Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Cecilia Daniel Paresso

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nami naungana na Wabunge wenzangu kukupongeza kwa nafasi hiyo ya kuwa Mwenyekiti wa Bunge. Hongera sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana.

MHE. CECILIA D. PARESSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mchango wangu utajikita katika mambo yafuatayo: kwanza, sote tunatambua umuhimu wa sekta ya utalii kama nchi, kwa sababu ni sehemu ya kutoa ajira, kuchangia pato la Taifa, kuiingizia nchi fedha za kigeni. Utalii wetu umejikita zaidi kwenye utalii wa wanyamapori. Hivyo basi, bado tuna fursa nyingine nyingi za kupanua zaidi utalii wetu ili uendelee kuwa na manufaa kwenye nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haina budi kuhakikisha utalii wetu unakuwa endelevu kwa kuendelea kutunza maeneo yetu ya utalii, kuvihifadhi, kuhakikisha haviharibiwi, kuhakikisha kile ambacho kinawavutia wageni kuja na kutupatia faida kama nchi, basi vinatunzwa kwa nguvu zote na kuhakikisha vinakuwa endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna athari za kutoweka hatuoni uendelevu wake kama bado upo ama utaweza kuendelea kuweko kwa miaka 10, 20 au 30 ijayo. Kwa sababu nyingi ambazo zinajitokeza, kwanza, mapito ya Wanyama, maarufu kama shoroba, nyingi zimevamiwa na wananchi. Zinavamiwa kwa sababu hatukuwa na mipango bora ya ardhi kwenye maeneo yetu. Pia kuna ongezeko la idadi ya watu na kuna ongezeko la matumizi ya ardhi. Siku zote napenda kusema ardhi haiongezeki, idadi ya watu inaongezeka, mahitaji na utumiaji wa ardhi unaongezeka kwa kasi kubwa kwa sababu ya idadi ya watu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, ni lazima Serikali mwone namna gani ardhi yetu tunapangia matumizi bora na kuiwekea sheria; kama ambavyo tumetungia sheria maeneo yetu ya hifadhi, hivyo hivyo ukienda kwenye maeneo ya kilimo haina budi kuwa na sheria maalum ili wasiingiliane. Hivyo hivyo kwa wafugaji itatusaidia angalau kupunguza migogoro ambayo inajitokeza kwa wingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya pili, Hifadhi ya Ngorongoro. Kwanza tunamshukuru sana Mheshimiwa Mama Samia, katika speech zake zilizopita ameweza kuonyesha kwamba tunahitaji kuendelea kuilinda Hifadhi ya Ngorongoro kwa nguvu zetu zote. Hifadhi ya Ngorongoro ni Kivutio cha Asili, na ni Hifadhi ya Urithi wa dunia toka mwaka 1979 na ni hifadhi ambayo inatambulika kama Hifadhi Mseto. Ni hifadhi ambayo ina wanyamapori na shughuli za binadamu na makazi ya binadamu humo ndani. Kwa hiyo, siioni Ngorongoro ya miaka 20 ijayo kwa sababu, matumizi mseto ilikuwa ina-apply miaka ya nyuma, lakini siyo leo. Leo shughuli za kibinadamu zikiongezeka, ule uhifadhi tunaotamani kuuona Ngorongoro utapotea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nampongeza sana Mhifadhi Mkuu wa Ngorongoro, wameanza kuonyesha mfano, kwa sababu Ngorongoro sasa hivi wamehama; Makao Makuu ya Hifadhi ya Ngorongoro imehama kutoka kule Ngorongoro iliko hifadhini na kuhamia Karatu. Ni nia ambayo ilikuwepo muda mrefu, haijawahi kutelezwa, lakini leo imetekelezwa. Nampongeza sana Mhifadhi wa Ngorongoro na timu yake nzima, na bodi yake kwa hatua hii muhimu ambayo sasa itatoa mwelekeo mzuri wa kuendelea kuifanya Serikali ipunguze matumizi ya watu na binadamu ndani ya Hifadhi ya Ngorongoro ili kuendelea kuilinda Ngorongoro ile ambayo tunaifahamu ilikuwa zamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukisoma ripoti ya CAG, ameonyesha mambo mengi kuhusiana na Hifadhi ya Ngorongoro. Kuna tatizo la magugu vamizi, ambayo yanahatarisha Wanyama. CAG kwenye ripoti yake ameieleza vizuri sana. Amesema kwamba management wamejitahidi kuondokana na hiyo, lakini bado kuna mkwamo. Kwa hiyo, Wizara muone namna gani ya kukabiliana na hayo magugu vamizi ili tuendelee kuona Ngorongoro inastawi na inaendelea kuwa urithi wa dunia kama ambavyo imetangazwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja yangu ya tatu, kuna mgogoro wa muda mrefu kati ya wananchi wa Kata ya Buger na Hifadhi ya Msitu Mara ambao unalindwa na TANAPA. Niseme yafuatayo: mwaka 2013 mwananchi mmoja alipigwa risasi mguuni na Askari wa TANAPA; tarehe 25 Mei, 2015 mwananchi mmoja alipigwa risasi akafariki; tarehe 28 Oktobam 2020 siku ya kupiga kura wananchi wa TANAPA waliwapiga risasi ng’ombe kumi wa mama mmoja mjane kwenye ile kata. TANAPA waliahidi watamfidia yule mama, lakini mpaka leo yule mama hajapata fidia hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tarehe 28 Desemba, 2020, watu saba waliingia kwenye msitu ule wa hifadhi, walikuwa wanakwenda kuchimba madini. Sitetei watu wanaoingia na kuvamia hifadhi na kutaka kuharibu hifadhi zetu, nachukizwa na utaratibu unaofuatwa baada ya hapo. Kama hao watu ni wahalifu, sheria zipo, tumezitunga ndani ya Bunge. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hao watu saba waliongia kwenye huo msitu, watu wanne mpaka leo hawajulikani walipo. Watu watatu walifanikiwa kutoroka, watu wanne inasemekana walichomwa mpaka kufa na Askari wa TANAPA. Haya ni mambo ambayo hayakubaliki. Sitetei uhalifu, lakini kuna sheria za kumchukulia hatua mhalifu yeyote. Sheria ziko very clear. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeshakuwa ni utamaduni wa kudumu wa mgogoro kati ya wananchi hawa wa Buger na Askari wa TANAPA. Ni eneo pekee ambalo Askari wa TANAPA hajawahi kukwaruzwa na mwananchi yeyote, ukilinganisha na maeneo mengine, labda inawezekana askari akauawa na wananchi kwa hasira; lakini kwa jinsi ambavyo wale wananchi walivyo, hakuna Askari aliyekwaruzwa wala kutolewa unyayo au kufanywa chochote kile, hakuna.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, tuone namna bora ya kumaliza mgogoro huu. Leo ninapoongea hapa askari wale wako kule, nasikia wanarekebisha beacon, ambao ni mgogoro wa muda mrefu. Hatujapata suluhisho, lakini tunakwenda tena kuendelea ku- create matatizo ambayo yanaendelea kujitokeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba sana Mheshimiwa Waziri, tuone namna bora ya kumaliza tatizo hili ili wananchi wale wakae kwa amani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. (Makofi)