Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Ritta Enespher Kabati

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika hii hoja muhimu. Kwanza nianze na kuwapongeza sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri na Katibu Mkuu, Mr. Kijazi na watendaji wote wa Wizara kwa kazi nzuri ambayo wamekuwa wakiifanya na kutuletea bajeti hapa Bungeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, nianze na mradi wa REGROW. Mradi huu ni mradi wa kukuza utalii Kusini. Huu mradi kwa kweli, umeanza mwaka 2018 na tunategemea mwaka 2023 utakuwa umekamilika, lakini naona kama kasi ya mradi huu ni ndogo sana. Kwa sababu, huu mradi tunategemea sasa Nyanda za Juu Kusini tuna vivutio vingi, Wabunge wengi sana wa Nyanda za Juu Kusini wameongea vivutio vyao vilivyopo katika mikoa yao. Hata hivyo, kama huu mradu utakuwa haujakamilika bado tutakuwa hatujawasaidia wananchi wa Nyanda za Juu Kusini kupitia Utalii.

Mheshimiwa Naibu Spika, tulitegemea kwamba huu mradi ungeleta ajira nyingi za vijana, akinamama na watu wote na ungeongeza pato kubwa sana, lakini hatuelewi kama mwaka 2023, huu mradi utakuwa umeshakamilika au umeshaanza kufanya kazi yake. Kwa sababu Makao Makuu ya huu mradi yanategemea kuwepo Iringa lakini pia GN ndiyo kwanza juzi tu tumeona imesainiwa na yenyewe ilichukua muda mrefu sana kusainiwa. Pia bado hatujaona hata Makao Makuu yenyewe yameshaanza kujengwa na tunategemea sasa kutakuwa na vyuo vingi pale Iringa kwa ajili ya Nyanda za Juu Kusini, Vyuo vya Misitu, Maliasili na kila kitu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niombe Serikali ilichukue suala hili kwa umuhimu wake ili kuhakikisha kwamba huu mradi unakamilika na unaleta manufaa. Ikiwezekana labda kuwepo na mashindano kati ya Nyanda za Juu Kusini na Kaskazini, pengine labda hata watendaji wangechamka kuona kwamba haya mashindano yanaleta manufaa na pengine tungekuwa tunawapatia zawadi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia vivutio bado havijatangazika kiasi cha kutosha. Bado tunaweza tukawa na utalii wa ndani kama vivutio vyetu itakuwa watu wanavielewa na nafikiri Wabunge wengi sana wamezungumzia kwamba utalii wa ndani pia unaweza ukalipa, unaweza ukasaidia pia hata mafunzo kwa watoto wetu, wakue wakijua kwamba tuna utalii katika nchi yetu. Hiyo inaweza ikamjenga kwamba sisi tuna maliasili ambazo zinaweza zikatusaidia wananchi wote. Kwa hiyo, niombe kwa kweli matangazo yaongezeke, biashara ni matangazo. Matangazo yakiwa mengi, vivutio vyetu vitaeleweka na wananchi watakwenda hata kuviangalia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine nielezee kuhusu Ruaha National Park. Kwa kweli, hii mbuga ni ya pili kwa ukubwa na niliona hata Mwenyekiti wa Kamati aliizungumzia kwamba hii mbuga imesahaulika wakati ina wanyama wazuri, ina wanyama wengi, barabara haifikiki kabisa. Maana hii ingesaidia hata utalii wa ndani kama barabara ingekuwa inafikika. Hata sisi wenyewe Wabunge, nishukuru kwamba Kamati ilikwenda kutembelea na imeona changamoto nyingi sana zilizopo katika Ruaha National Park. Kwa hiyo, niombe kwa kweli ile barabara Waziri wa Ujenzi na Mawaziri wote wapiganie, watoe kipaumbele kwa hii barabara kwa sababu ni barabara ambayo itasaidia kabisa kukuza utalii katika nchi yetu na kuleta pato kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nizungumzie kuhusiana na utalii ulioko Iringa Manispaa. Kuna sehemu ambapo wakoloni walikuwa wananyongea watu, panaitwa kitanzini. Pale kuna kitanzi ambacho kuna boma lake limebomoka kabisa, yaani watalii wanatakiwa waje watembelee. Nitamwomba hata Mheshimiwa Naibu Waziri Masanja twende sio mbali sana, akaone jinsi ilivyo. Pamesahaulika kabisa wakati ni utalii mzuri. Kuna jiwe lile Gangilonga, lilikuwa linaongea zamani, hata watalii wakienda…kutembelea pale wanapata madhara wanavamiwa. Kwa hiyo, ni vizuri hivi vivutio vingewekewa mkakati kwanza viwe vinafikika na viwe vinatangazika, lakini tatizo kubwa kwenye halmashauri zetu hakuna Maafisa Utalii. Kwa hiyo, unakuta kwamba, kuna Maafisa Kilimo, kuna afisa nani, lakini Afisa Utalii bado Wizara haijawapa kipaumbele, hakuna connection kabisa, unaona wanajifanyia tu kazi wenyewe, hawana vifaa, hawafanyi kitu chochote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ingewezekana pengine labda Wizara itoe ruzuku kwenye halmashauri, ili hivi vivutio viweze kufikika na viweze kutangazika vizuri ili tuweze kuongeza pato kubwa sana katika halmashauri au kuwepo na kurugenzi inayoshughulikia mambo ya utalii tu katika manispaa zetu kwa sababu ndiko kwenye utalii mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie pia kuhusu mazao ya misitu. Tunayo mazao ya misitu Mufindi, Kilolo na kwingine kwingi Njombe, lakini tunaona tozo zimekuwa nyingi sana, karibu tozo 13 kwenye mazao ya misitu. Wananchi wengi wengine wamepanda haya mazao ili yawasaidie kusomesha watoto, yawasaidie kama ajira pia, lakini tozo zikiwa nyingi bado tunaona hatujamsaidia Mtanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho kabisa nikushukuru, lakini niombe kwamba, matangazo, Simba niwapongeze kwamba, wametangaza nchi kwa kutumia jezi zao…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

NAIBU SPIKA: Haya, kengele imeshagonga Mheshimiwa, ahsante sana.

MHE. DKT. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Naibu Spika, asante sana na naunga mkono hoja.