Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Shally Josepha Raymond

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. SHALLY J. RAYMOND: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii. Kipekee kabisa namshukuru Mungu kutujaalia uzima na ninawashukuru sana wanawake wa Kilimanjaro walionipa hii nafasi ya kuja kuwasemea Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nichukue nafasi hii kwa moyo wa dhati kabisa niipongeze hii Wizara ya Maliasili na Utalii. Kipekee nimpongeze sana Waziri, Mheshimiwa Dkt. Damas Ndumbaro; nimpongeze Naibu Waziri, Mheshimiwa Mary Masanja; Katibu Mkuu, Dkt. Allan Kijazi na pia niwapongeze watendaji wote na vile vile niwashukuru wale wa Kamati iliyowasilisha hoja mezani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimesimama hapa kwa sababu nilitaka tu kusema hii Sekta ya Utalii iko mahututi hospitali. Iko mahututi kwa sababu kwa kweli walipigwa na mambo mengi, lakini zaidi sana na UVIKO 19. Wote waliokuwa na biashara za utalii wanalia, maduka au ofisi zao zimefungwa na hata wale wanyama waliokuwa wanachangamka wakiona magari yanazunguka kule, wamenyong’onyea sana. Naomba Wabunge wote kwa pamoja na wananchi wote tuungane tuhakikishe tunairudisha hii sekta katika hali ambayo italeta faida tena. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sekta ya Utalii inatuingizia nchi hii mapato (GDP) ya asilimia 21, lakini sasa unakuta yameshuka ghafla bila hata ile graph kwenda iki-dwindle, yaani imeshuka chup! Kwa sababu hali siyo nzuri. Hata hivyo ilianza kushuka, kama msemaji aliyenitangulia alivyosema baada pia ya mapato haya kwenda kwenye kapu kuu. Sasa jambo kubwa ambalo linatakiwa tukubali ni kwamba kuna mambo yanayofanyika hata kwenye hesabu, unafanya trial and error halafu kama haitekelezeki, yaani if it doesn’t work mnaamua sasa kusimamia njia moja.

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu uharibifu mkubwa wa barabara za kwenye hifadhi hauwezi kuja kuwapeleka watalii katika hali salama. Mtalii anapotoka kwao anataka hata akija kutembea au hata kama ni mtalii wa ndani, amalize route yake kwa siku. Barabara zile zimeharibika, kwa sababu hakuna namna ambavyo wanapata hela kwa haraka kwenda kuzitengeneza. Hii inakuwa siyo rafiki na haina afya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, barabara za Serengeti zimeharibika, Manyara zimeharibika na hata zile barabara za kupanda mlima Kilimanjaro zimeharibika. Sasa hivi route ile, ule muda uliokuwa unatumika kupanda mlima umeongezeka. Bahati tu ni kwamba mvua imenyesha sana, hawapandi mlima sasa hivi kwa wingi, kwa sababu kila saa ni mvua na ukungu. Kwa hiyo, naomba tu, mvua zikisita, hela ipatikane kutoka Serikali Kuu, barabara zikatengezwe.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia hata kile kibanda cha Mandare ambacho ni maarufu wanapotulia wale watalii wakifika kule juu, kiliungua na mpaka leo hakijakarabatiwa kwa sababu hela haijapatikana kwa urahisi. Hili siyo jambo zuri kabisa. Ukienda Afrika Kusini, ukiwa unataka kwenda Table Mountain, kile kifaa cha kukupeleka Table Mountain kinashughulikiwa kama vile ni jicho, kwa sababu ni utalii unaotangazika. Sasa sisi hata hii ya kupanda tu mlima inashindikana.

Mheshimiwa Naibu Spika, mbaya zaidi mlima Kilimanjaro kunakuwa kuna ile rescue route; kuna wakati ambapo baada ya mvua kunakauka, mtu akiwasha kiberiti au sijui ni watu wale wabaya tu waharibifu wanawasha tu bila kujijua, basi inabidi waende waka-rescue. Barabara zile hazionekani tena na hakuna njia.

Mheshimiwa Naibu Spika, hata vyoo vile vya kwenye route haviko katika hali nzuri. Hivi Watanzania tuko serious kweli! Hii tumeipa Wizara na bado hawana hela na tunasema kwamba hii Wizara inatuingizia mapato. Mimi naleta hiki kilio hapa Bungeni, Waheshimiwa Wabunge, naomba mniunge mkono kila atakayesimama asemee hali ya kurudisha hii Wizara katika hali nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wao walikuwa wanatuingizia mapato ya nje asilimia 25 na hiyo iko katika utalii, lakini pia unakuta kwenye huduma za jamii wanatuingizia asilimia 60. Zimekwenda wapi? Ajira milioni 5.6 ni pamoja na wale porters, nachanganya wote; wale wanaobeba, wale waongozaji, wako huko huko. Sasa hivi nimesema nawasemea wale akina mama kwa sababu vijana wao wako nyumbani na wao, wanangoja mahindi yakomae wachome na mama zao. Vijana walikuwa hawakai ndani, wote wako njiani wanawasindikiza watalii. Naomba sana, hili jambo lifanyiwe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nasema hivyo kwa sababu, ni bahati mbaya sana kwamba sio Wabunge wote wamepata fursa ya kwenda kutembelea Mbuga za Wanyama au Hifadhi. Naomba ikikupendeza, wakati ambapo mnafikiria huko kwenye Kamati ya Uongozi, mtenge fungu kidogo tu, nasi Wabunge tutaongezea wenyewe, tuwe kama group la Wabunge, watalii wa ndani. Wenzetu huko nje wanafanya, kwa nini hapa nje ishindikane? Haina haja tuko hapa tunazungumza jambo ambalo hatulielewi wala hatuzungumzi pamoja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, walitutembelea Kilimanjaro, Wabunge walemavu. Walikuja, walihamasisha, waliwaleta ma-pilot, walikuwa wanaongozwa na Mheshimiwa Riziki Lulida, tulipanda nao mlima. Wale ni walemavu na tukaweza kupanda mlima na leo wanatutangaza huko nje. Leo asubuhi umetuambia Mabalozi wa Utalii wametutembelea wengi, sasa wataenda kutangaza halafu wakifika tutatembeaje? Naomba jambo hilo liangaliwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kuhusu misitu yetu. Nimeona kwamba waliomba kifunguliwe chuo kingine cha misitu, lakini nakumbuka kulikuwa kuna Chuo cha Olmotonyi. Sasa naomba wanapokuja kujibu waseme kile Chuo cha Olmotonyi kiliendaje? Au hakiendi vizuri ndiyo maana kinatakiwa kufunguliwa chuo kingine? Maana iliombwa katika ile report ya Kamati ya Kisekta.

Mheshimiwa Naibu Spika, mchangiaji wa kwanza alileta ugomvi wa mifugo na Mbuga za Wanyama. Nataka niseme hivi, Mungu alipoumba, aliumba kila kitu viwili viwili. Wanadamu waliumbwa wawili, simba wakaumbwa wawili; yaani wanyama, ndege na kila kitu na akasema enendeni mkazaane mwongezeke. Pia akampa mwanadamu utashi akatawale wanyama wote hao. Sasa leo tunawajua ng’ombe wetu walivyo na Tanzania wengi wanafuga ng’ombe wa kuswaga. Yuko Rais wetu mstaafu alisema mnaposwaga ng’ombe, mswagaji anakonda na ng’ombe wanakonda. Hivi kwa nini tusifuge hawa ng’ombe?

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba kama nchi yetu na Serikali za Mitaa zitoe maeneo ambayo yanatosheleza kufuga ng’ombe wakanenepeshwa tukawa ni wafugaji wazuri, tukawa na maziwa mazuri kuliko kuhesabu tu kwa idadi, kuliko kwenda kuingilia wanyama.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. Naomba tuwapatie hizo hela wakarejeshe. (Makofi)