Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Eng. Ezra John Chiwelesa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Biharamulo Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. ENG. EZRA J. CHIWELESA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii nami pia niweze kuchangia kwenye hotuba ya Wizara hii ya Maliasili na Utalii. Kwanza kabisa, nichukue nafasi hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri na Naibu wake kwa kazi kubwa na nzuri ambayo wanaifanya, hasa Mheshimiwa Naibu Waziri ulishanitembelea Biharamulo, nashukuru sana kwa sababu ulifanya ziara pale.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nampongeza Mtendaji Mkuu wa TANAPA ambaye pia ndio Katibu Mkuu wa Wizara hii kwa response kubwa ambayo amekuwa anaifanya pale ambapo nimekuwa nikijaribu kuwasiliana naye juu ya mambo ambayo yanaendelea kwetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haraka kwa sababu ya muda pia; na kwa sababu ndiyo nachangia Wizara hii kwa mara ya kwanza tangu nimeingia humu kama Mbunge wa Biharamulo; na tukiwa na Hifadhi ya Burigi Chato; nachukua nafasi hii pia kutambua juhudi kubwa za Hayati Rais wa Tano, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli ambaye alihakikisha anatutoa katika pori hili la Burigi, pori ambalo limetumika katika utekaji na kuwanyanyasa watu wa Biharamulo kwa muda mrefu sana na hatimaye leo ni sehemu tunayojivunia tuki-anticipate tunaanza kupokea wageni muda siyo mrefu, hasa baada ya haya ambayo tunayatarajia kwenye bajeti hii yatakapokuwa yamefanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninayo mambo kama matatu ya haraka haraka ya kwenda nayo kwa sababu ya muda. Jambo la kwanza, hifadhi hii imekuwa na kelele kidogo hasa kwa wakazi wa Biharamulo. Nadhani suala hili nimeshalifikisha kwa Waziri, lakini kikubwa ambacho kimekuwepo ni jina la hifadhi. Maana kwetu sisi wakati hii hifadhi inaundwa, imechukua sehemu ya Chato na sehemu ya Biharamulo ukiunganisha wilaya mbili kama hifadhi moja. Kwa upande wa Biharamulo kwa sababu pori lilikuwa linaitwa Burigi, wakazi wa Biharamulo walipoona sasa pori linaundwa hifadhi, linabaki jina Burigi na huku linabaki jina Chato, wakahisi kama vile sasa ni kwamba pori limesomeka chini ya Chato. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hali hii imeleta kelele na Mheshimiwa Waziri nilimwambia, wakati wa kampeni ilikuwa ni saga kubwa sana. Hata leo nilikuwa na kipindi Star TV asubuhi. Siongelei hili suala kabisa, ni suala lingine, lakini miongoni mwa mada zilizokuja ilikuwa ni mada ya jina.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba kwa sababu mbuga hii inaunganisha wilaya mbili; tuna Wilaya ya Biharamulo na Wilaya ya Chato, nilikuwa naomba pale penye neno “Burigi” mridhie kubadilisha neno “Burigi” likae jina “Biharamulo.” Mbuga isomeke “Biharamulo Chato National Park” ili wakazi wa Biharamulo ambao wanabeba sehemu kubwa ya hili pori waone kwamba juhudi kubwa ya kuwatoa katika mateso na unyang’anyi wa watekaji wale, inaleta faida kwao.

Mheshimiwa Naibu Spika, hilo nilikuwa naliomba Mheshimiwa Waziri alichukue kwa niaba ya wakazi wa Biharamulo, wakubali ku-amend jina, kwa sababu kinachoonekana Tourist Board wakati wanaanzisha hiki kitu ni kwamba hawakutoa elimu ya kutosha kwa ajili ya wakati wa Biharamulo. Nasema hawakutoa elimu kwa sababu hata geti tu la kuingilia mbugani, uwanja mkubwa ambao tuna- anticipate kuutumia utakuwa ni uwanja wa Chato; kutoka Chato mpaka Biharamulo kama watalii wametua pale ni takribani kilometa 50. Unapofika Biharamulo huingii mjini, kwa sababu Mji wa Biharamulo barabara kubwa inatoka inaeleke Nyakahura na hatimaye inaelekea Rwanda na Burundi. Sasa mjini hutaingia kama unakwenda mbugani kule; na geti linalofuata liko kilometa 82 kutoka Biharamulo Mjini upande wa Nyakahura kule karibu unaelekea Rwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa unafikiria, mgeni yupi ambaye utamtoa Chato Airport, kilometa 50 umtembeze, afike aone Mji wa Biharamulo kulia, unamkatisha mbuga kilometa 82 yule mgeni ndio anakwenda kuingia kwenye hifadhi kupitia Geti la Nyungwe, halafu tena aanze kutembea kurudi nyuma ya Biharamulo. Kwasababu Basically, hata Naibu Waziri alipokuja Biaharamulo tulimweleza, Central Burigi lilipo, lile Ziwa Burigi ambalo linaunganisha Karagwe na Mulega, lipo nyuma ya Biharamulo pale; ni takriban kilometa 10 tu, ukipitia kati ya Ruziba, Kijiji cha Kitochembogo na Kitongoji cha Muungano, unatokea kwenye hifadhi, katikati kabisa kwenye ziwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa tulikuwa tunaomba, najua mtaongeza mageti, nilishaambiwa kuwa kuna haja ya kuongeza geti na niliomba geti liongezwe. Sasa ninachoomba, geti litakaloongezwa this time litokee pale pale Biharamulo ili wageni hawa sasa wasizunguke umbali mrefu. Maana mgeni anapokwenda sehemu anataka aone Wanyama. Sasa ukianza kumtembeza kule na bado miundombinu haipo, itakuwa haisaidii. Kwetu sisi kwa wakazi wa Biharamulo tunataka mbuga hii tuituimie kutangaza utalii na vile vile ku-brand wilaya yetu, maana imekuwa ni nyuma sana. Hii wilaya imekuwepo tangu mkoloni, lakini haijulikani.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, tulikuwa tunaomba fursa hii na geographical location ambayo Mwenyezi Mungu ametupatia pale iweze kutunufaisha. Mheshimiwa Waziri nikienda haraka haraka, nimeona hapa mnao mpango wa kujenga hoteli pia. Sasa nilikuwa naiomba Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii watusaidie kwenye plan ya kujenga hoteli hata sisi tupate angalau hoteli moja pale. Tukipata hoteli moja itatusaidia. Pia nimeona kwenye bajeti mna mpango wa kujenga barabara kilometa 2,256 pia sehemu ambayo mna madaraja takribani 18 na culvert 157.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nilikuwa naomba kwa sababu mbuga hii haina miundombinu kabisa kabisa. Tunaomba mtusaidie, wakazi wa Biharamulo watakapojua kwamba kilometa ngapi zimetengwa kwa ajili ya hii ya kwetu Burigi, Chato itatusaidia sasa hata sisi kujipanga ku-grab hizo opportunities. Maana najua kama ni ujenzi wa barabara hamtafanya nyie, nami nahitaji watu wangu kwa sababu mbuga ipo kwao, watumike na washiriki kwenye kujenga barabara na kuchukua opportunities za kufanya kazi hizo ili waweze kujinufaisha kimapato. Kwa sababu basically tunachokiangalia ni kwamba hii mbuga iwanufaishe wao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba haya yazingaiwe kwa haraka kwa sababu ya muda. Ili haya yote yaweze kufanyika, lipo jambo moja. Tumekuwa tunaona kwamba mapato yote yanayokusanywa na TANAPA siku hizi yanakwenda TRA. Sasa hawa watu mvua inaponyesha na kwenye hifadhi hizi, maana tunazo taarifa kwamba mbuga zetu za Tanzania barabara zimeharibika kweli kweli, hata huduma zipo chini sana. Kwa sababu wanapoomba fedha ya miradi ya maendeleo kutoka Hazina mpaka irudi inachukua muda mrefu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa hizi mbuga basically lazima zijiendeshe kibiashara, kwa sababu zinajiendesha kibiashara na tuna-competition na jirani zetu wa Kenya au watu wengine wanaotuzunguka, tunaomba kosa moja la mtendaji mmoja au watendaji wawili la kuharibu au kutapanya zile fedha isiwe adhabu ya kuharibu biashara ya utalii. Tunaomba Serikali ifikirie ku-amend hii sheria, fedha irudi TANAPA, waikusanye, muweke usimamizi maalum, ili sasa watakapohitaji fedha ya kutengeneza barabara kule, tusianze wote kuomba kwenye kapu moja, kwa sababu hii ni sehemu ya biashara. Tunaporudi kuomba kwenye kapu moja, inakuja kutuchelewesha na inashindwa kufanya maendeleo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)