuna wale watu waliozungumza kwa kutoa mifano mbalimbali katika nchi tofauti ambazo wameshabihisha Misri, South Africa pamoja na nchi zote zilizokuwa na utalii wa hali ya juu. Tufahamu wazi kwamba nchi hizo zote hizo ambazo zimezungumzwa kwa mifano, tukiangalia ile nature ya zile nchi maana yake kunakuwa na identification ya kitu wanachokitangazia hasa katika nchi zao. Kwa mfano kama nchi ya Misri, ukiangalia hasa kivutio chao kikubwa maana yake pale watakuwa wanazungumzia suala la pyramid. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukizungumzia suala la South Africa, utalii wao mkubwa maana yake unategemea kumbi za mikutano. Sasa sisi Tanzania maana yake tujaribu kuangalia kwamba identity ya Tanzania yetu hasa ni kitu gani? Maana yake ni kitu ambcho cha kuweza kukitizama kwamba, sisi Tanzania tunataka kuingia katika suala la utalii au tuko katika suala la utalii ambao ni biashara, ambao ni ajira kwa Watanzania, je sisi hasa identity yetu kuhusiana na utalii hasa ni kitu gani? Utakuta kila mmoja anazungumzia suala la vivutio mbalimbali, kwamba kuna kuna kivutio cha Mlima Kilimanjaro, kuna kivutio cha wanyama, kuna kivutio cha utamaduni, lakini kuna vivutio vingine tunaviita kwamba ni alternative katika suala la utalii. Sasa hapa tunatakiwa tuwe na utalii ule ambao ni identity kwa nchi yetu. Katika nchi yetu ukijaribu kutazama hasa sisi kwa Tanzania kipaumbele chetu hasa kwenye utalii ni kitu gani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho nijaribu kuishauri Wizara ni kwamba, wakati mwingine utalii kama ulivyo katika suala la mzunguko wake, utalii ndiyo kichwa ambacho nitasema kwamba kwa Wizara kinachoweza kuleta ile biashara yenyewe na kwa nini nazungumza hivyo? Nasema hivyo kwa sababu utalii wenyewe ndiyo uliosababisha vichochezi vya hizi maliasili maana yake kuweza kutambulika. Sasa bila ya utalii maana yake hivi vichochezi vyote, vivutio vyote hivi vya maliasili maana yake visingeweza kufahamika. Sasa ukiangalia kutokana na mfumo wetu wa Wizara ya Maliasili na Utalii maana yake maliasili imekuja juu sana ambapo ningetegemea sana utalii uje juu, ikisha maliasili ndio iwe ndani ya utalii, lakini sasa sisi tuko katika hali ambayo ni kinyume. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kingine tujaribu kuangalia suala la utalii; ukiangalia kwenye bajeti zetu hizo tumejaribu kugusa sana masuala ya international tourism, lakini suala la domestic hatukuligusa hata kidogo. Suala la domestic ambalo nalo lina umuhimu wake, lakini katika domestic nako tunahitaji tufanye kazi kubwa sana. Ili tuwe na domestic, wakati mwingine, pamoja na vivutio vyote tulivyokuwa navyo, lakini ningeshauri tutengeneze hizi amusement park katika yale maeneo ambayo tunakusudia wale wenyeji wawe wanafika na kupumzika. Kwa mfano kama hapa kuna Mbunge mmoja kazungumzia suala la Dodoma, kuna jiwe pale, kule kungetengenezwa amusement park, maana yake pengine ingekuwa moja ya kivutio cha ile jiwe na kisha ile amusement maana yake watu pengine wanaweza wakapumzika na kuendelea na shughuli nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa suala la utalii ni suala ambalo ni kubwa sana linahitaji huduma ambazo zilizokuwa bora, tunahitaji miundombinu iliyokuwa bora. Ili tuweze kufanikiwa katika suala hili la utalii, hayo yote yanatakiwa yazingatiwe kwa ubora wake, tuwe na huduma zilizokuwa bora, tuwe na miundombinu bora.

Mheshimiwa Naibu Spika, kimsingi, yote hayo juu ya utalii maana yake ni kuwa na amani. Bahati nzuri sisi Tanzania amani yetu inajitosheleza, kwa hivyo amani yetu ndiyo inaweza kutusababisha kwamba kila mmoja akawa ni kivutio kwa mtalii kuja nchini Tanzania kutokana na amani yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hayo, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)