Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Miraji Jumanne Mtaturu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Singida Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MIRAJI J. MTATURU: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Wizara hii muhimu ya Wizara ya Maliasili na Utalii. Nianze kwa kuwapongeza sana Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa kazi nzuri, lakini pia kwa wasilisho lao ambalo wameliwasilisha mbele yetu. Wasilisho hili limeonesha mipango mizuri ambayo wanaipanga kwa ajili ya mwaka mmoja ujao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze pia Katibu Mkuu pamoja na Watendaji wote kwa kazi nzuri wanayoifanya kuratibu shughuli hizi. Wote tunajua kwamba sekta ya utalii ni miongoni mwa sekta zinazotupatia fedha nyingi sana katika mapato ya nchi. Kwa hiyo ni maana yake ni kwamba, tunapotoa ushauri hapa tunataka tuendelee kuwa na uhakika wa mapato hayo ili kuisaidia nchi katika maendeleo. Wengi wamenukuu taarifa yake asilimia 17 ile ya Pato la Taifa, lakini tunapata asilimia 25 ya fedha ya kigeni, ambazo kwa kweli ni fedha nyingi zinazotuimarisha katika kuleta huduma za wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa maeneo yangu nitasema pamoja na kuwa TANAPA, TTB, pamoja na wenzetu wa TAWA wanavyoratibu shughuli za utalii, lakini kuna wenzetu hawa wa sekta ya binafsi ambao ni tour operators, wanafanya kazi nzuri sana kusaidiana na Wizara. Ombi langu ni dogo tu kwamba, kuna baadhi ya mambo ambayo yanapaswa tuwawezeshe na kuwaimarisha ili waweze kufanya kazi nzuri kwa niaba ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kiukweli watu hao wanafanya kazi nzuri na Wabunge wengi wamesema hapa. Hivyo, changamoto zilizopo ni vizuri tukazitafutia ufumbuzi ili waweze kufanya kazi nzuri na kusaidiana na Serikali, kwa sababu wao wanakutana moja kwa moja na watalii, wao ndiyo mawakala wanaowaleta watalii katika nchi yetu. Baada ya sisi kutangaza kama nchi, wao ndiyo wanaratibu kule katika shughuli zao mbalimbali kwenye vivutio vyetu. Kwa hiyo, niombe Serikali wapate muda, wakae na na hao wenzetu, waweze kuwapa taarifa mbalimbali zinazohusiana na taarifa za watalii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watalii hawa lazima tufikirie kwamba wao wanataka nini ili tuweze kuwatafutia kile wanachotaka, tusiwe tunaandaa sisi kwa utashi wetu. Ni sawasawa wewe una duka, stahili ya nguo fulani unauza unazozipenda wewe badala ya kutafuta nguo wanazopenda wateja. Kwa hiyo, hili ndiyo tatizo ambalo tunaliona liko mahali pale. Kwa hiyo niwaombe sana Wizara wakae na hawa tour operators waweze kuwaambia taste ya watalii wanaokuja nchini wanataka nini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kikwazo kimojawapo ni pale mfano Serengeti; wamekuwa wana limitation katika yale makambi, wamezuia kuwa na mahema 10, sheria inasema kuwe na mahema kumi, maana yake mnamlazimisha huyo tour operator aweze kuwa na kambi nyingi ambazo zinamwongezea mzigo. Kwa hiyo niombe sana angalau waongeze badala ya kuwa na hema kumi, ziwe hema 25 zisaidie kuwa na watali wengi katika eneo moja kwa ajili ya kusaidia kupunguza gharama ambazo wanaziingia hawa watalii ambao wanakuja kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niongelee tu kwamba wawe na mikataba, badala ya miaka mitatu basi waende hata minne na kuendelea ili wawasaidie kuwa na muda wa kutosha. Kama wachangiaji mbalimbali walivyosema leo limetokea tatizo la Covid-19 waweze ku-compensate gharama zao ambazo wamewekeza katika eneo hili, vinginevyo tutawafanya washindwe kuendelea kutusaidia.

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu ambalo ni muhimu sana, Wizara wanajua katika sekta hii kuna tozo na kodi 20 ambazo ni nyingi sana, zinawaletea vikwazo wale wanaoendesha sekta ya utalii. Mfano mdogo, ukiangalia, kuna tozo nyingi ambazo zimekuwa ni kikwazo, ni vizuri wakaziangalia upya mfano kuna TALA, kuna Halmashauri, kuna COSOTA, kuna NEMC, OSHA, Fire, Land Rent, Property Tax na Swimming Pool License yaani zote analipa huyu ambaye anatakiwa kuja pale. Maana yake nini, unamfanya huyu mtu awe na mlolongo na utitiri mkubwa wa zile kodi ambazo zinawaletea matatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba Mheshimiwa Waziri waangalie upya namna ambavyo wataweza kusaidia kupunguza gharama na mlolongo huu wa utitiri wa kodi, kwa sababu tunajua kwamba kodi inasaidia kuboresha maisha ya wananchi kweli, lakini ni vizuri watu walipe kodi kwa furaha ili kodi hii iwe endelevu kwa ajili ya kuipata kwa muda mrefu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, niongelee suala la sisi kujitangaza. Kuna mikutano mbalimbali, niiombe sana Wizara iweze kuhudhuria kwa ajili ya kutangaza vivutio vyetu katika dunia. Mfano, kuna wenzetu wa World Travel Market ambao ni WTM, tuendelee kwenda kule kwa ajili ya kupeleka taarifa zetu za vivutio katika nchi yetu ili kusaidia utalii wetu kuweza kutangazika duniani kote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya maneno hayo, naunga mkono hoja na naomba niwatakie kila kheri Wizara hii. Ahsante. (Makofi)