Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Neema Gerald Mwandabila

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. NEEMA G. MWANDABILA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nami niungane na wenzangu kukupongeza, kwa mara ya kwanza unatuongoza vema. Tunaamini tumepata Mwenyekiti sahihi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa uhaba wa muda nitaweza kuongelea mambo machache ambayo naamini Wizara ikiyafanyia kazi watakuwa wametunusuru sisi wananchi wa Mkoa wa Songwe, hususan Wilaya ya Songwe yenyewe.

Mimi napenda kusema kwamba nilitamani sana niwapongeze watendaji wa Wizara hii kwamba wanafanya kazi vizuri, lakini nikikumbuka machungu ambayo tunayapata na watendaji wao wa chini kule, roho inakuwa inaniuma kidogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme hii ndiyo Wizara pekee ambayo haina mahusiano mema nasi wananchi. Kimsingi tumekuwa tunalianao kila eneo. Tunaona kabisa Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri ni watu wema, tunawaza ni kwa nini watu wao kule chini wanakuwa na roho za kiukatili namna hii kiasi kwamba inakuwa kama wao Kanisani hawakujui? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea suala la wavuvi ambao wanavua katika Ziwa Rukwa. Tunajua uvuvi ni kazi kama kazi nyingine na wale wavuvi wanafanya kazi zile kuweza kujipatia kipato ku-sustain maisha yao na watoto wao na ndugu zao wa karibu; lakini mambo yanayotendeka katika Hifadhi ya Katavi ni mambo magumu ambayo yanasikitisha. Wavuvi wananyanyaswa sana. Sidhani kama taarifa hizi zingekuwa zinafika kwao viongozi wetu; Waziri na Naibu Waziri kama haya mambo yangekuwa yanaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina taarifa kutoka kwa wavuvi ambao wanapatikana katika kambi za Kichangani, Malangali, Kasimanyenze, Kambang’ombe na nyinginezo, kule kuna kambi nyingi, wavuvi wale wanalalamika kwamba, ma-game, sasa sijaelewa ma-game na uvuvi kwa nini wanawaingilia wavuvi kwenye kazi zao eti kisa tu hifadhi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ma-game wanaolinda hifadhi ya Katavi wamejitengenezea mazingira ya kujipatia kipato kisicho halali. Wamekuwa ni watu ambao wanawatishia wavuvi kwamba wakiwakuta kando kando ya ziwa wanaendelea na shughuli zao, wanawatishia na kuweza kuwapora mali zao. Pia wamejitengenezea utaratibu wa kupata rushwa. Watu hawa wamejitengenezea utaratibu wa kupata shilingi 300,000 kila wiki kwa kigezo tu kwamba, wavuvi wanaofanya kazi kule, hawatakiwi kukanyaga ardhi ya hifadhi. Mwisho wa siku tunajiuliza kwamba, ile hifadhi imewekwa kwa ajili ya kututesa au imewekwa kwa ajili ya kutusaidia kama Taifa tuweze kupata kipato? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna kisichoweza kuongeleka. imi naamini kabisa Wizara inaweza ikatafuta namna ya ku-compromise na wavuvi ili mwisho wa siku Serikali ipate pesa yake. Badala ya hizi shilingi 300,000 kuendelea kuingia mifukoni mwa watu. Serikali ingeweza kutoa vibali halali, kama inavyotoa vya watu kuwinda na kadhalika; wavuvi wanapovua samaki wao waweze kuwaanika kandokando ya ziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, wavuvi wamekuwa wakiendelea kupata tabu hii. Pale wanapoonekana hawana pesa ya kuwapa, wanachomewa vitu vyao; wavuvi wanachomewa mitumbwi, wavuvi haohao wanachomewa ngalawa, lakini chumvi zao zinaloanishwa. Pia hata samaki wale ambao wameshakauka wanachomwa moto. Sasa hebu jiulize, mtu kawekeza pesa yake, ni mtaji, ndio inamfanya afanye maisha, vinachomwa halafu anaishije? Anaenda kuanza vipi maisha upya? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kwa mambo haya ambayo yanakuwa yanaendelea, kwa sisi wanawake tunajua kabisa, imeshaelezwa hapa, ndio wanaofanya mazoezi ya kubaka wanawake. Sasa najiuliza kwamba, kuwa mwanamke ni kosa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niseme tu kwamba, kwa kweli sina amani na askari hawa. Napenda kuona kwamba Serikali inakuja na tamko au na neno ambalo kwa kweli litatufariji kuona kwamba wako kwa ajili yetu na siyo kwa ajili ya wanyama tu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuunga mkono.