Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Aida Joseph Khenani

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Nkasi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. AIDA J. KHENANI: Mheshimiwa Naibu Spika, nami nakushukuru kwa kunipatia nafasi. Kabla ya yote naomba kutoa pole kwa Jimbo langu la Nkasi Kaskazini na kwa wazazi wa binti huyu kwa kuwa ni mpiga kura wangu, Petronela Mwanisawa aliyenyongwa na mpenzi wake. Kwa mazingira ya kawaida miongoni mwa mikoa ambayo bado tulikuwa nyuma sana kielimu ni pamoja na Mkoa wa Rukwa. Inapotokea hasa tena kwa mtoto wa kike mwenye umri wa miaka 22, kwa mazingira ya wazazi kama wale wa Mkoa wa Rukwa, inatia uchungu sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua umekuwa mtetezi sana wa wanawake na umetoa mwongozo wako vizuri, lakini ni vizuri Serikali ikaliangalia jambo hili. Leo tunapoona adui wa kwanza sasa wa kumaliza maisha ya wanawake ni pamoja na mahusiano ya kimapenzi, iwe kwenye ndoa au mahusiano ya kawaida. Ni vizuri jambo hili likaangaliwa vizuri. (Makofi)

Mheshimwia Naibu Spika, nami napenda kuchangia Wizara hii na kabla sijachangia niwapongeze sana Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri pamoja na cabinet yake. Nawapongeza zaidi kwa sababu Waziri na Naibu wake wamekuwa wasikivu na kuchukua hatua pale ambapo matatizo yanajitokeza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wilaya yangu ya Nkasi ni miongoni mwa wilaya ambazo zina migogoro ya kutosha juu ya wananchi na Hifadhi au Mapori Tengefu. Nitaanza na suala la mipaka katika Hifadhi kwa Mapori Tengefu. Nilizungumza ndani ya Bunge na Waziri Mkuu akatoa maelekezo kupitia Waziri wa Maliasili na Utalii kulingana na uzito wenyewe, lakini hapa nazungumza kulingana na mgogoro huo, imefikia mahali sasa wananchi walifikia hatua mpaka kumuua Game, jambo ambalo siyo zuri. Leo limefanyika Nkasi, litaendelea maeneo mengine. Lazima mfanye uchunguzi wa kutosha, nini kinapelekea migogoro hii kuendelea? (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye Wilaya yangu ya Nkasi nitataja kata chache tu ambazo zina migogoro. Kata ya Kabwe, Kata ya Kilando, Kata ya Kipili, Kata ya Kipundu na Kata ya Nkomoro. Nilifanya utafiti wa kutosha baada ya hii migogoro kuona inaendelea sana. Ukienda Kata ya Kirando, Kata ya Kipili, Kata ya Kabwe, mpaka wa kwanza kabisa uliwekwa mwaka 1948. Ukiangalia huo mwaka, idadi ya wakazi ilikuwa ni ya watu wachache sana. Huo mpaka ukabadilishwa mwaka 1992, ukabadilishwa tena mwaka 2002. Sasa ulivyobadilishwa mwaka 2002 ukarudishwa tena, kule kwenye ule mpaka uliowekwa mara ya kwanza mwaka 1948. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, unaweza ukaona hapo idadi ya watu imeongezeka kiasi gani kutoka mwaka 1948 mpaka leo mwaka 2021. Pamoja na kwamba mawazo ya Wabunge wengi tumekuwa tunaomba tuongezewe ardhi kutoka kwenye Mapori Tengefu au kwenye Hifadhi, jambo hilo halitakuwa suluhisho la kudumu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kushauri Wizara, kwa sababu, idadi ya watu inaongezeka, kuna haja kubwa sasa Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Ardhi, Wizara inayohusika na mazingira, TAMISEMI, Uvuvi, pamoja na hizo Wizara ambazo Mheshimiwa Rais aliona kuna umuhimu wa wao kukaa pamoja, kuna haja ya kwenda kupitia mipaka hii upya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitazama leo maumivu waliyonayo wananchi wetu, wanaona ni kama Serikali ya Tanzania inaheshimu zaidi wanyama kuliko binadamu. Lazima tuwaondoe kwenye hiyo dhana. Tunaiondoaje? Matamko na makatazo bila mbadala, haina maana yoyote, inaleta unyanyasaji kwa wananchi wetu. Leo mkiwaambia wananchi hawa wako kwenye Hifadhi, Serikali ni moja, mnajua kwamba idadi ya watu inaongezeka. Hiyo mipaka ya mwaka 1948 kwa hali ya kawaida, kulingana na idadi ya watu inavyoongezeka, lazima migogoro itakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, lazima Serikali ije na mbadala. Ukisema hii ni Hifadhi, lazima tuungane kwa pamoja tutenge eneo lingine. Kwa sababu, wengi wanaoathirika na hii mipaka ni wakulima, ni wafugaji na wavuvi. Lazima tutafute eneo mbadala na hapo tutakuwa tumekwenda kuondoa tatizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye hilo jambo ni vizuri nikaliweka sawa. Adhabu zinazotolewa na watu wa TAWA, TANAPA na wengine wote, ni adhabu ambazo ni za ajabu sana. Wananchi wananyanyaswa. Mambo yaliyokuwa yanafanyika na Wakoloni, yanafanyika kwa watu wa TAWA. Jambo hili halikubaliki. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi nimekwenda walipokuwa wanaadhibiwa watu wa mpaka ule wa Korongwe, nilimwambia Mheshimiwa Waziri, mzee anapigwa, amekutwa nyumbani. Pia kuna mama amejifungua, ana siku mbili, nyumba yake inachomwa. Anaenda wapi na huyo mtoto? Yaani imefikia mahali haki za binadamu hazipo tena. Haya mambo hayakubaliki, hayakubaliki kabisa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye jambo hilo, inapotokea mwananchi ameliwa na mamba, ameliwa na kiboko, mnachelewa sana ku-react ninyi Wizara ya Maliasili, lakini ikitokea mwananchi amekamatwa na aidha, nyama nyamapori kidogo, adhabu anayopewa ni wakati huo huo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ikitokea pia mfugaji amekamatwa kwenye Hifadhi, adhabu wanazopewa zinaanzia siku hiyo hiyo. Hapa nina risiti kadhaa za wafugaji ambao wamepewa adhabu. Ukifuatilia ule mgogoro pia kuna watu wenu ambao ni watendaji ambao sio waaminifu, wanachukua ng’ombe zilizokuwa nje huko wanazipeleka ndani kwenye Hifadhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, haya mambo, unajiuliza, kama wakazi wanaweza wakajenga nyumba, wakajenga shule, wana mashine pale za kusaga, hawa watu wa hifadhi walikuwepo. Wanakwenda kuchoma watu wamekaa zaidi ya miaka 10, miaka 20 Serikali ilikuwepo. Kwa nini mnashindwa kufanya hayo mambo mapema? Inatuonyesha kwamba kuna mambo yanayofanyika juu ya hao watendaji wachache, ambao wanawaingiza wafugaji pale kwa mkataba na siku hiyo wasipowapa fedha, wanakwenda kufanya maamuzi kama hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna sehemu rushwa zipo, ni pamoja na eneo hili, ni lazima liangaliwe vizuri. Nakumbuka kauli ya Mheshimiwa Rais akiwa ndani ya Bunge kwenye hotuba yake ya mwisho, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan, juu ya maliasili zinazopatikana ndani ya Hifadhi. Lile jambo alilolitamka ni vizuri sana, lakini kuna haja ya kufanya utafiti wa kutosha kwenye maamuzi haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukitazama hata wale wananchi ambao wanaibua labda madini, namna wanavyochukuliwa na wale watu wa TAWA, TFS, adhabu wanazopewa; kitendo cha kusema hapa nimegundua kuna madini; pamoja na kwamba ni nia njema ya Serikali leo kuruhusu madini na vitu vilivyoko kwenye Hifadhi kuvunwa, ni lazima tuwe na utaratibu mzuri utakaotumika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, kugundua, pia watu ambao ni wa eneo lile waweze kuwa wanufaika wa kwanza ili tuweze kuleta uthamani. Kwa sababu mimi naamini wahifadhi namba moja ni wale watu ambao wako karibu na Hifadhi. Jambo hilo likitumika kwa busara hiyo naamini kila mtu anapenda uhifadhi. Sasa tunahifadhi kwa ajili ya nani? Tunahifadhi kwa ajili ya wananchi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana, Mungu akubariki. (Makofi)