Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Godwin Emmanuel Kunambi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa dhati kabisa kwa kuwa miongoni mwa wachangiaji. Nitajikita kwenye utalii wa ndani, sote tunafahamu kwamba sekta hii ya utalii ni sekta muhimu na mchango wake kwa Taifa takribani kwenye GDP inachukua asilimia 21. Mimi nieleze tu utaona hapa katika asilimia 21, asilimia karibu 17 ni fedha zinazotokana na watalii kutoka nje ya nchi. Sasa utaona kwa kiwango gani utalii wa ndani haufanyi vizuri.

Mheshimiwa Naibu Spika, nishauri tu, Wizara ya Maliasili na Utalii ijikite kwenye manmade tourism. Manmade tourism itatusaidia, kwa mfano, ukienda kule Dubai una-drive kilometa 100 kutoka city center, kuna eneo unakwenda linaitwa Camel Ride, unafika pale unapanda ngamia tu, unaendesha ngamia, ukitoka unapanda kwenye V8 unaruka ruka. Yaani jambo lenyewe ni la kawaida kabisa lakini watu wanakwenda na wanapata fedha kule Dubai. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, niseme tu Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana hii atusaidie. Aongeze thamani ya maeneo yetu ya utalii, kwa kuwekeza kwenye utalii ambao tunauzungumzia manmade tourism.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine watu wengi wamezungumzia migogoro baina ya wananchi na wahifadhi. Naomba niseme hili ni janga la Taifa, hili tulipofikia sasa ni janga la Taifa. Kuna Watanzania wanaishi kwenye nchi hii kama wageni, hasa wanaoishi maeneo ya mipaka ya hifadhi, hawajui kesho yao. Sasa jambo hili lifike mwisho, tutakuwa tunajadili kila siku humu tufike mahali tuseme inatosha. Hatuwezi kuwa tunakaa humu tunajadili kitu hicho hicho wakati wote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niishauri Serikali naona hili jambo sio tu la Wizara ya Maliasili na Utalii. Niishauri Serikali, ije na mpango wa pamoja shirikishi. Wananchi washirikishwe lakini twende pamoja, kwa mfano, custodian wa masuala ya ardhi ni Wizara ya Ardhi, Maliasili wao wanakabidhiwa tu kulinda. Leo hii mimi nashangaa kuona Maliasili nao wanakwenda kuweka mipaka, sasa kazi ya Wizara ya Ardhi itakuwa ni kazi gani? Nadhani Wizara ya Ardhi iachiwe jukumu lake, libaki pale pale na kuna baadhi ya maeneo hakuna migogoro, Wizara ya Ardhi imeshafikia imefanya hadi mpango wa matumizi bora ya ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano pale kwangu Mlimba Kijiji cha Ijia kimeshasajiliwa kwa mujibu wa sheria na tayari kina mpango wa matumizi bora ya ardhi, lakini mpaka leo wananchi wale wanaishi kama ugenini. Hivi punde wiki iliyopita walikuja hapa wananchi tisa wamelala pale stendi, asubuhi napewa taarifa. Eneo hili halina mashaka, kijiji kimesajiliwa kwa mujibu wa sheria na wananchi wale wangepaswa kuishi bila bugudha. Niombe na niwapongeze pia Waziri wa Ardhi kwa kweli kuna baadhi ya maeneo tayari mipango ya matumizi bora ya ardhi yamekwisha.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tushirikiane kazi ya Wizara ya Maliasili na Utalii ni kuomba ramani kwa Wizara ya Ardhi, waende wakazingatie hizo ramani. Yaani hilo jukumu sio la Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara inajipa mzigo ambao isingefaa ijipe, eneo hilo nadhani tulitazame.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende katika eneo lingine ambalo pia hapa nimshukuru kwa dhati kabisa Mheshimiwa Waziri. Ametusaidia wananchi wa Jimbo la Mlimba kutoa vibali vya kuvuna mpunga wetu, ahsante sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, changamoto inayokuja kwa wananchi wale, naomba, tufanikiwe kwenye eneo hili Mheshimiwa Waziri anapokuja kuhitimisha basi atoe tamko. Wananchi wangu wamekuwa waoga sasa, Meneja wa TAWA anasema njoo uombe vibali, wananchi wanasema wanatuorodhesha ili watukamate tena. Kwa hiyo, hawawezi tena kuvuna. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, namwomba shemeji anapokwenda kuhitimisha bajeti yake atoe tamko kwamba, suala la kuhakikisha wananchi wa Mlimba...

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kunambi Taarifa Rasmi za Bunge hazitajua nani ni shemeji yako humu ndani.

MHE. GODWIN E. KUNAMBI: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri wa Maliasili na Utalii ni shemeji yangu.

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme tu kwamba, Waziri aje atoe tamko hapa ili awatoe hofu wananchi wa pale Ijia kwamba, Wizara imeruhusu wavune kwa wakati, wakimaliza kuvuna maeneo yale ni vyema sasa yakaendelea na shughuli ambazo zimekusudiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine, nizungumzie kuhusu hawa vyura walioelezwa, vyura ambao wanazaa na kunyonyesha, wapo pale Kihansi Udagali. Sasa niombe tu ndugu zangu Mheshimiwa Waziri atusaidie, kuna watu hawa academic tourism, wakija pale na wenzetu wa TANESCO wamefanya kazi nzuri sana wameweka hadi rest house pale. Kwa hiyo, mtalii akija pale analala vizuri, waje waone academic tourism, waje Mlimba pale Kihansi kuna vyura wanaonyonyesha na wanazaa. Duniani kote hawapatikana wanapatikana pale tu Kihansi.

Mheshimiwa Naibu Spika, eneo lingine ambalo nataka niliseme, kuna hoja hapa ya msingi, nihitimishe kwenye hoja hii ya eneo hili la utalii wa ndani. Tukijiuliza hapa maswali Wabunge wote humu ndani ni wangapi wameshafanya utalii wa ndani hapa? Jibu utakalopata ni wachache kati yetu. Kwa hiyo, nitoe rai kwa Wabunge, tuwe sehemu ya utalii wa ndani, twende tukahamasishe kama mabalozi wa utalii wa ndani ili nchi yetu ipate fedha za ndani.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii na Mungu atubariki sote. (Makofi)