Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Anna Richard Lupembe

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nsimbo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi. Naomba nikupongeze kwa kuteuliwa kuwa Mwenyekiti, kiti kimekufaa, hongera sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru Mungu ambaye ametupa uhai na uzima na ametupa kibali sasa hivi tuko ndani ya Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tukiendelea kufanya shughuli mbalimbali za Kiserikali. Naomba nimshukuru na kumpongeza sana Rais wetu, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu kwa kazi kubwa ambayo anaendelea kuifanya katika nchi yetu ya Tanzania. Tunaona jitihada zake, na kazi zake, nasi tunaendelea kumuunga mkono kwa asilimia mia moja ili aweze kufanikiwa kuijenga nchi yetu ya Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpongeze Waziri pamoja na Naibu Waziri. Waziri ni mtani wangu pamoja na mdogo wangu, hongereni kwa kazi kubwa, tunaona jitihada zenu mnazozifanya. Naomba nimpongeze Katibu Mkuu wa Wizara hii, Ndugu Kijazi kwa kazi kubwa. Tunajua anahangaika, ametokea mbali pamoja na kupitia Wizara hii katika sekta mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile naomba nimpongeze Mkurugenzi wa TFS, ni msikivu chief ni msikivu, lakini sasa vijana wake ndio tatizo. Naomba nianze kwa TFS ambayo ni tatizo kupitia wananchi wetu. Tunajua Serikali ni moja, lakini ukienda katika maeneo yetu ya vijijini TFS wamejitenga wao kama wao. Wanafanya kazi wao kama wao, hawathamini kabisa viongozi ndani ya vijiji vyetu. Wakiingia pale vijijini, wenyewe wakishasema hii ni hifadhi, basi wamesema, wanaanza kutandika wananchi; na wakati mwingine inakera zaidi wanapochukua mali zao. Inasikitisha sana maana wakikuta hata ng’ombe wanabeba. Sasa tunajiuliza, hii TFS ni chombo kiko tofauti kabisa, kinajitegemea chenyewe kama chenyewe? Ina maana hakina suluhu na wananchi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru sana Mkurugenzi wa TFS, tumeendelea kumlalamikia kwa ajili ya Meneja wa Kanda, tunamshukuru sana kwani amechukua hatua ya kumhamisha. Tunamshukuru sana kwa sababu ilikuwa ni kero kubwa sana kwa wananchi, alikuwa hataki suluhu na viongozi wa Serikali ndani ya wilaya na ndani ya mkoa, na alikuwa hataki kuonana na sisi Wabunge, anasema sisi ni wanasiasa. Sasa kama ni wanasiasa, ni lazima tuwatetee wananchi wetu kwa sababu mali mazao wanayolima wakulima wale ndiyo inayoleta maendeleo ndani ya nchi yetu pamoja na kukuza uchumi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nitoe ushauri, ifike mahali sasa TSF ipite katika maeneo yote nchi nzima, waonyeshe mipaka yao na wananchi. Unakuta sasa hivi kama Kata yangu ya Ugala, wanasema yote ile ni hifadhi. Sasa unajiuliza, hii ni kata, ina vijiji, ina vitongoji; wanasema wananchi wote wahame kwenye Kata ya Ugala, waende wapi sasa? Wameshakaa zaidi ya miaka 50 mpaka 60, leo mnasema ni hifadhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Kijiji cha Usense Kata ya Urwila, wameweka beacon katikati ya Kijiji, wanasema yote hiyo ni hifadhi. Sasa siku zote hizo mlikuwa hamuoni, leo ndiyo mnakuja kuona kama ni hifadhi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa naomba sana TFS wapite katika maeneo sasa tukubaliane, twende kuanza kuonyeshana mipaka ili tujue mipaka ya TFS iko wapi; na mipaka ya wananchi? Tujue wananchi waende wapi kwa ajili ya maendeleo mbalimbali ya kilimo na ufugaji. Kwa sababu tukienda namna hii tutaendelea kuwavuruga wananchi kwa sababu wanapigwa, wananyang’anywa mali zao, hawana amani, wanaishi maisha magumu sana katika nchi yao na maeneo yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Waziri kipindi hiki atoke, asikae ofisini pamoja na watendaji wake wote, twendeni tukaonyeshane mipaka ili wananchi tujue mipaka yetu iko wapi ili tusiweze kuwaingilia kazi zenu. Kwa hiyo, tunajua mnafanya kazi kubwa ya kuendelea kuhifadhi…

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Engineer Stella Manyanya, karibu.

T A A R I F A

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Taarifa ninayotaka kumpa ni kwamba malalamiko hayo ya kuweka mipaka ya hifadhi yanafanana sana na kule jimboni kwangu Nyasa katika eneo la Lipalamba. Wananchi wanasema mpaka waliokuwa wanaujua, wanauona kabisa, lakini sehemu waliyoenda kuweka kama ndiyo mwisho wa eneo la kwao, wamepitiliza ndani huko kiasi kwamba hata wanavyoelezwa, wao hawaelewi. Wanasema kwa sababu kwanza kwa nini waende kuweka hiyo mipaka peke yao bila kuwashirikisha hao viongozi wa vijiji? Ndiyo taarifa yangu.

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Lupembe, unaipokea hiyo taarifa?

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea. Ni tatizo kusema kweli. Hawataki maelewano kabisa TFS. Mkisema mkae pamoja mkaelezana jambo, hawakubali. Naomba nimuunge mkono kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ndani ya jimbo langu, nina Hifadhi ya Katavi. Hifadhi hii bado haijatangazwa vizuri. Hifadhi ya Katavi ni nzuri, ina wanyama wakubwa, ina mambo mazuri sana, ina twiga mweupe, tembo wakubwa sana, lakini bado hatujaitanga vizuri na hatujajenga mahotel na mazingira yake siyo mazuri sana ya kuvutia watalii kuja katika Hifadhi ya Katavi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba basi Serikali, najua Waziri ana jitihada kubwa sana ya kufanya kazi na uhamasishaji, tunaona leo hii kuna mtu yupo Serengeti. Basi siku nyingine mlete Mbunga ya Katavi ili iweze kutangazika kwa sababu najua ikitangazika, sasa hivi tuna uwanja wa ndege, anatua Mpanda bila matatizo na kutoka pale mpaka kwenye hifadhi yetu, siyo mbali sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Hifadhi ya Katavi ambayo inasimamiwa na TANAPA, ule ujirani mwema bado haujawa mzuri sana. Ndani ya Kata ya Stalike nina mto pale. Ule mto una samaki pale…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Haya, ahsante Mheshimiwa.

MHE. ANNA R. LUPEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niunge mkono hoja. (Makofi)