Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Joseph George Kakunda

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sikonge

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. JOSEPH G. KAKUNDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nami niungane na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na timu yake yote, akiwemo Naibu Waziri, kwa hotuba nzuri, fupi, ambayo inaeleweka; brief to the point. Hongera sana Mheshimiwa Waziri. Kwa maana hiyo, naunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri kwa asilimia mia moja. Ndiyo maana nasimama hapa kuzungumzia suluhisho badala ya malalamiko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo nitakalolizungumzia ni la Jimbo langu la Sikonge. Jimbo la Sikonge au Wilaya ya Sikonge, ina eneo la kilometa za mraba 27,873. Eneo la Mkoa wa Kilimanjaro linaingia mara mbili na eneo la wilaya ni kubwa kuliko Mkoa wa Tanga. Kati ya kilometa hizo, eneo lililohifadhiwa ni kilometa za mraba 26,834, sawa sawa na asilimia 96.3 ya eneo lote la wilaya. Eneo ambalo wananchi wanaruhusiwa kuishi na kufanya shughuli zao za kiuchumi ni eneo la kilometa za mraba 1,039.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hizi takwimu hata kama mtu yeyote akiamua ku-google Sikonge District, atazikuta ziko hapo, Kimataifa, hata kama yuko Marekani. Hii ndiyo concern yangu kubwa na ni concern ya wakazi wa Sikonge kwa sababu moja kubwa. Wakati wa kupima eneo la kuhifadhi, mwaka 1954 mpaka 1956, wakazi wa Sikonge wakati huo ilikuwa kata tu, kwa ujumla wao hawakuvuka hata 30,000. Leo tuna wakazi wanaopindukia 350,000 katika eneo lile lile dogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati wanapima eneo hilo lililohifadhiwa mwaka 1954 hadi 1956, wakazi wa Sikonge wakati ule hawakuwa wafugaji wa asili. Kwa hiyo, ng’ombe kule hawakuzidi 2,500 kwa eneo lote. Leo tuna ng’ombe zaidi ya 400,000 kwa eneo lile lile dogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana nasema wakati mwingine lazima ndugu zetu walioko Serikalini tutumie busara katika kutekeleza sheria. Kwa sababu eneo hilo sasa lime-burst, hakuna sehemu tena ya makazi, hakuna sehemu ya ng’ombe, mtu yeyote anayefuga ng’ombe ataingiza kwenye hifadhi. Asipoingiza kwenye hifadhi atalisha mashamba, kwa sababu hakuna eneo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii imesababishwa na makosa mawili makubwa ambayo yalifanywa na Serikali. Kosa la kwanza, mwaka 1959 Gavana wa kikoloni baada ya kuwa amepata taarifa ya uharibifu wa mazingira katika eneo la wafugaji kule Usukumani hasa, akatoa decree, inaitwa order, kwamba sasa kila mfugaji kwenye maeneo yale anatakiwa apunguze mifugo ibaki 100 au chini ya hapo kwa ajili ya kutunza mazingira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya sana kipindi kile hakukuwa na Maafisa wa Serikali wa kuweza kutekeleza hiyo decree. Kwa hiyo, ikabidi isubiri decree kutotekelezwa mpaka tulipopata Uhuru mwaka 1961. Tulipopata Uhuru mwaka 1961, Mwalimu Nyerere akasema hii decree hatuwezi kuitekeleza katika nchi huru kwa sababu nchi hii Tanzania ina maeneo mengi ambayo bado wananchi wanaweza wakahamia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo lilikuwa ni kosa la kwanza, kwa sababu uhamiaji ule sasa wa kutoka maeneo yale ya wafugaji, kuja kwenye maeneo ya Wilaya ya Sikonge, haukuratibiwa na Serikali. Hilo lilikuwa ni kosa. Kwa hiyo, matokeo yake, wameingia watu wengi sana Sikonge na hatuna eneo la kulima wala kufugia na mifugo ni mingi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kosa la pili la Serikali; ilikuwa ni wakati wa operesheni vijiji, walikwenda kuanzisha Vijiji vya Ujamaa karibu kabisa na hifadhi ndani ya mita 500 unaingia hifadhi. Nina kata 16, nina vijiji 40 viko ndani ya mita 500 unaingia kwenye hifadhi; kosa kubwa la Serikali hilo. Unategemea mtu ambaye yuko ndani ya kijiji mita 500, asiingie kwenye hifadhi? Kwa hiyo, hilo lilikuwa ni kosa. Ndiyo maana mimi niko hapa kwa sababu matokeo yake yamesababisha adha kubwa na usumbufu mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono suluhisho ambalo linaletwa na Serikali la kuanzisha nature reserve kwenye maeneo yote haya. Nature reserve ambayo sasa itatoa nafuu kwa kupunguza eneo la hifadhi ili wananchi wabaki na eneo kubwa zaidi la kulima. Wananchi hao kupitia Halmashauri tumeshaanza kuzungumza nao namna ambavyo watashiriki kulinda ile nature reserve mpya ambayo itaanzishwa ambapo itaacha maeneo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hilo ndilo suluhisho ambalo kwa kweli naomba kulileta mbele ya Bunge lako Tukufu ili Mheshimiwa Waziri na timu yake yote waje Sikonge, tukae pamoja tuweze ku-determine kwamba sasa eneo ambalo ni la nature reserve lianzie wapi? Lazima tulinde miti yetu mizuri kabisa; Mininga na miti mingine ya thamani tuilinde, lazima tulinde maeneo ya shoroba, lazima tulinde mbuga ambazo zina wanyama bado, tunazifahamu sisi. Kama hawafahamu wao, watuulize, sisi tunazifahamu zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nimesimama hapa kuleta suluhisho la kudumu ambalo litaondoa malalamiko ya wananchi kutokana na yale makosa mawili makubwa ya Serikali ambayo yalifanyika ambayo yameifanya sasa Sikonge ime-burst, hakuna sehemu ya kuishi, hauna sehemu ya kulima wala kufanya shughuli za kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, baada ya kuiwasilisha hoja hii hapa Bungeni na kuunga mkono hoja ya Mheshimiwa Waziri; na ninamwamini huyu bwana kwa sababu tuliajiriwa siku moja Serikalini, mambo haya niliyowasilisha atayatilia mkazo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ahsante sana.