Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Minza Simon Mjika

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MINZA S. MJIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru sana kwa kunipatia nafasi hii, lakini kulingana na ufinyu wa muda nitaenda haraka sana na nitasema tu baadhi ya vitu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru sana Waziri pamoja na Naibu Waziri kwa hotuba yao nzuri iliyosheheni matumaini kwa Watanzania. Nimefurahi sana kwa mambo mengi ambayo wameweza kuyasema mle, kama yatatekelezeka hawatakuwa na ugomvi na wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaingia moja kwa moja katika Mkoa wangu wa Simiyu. Mkoa huu una wilaya tano, lakini wilaya nne ndizo zinazoshambuliwa na Wanyama. Kuna Wilaya ya Busega, Bariadi, Itilima na Meatu. Maswa tuko vizuri tunamshukuru Mungu. Nashukuru kwa upande wa Wilaya ya Busega, Mheshimiwa Songe ameweza kuongea kwa hiyo, sina haja ya kurudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niingie katika Wilaya ya Bariadi. Bariadi tunashambuliwa sana na wanyama, tembo hawa. Kwa mfano, Kijiji cha Nyawa, Gibeshi, Kindwabihe, Mwasenase pamoja na Ihusi, kule kuna mashambulizi makubwa sana ya tembo. Tunaomba Serikali iangalie sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda niingie moja kwa moja tena kwenye Wilaya ya Itilima. Napenda tuishukuru kwanza Serikali yetu. Ninashukuru kwamba tuna gari la wanyamapori katika Wilaya ya Itilima, tayari wameshaleta, tunashukuru. Kwa hiyo, msaada mkubwa umepatikana pale japokuwa kuna vijiji ambavyo vinahangaishwa sana na hawa wanyama; kuna Mwaswale, Nyantuguti, Nkuyu; hivyo ni baadhi ya vijiji tu ambavyo vinashambuliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiingia katika Wilaya ya Meatu ninashukuru Mheshimiwa Mpina ameongea na baadhi ya vijiji amevitaja pamoja na changamoto zake. Tunaomba kupata msaada, katika hivyo vijiji tunahangaika sana. Vijiji ni vingi sana; tukiangalia kwa mfano katika Wilaya ya Meatu kuna Mwasengela, Mbuga ya Banyha, kuna Sakasaka, Nyanza, Igobe, Longaloniga; vijiji ni vingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiingia kwangu ninakotoka Meatu kuna Mwanyahina, Makao, Mwagwila, Mwajidalala, Busia, Mwanzagamba, Mwangudo, kote kule wanyamapori hawa tembo wamesambaa sana. Tunaomba msaada kutoka Serikalini.

Katika Wilaya ya Meatu hatuna hata gari la wanyamapori. Askari wapo, lakini hakuna usafiri. Hata tembo wakionekana wanafanya uhalifu sehemu, akipigiwa hana usafiri, inakuwa ni shida. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali iliangalie sana hili. Hatuna ugomvi na Serikali, lakini tunaomba watutendee ilivyo sahihi. Akina baba wengi katika Mkoa wa Simiyu, hususan hizo wilaya nne ambazi nimezitaja wameshakuwa doria, hawana combat, hawana silaha, hawana usafiri, lakini ni watu wa kulinda wanyamapori. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuomba tuone. Watu wengi sana wamepoteza maisha, akina baba, akina mama na watoto, hususan wanafunzi wanapoenda shule. Kwa mfano, mwaka juzi 2019 kuna mwanafunzi mmoja aliuawa katika Kijiji cha Mwangudo, mtoto wa Darasa la Pili anaenda shule. Alikutana na tembo, alimjeruhi vibaya sana yule mtoto, alimsaga na akaisha kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba vitu kama hivi tunavyoviongea tunaweza tukaona rahisi, lakini wananchi wanalia sana na wanateseka sana. Tunaomba basi Serikali ifanye hima itufanyie msaada huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Napenda kuunga mkono hoja. (Makofi)