Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Antipas Zeno Mgungusi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Malinyi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa nafasi. Awali ya yote nakupongeza wewe kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti, lakini pia umetosha kwenye kiti kana kwamba ni mzoefu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, nitoe shukrani kwa Wizara ya Maliasili. Pamoja na changamoto nyingi za Bonde la Kilombero, nimekuwa tukipishana nao mara nyingi tunagombana, lakini walau kwa kidogo tunashukuru kwamba wametoa idhini wananchi wetu waliolima kule waweze kuvuna kipindi hiki ambapo mpunga upo tayari. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hilo, niseme tu, natoa pongezi kwa Watendaji wa Jeshi USU la Uhifadhi, Kamishna wa Uhifadhi wa Ngorongoro Daktari Manongi; Kamishna wa TFS, Profesa Silayo Dos Santos, Kamishna Kijazi wa TANAPA, ambaye kwa sasa amepanda kuwa Katibu Mkuu wa Wizara. Nawapongeza kwa utendaji mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yote kwa yote, niseme utalii nchi hii unakumbana na changamoto kubwa mbili; ya kwanza, ni utegemezi wa aina moja ya utalii kwa maana ya utalii wa wanyamapori ndiyo sehemu ambayo tumelalia sana. Changamoto ya pili ni utangazaji wa utalii usiotosheleza. Kipande hicho hicho cha utangazaji wa utalii na chenyewe kina changamoto mbili; ya kwanza ni ufinyu wa bajeti; na ya pili ni ubunifu usiotosheleza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa katika suala la kutegemea utalii wa aina moja, zaidi ya asilimia 80 au 90 ya watalii wanaokuja Tanzania wanaenda kwenye Hifadhi ya Taifa, kwenye Mapori ya Akiba na maeneo mengine mbalimbali ambayo tumejaliwa kuwa nayo. Ila ukiangalia takwimu za nchi ambazo zinafanya vizuri duniani na Afrika kiutalii kwenye kumi bora zote za Afrika, zimetajwa hapa asubuhi; Morocco, South Africa na maeneo mengine hawana vivutio vingi kwa maana ya wanyamapori, hawana hifadhi nyingi nzuri kama za kwetu, lakini wanafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa jambo hili linatakiwa liifikirishe Wizara, Serikali na nchi kwa maana tunakoelekea utalii wa wanyamapori unaweza ukapotea na utalii mwingine mbadala ndiyo ambao unashika hatamu. Kwa hiyo, naomba Wizara ichukue hili kama changamoto. Tuna vivutio vya asili; ukiangalia beach ya Lake Tanganyika, kule Kirando na Kipili Nkasi, ukiangalia tuna kimondo pale Mbozi, Olduvai Gorge kule Ngorongoro na maeneo mengine mengi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utalii wa kitamaduni ni vitu ambavyo vinapendwa sana na watalii wengi. Kwa hiyo, naishauri Serikali tujikite kwenye maeneo hayo. pamoja na kwamba tunafanya utalii wa wanyamapori, lakini utalii mbadala hasa wa kitamaduni uweze kuzingatiwa na kuangaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto ya utangazaji wa utalii, nilizungumza suala la kibajeti, ni kweli bajeti yetu ni finyu, Bodi ya Utalii ambayo ina dhamana ya kufanya matangazo, imekuwa ikitoa fedha ambazo siyo toshelezi kulinganisha na nchi shindani, lakini hata hicho hicho kidogo hatufanyi ubunifu kuweza kukitumia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninafahamu hata tufanye vyovyote vile hatuwezi kuwa na fedha nyingi kama nchi nyingine ambazo zimetajwa saa zile, lakini ubunifu ndiyo kila kitu. Nitolee mfano, kufanya matangazo ya utalii kwenye Media kubwa kama CNN kwa dakika moja haipungui milioni 200, 300 na kuendelea. Ukweli ni kwamba tunaweza tusimudu sana, lakini ubunifu ni kwamba television zote kubwa; CNN na Aljazeera na wengine wana vipindi vya Makala kwa maana ya documentaries, wanaonyesha uhaba wa maji Afrika, Sudan, Tanzania na kwingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaweza kufanya lobbying tukatumia documentaries, tukawaalika wakafanya kama documentary kuonesha vivutio vyetu, sisi tunakuwa tumepitia humo humo, tukaonwa na dunia nzima kwa bei rahisi ambayo pengine inaweza ikawa bure kabisa kuliko kutegemea kujaza bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia bajeti ndogo ambayo imekuwa ikitolewa kwa ajili ya Bodi ya Utalii, maisha yangu yote ambayo nimekuwa Wizarani haikuwahi kutolewa hata kwa asilimia 90. Bajeti inatengwa, lakini fedha ambazo zinatolewa kwa ajili ya utekelezaji kazi ni ndogo mno. Kwa hiyo, katika hali hii hatuwezi kushindana na mataifa mengine ambayo yametutangulia Afrika na dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili kuongezea kwenye ubunifu, nilikuwa naishauri Serikali, jambo hili Wizara ya Maliasili isaidiwe na Serikali kiujumla, kwa maana kwenye balozi zetu; watalii wengi tunawategemea wanatoka kwenye mataifa ya nje, tunawaagiza mara kadhaa mabalozi wafanye kazi kuleta watalii Tanzania, lakini unaweza ukakuta wenyewe hawana uelewa mkubwa juu ya suala la utalii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba nishauri Wizara ya Maliasili na Mambo ya Nje wakashirikiana, tuwapeleke waambata wa utalii kwenye balozi zetu. Kuna waambata wa jeshi, kuna waambata wa idara, wapo kwenye balozi. Kwa hiyo, naomba Wizara ya Mambo ya Nje na Maliasili zishirikiane tuwaweke Maafisa Utalii kwenye balozi zetu waweze kuwasaidia mabalozi kuweza kutangaza nchi yetu. Kinyume na hapo, tutaishia kuwalaumu mabalozi tu, lakini kazi haitaonekana kwenye sekta hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikihama kwenye eneo hilo, kuna suala la vita dhidi ya ujangili. Mara nyingi kumekuwa na malalamiko na Jeshi USU la Hifadhi kutokana na kutotosheleza kwa manpower, kwa maana wapiganaji ni wachache. Mara kadhaa TANAPA, Ngorongoro, TFS na TAWA wamekuwa wakilalamika pengine na kuhitaji nguvu kazi kwa ajili ya ziada. Niseme, jambo hili tuli-support lakini ushirikiano uwe mkubwa kwa Serikali kiujumla wake. Tukimwachia Maliasili peke yake hataweza kulingana na manpower aliyonayo. Kwa hiyo, naomba tu, Wizara ya Ulinzi, Wizara ya Maliasili kuunganishwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, wafanye ushirikiano.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna vijana wanamaliza JKT, wanakaa kwenye makambi yetu, wanajitolewa miaka miwili kumwagilia maua, kupanda bustani; wamekuwa trained, wale ni askari, wachukuliwe, wapate short course kidogo ya uhifadhi, waripoti kwenye Jeshi USU la Uhifadhi, wakisimamiwa na Maafisa wa kule waweze kufanya operation ambazo zinapaswa hizo za kisheria. Kinyume chake tutalia suala la kuongeza askari, inaweza ikachukua miaka mingi tusiweze kumudu kupata idadi toshelezi, wakati tayari tuna nguvu kazi ya JKT au Jeshi la Wananchi Wapiganaji ambao wapo tu sasa hivi ambao ni ziada. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba hili jambo lisiachiwe Wizara ya Maliasili peke yake, askari wengine watumike, wapate course ya muda mfupi. Kule watalipwa tu posho kwenye paramilitary ile ya conservation, mishahara yao itaendelea kwenye majeshi yao ya msingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe mfano kwenye suala la TFS kwa maana Wakala wa Huduma ya Misitu, wamekutana na changamoto kubwa za kihifadhi. Doria zimekuwa ngumu, changamoto ni kubwa, askari wanalemewa hasa kwenye misitu yetu ambayo ipo karibu na mipaka. Kule Kigoma Misitu ya Makere Kusini na Kaskazini, majangili wamekuwa wakiingia kufanya uvunaji haramu wa misitu, TFS wanalemewa. Mara kadhaa kumekuwa na incidents wapiganaji wanazidiwa, wengine wanauliwa, mambo kama haya huwa hatutangazi, huwa hayasemwi, lakini yapo. Kwa hiyo, kuna haja ya Jeshi la wananchi au JKT kuongeza nguvu kwa TFS na Jeshi la Uhifadhi kwa ujumla wake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kuna suala la muundo mzima wa conservation paramilitary, Jeshi USU la Uhifadhi. Sasa kwa sababu masuala mengi ni ya kijeshi, siwezi kuyasema hapa, lakini nimeandika kitabu changu cha Maisha Yangu ya Uaskari kama Afisa wa Jeshi USU, humu kuna madini mengi. Naomba Wizara wakichukue, watapata vitu vingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kwa upendeleo, Jeshi la Uhifadhi kwa sasa lina-operate differently kwa maana ya kila…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa.

MHE. ANTIPAS Z. MGUNGUSI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru, ahsante. Naunga mkono hoja. (Makofi)