Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Dr. Medard Matogolo Kalemani

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chato

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, kwanza nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ya kuja kuhitimisha hoja. Nianze kukupongeza wewe mwenyewe kwa jinsi ambavyo umeongoza mjadala kwa upeo wa hali ya juu sana, ahsate sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumepata wachangiaji takribani 82 waliochangia kwa maandishi na wengine kwa kuzungumza na wengine kwa namna mbalimbali. Tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwanza niwahahakishie kwamba michango yenu yote mliyoitoa kwetu, ushauri na mapendekezo na maoni yenu sisi tunachukulia kama maelekezo ya kwenda kufanyia kazi. Tunawashukuru sana kwa michango yenu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nianze na kuchangia katika maeneo takribani 12, kwa ujumla jumla na machache sana nitagusia kwa kipekee. Nianze kuzungumzia Mpango wa Serikali wa kufikisha megawatt 5000. Tumeeleza kwenye kitabu chetu cha Mpango na Bajeti ya mwaka huu. Tunatekeleza miradi mikubwa mingi lakini mradi ambao kwa kweli Watanzania tungependa wote kujivunia ni Mradi wa Julius Nyerere, tunakwenda vizuri. Tumeeleza kwenye kitabu kwamba tumefikia asilimia 52 lakini ukienda kule site unaweza ukadhani tumefikia asilimia 80 na kitu, kazi inakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwahakikishie Watanzania na Waheshimiwa Wabunge kupitia Bunge hili Tukufu mradi huo unakwenda kukamilika ndani ya wakati. Nilizungumza siyo siku nyingi zilizopita kwamba hivi karibuni Novemba mwaka huu tunaanza kujaza maji bwawa. Ni kweli kuja kufika tarehe 15 Novemba 2021, tunaanza kulijaza maji bwawa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sisi siku hiyo wachache wetu itakuwa ni siku ya sherehe. Kwenye mabwawa kama hayo huwa kuna hatua kubwa mbili; ya kwanza, siku ya kujaza bwawa na ya pili ya kuchaji umeme unapokwenda kutumika kwa wananchi.

Niwaondoe wasiwasi ndugu zangu wananchi na Waheshimiwa Wabunge tutalijaza mpaka kufikia tarehe 25 Aprili, 2022 bwawa letu litakuwa limeshajaa maji ya kuanza kuzalisha umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama nilivyowahi kusema kuja kufika tarehe 14 Juni 2022 tunaunganisha kwenye Gridi ya Taifa, tunawasha transformer na wananchi wanaanza kupata umeme. Ni jambo ambalo nimeona niliweke wazi leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sina sababu ya kurudia manufaa ya miradi kama hii, lakini jambo la msingi ambalo Waheshimiwa Wabunge mmechangia ni kuwepo umeme mchanganyiko. Ni kweli tumejipanga vizuri sana kusema ukweli kuanza kutekeleza miradi ya kila aina kuhakikisha tunapata megawatt 5,000. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na mradi huu mkubwa wa Julius Nyerere, lakini tuna mipango ya miradi mingine ya gesi asilia ambapo mwakani kuanzia mwezi Septemba tunaanza kutekeleza mradi wa megawatt 300 kule Mtwara ambao utaunganishwa kwenye Gridi ya Taifa baada ya miezi 18. Kwa kueleza michache tu ni kwamba tumejipanga vizuri na Waheshimiwa Wabunge mnatusaidia kupitisha bajeti leo, sisi kazi yetu kubwa ni kwenda kuhakikisha tunapata megawatt 5,000 ndani ya muda mfupi kufika mwaka 2025. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi LNG ni muhimu sana na ni wa kimkakati. Ni lazima tukiri kwamba tumepoteza muda mrefu kidogo, lakini lengo ilikuwa ni kujipanga vizuri ili tusiliwe na wawekezaji. Mnafahamu vizuri sana ni kupitia Bunge hili mlishauri kwamba mikataba yote ya rasilimali ya gesi ichambuliwe na kupitiwa vizuri ili iwe na tija na manufaa kwa Watanzania. Naishukuru sana Serikali imeitika wito, imechambua mikataba yote sasa kazi imekamilika na tunaanza majadiliano. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda nitoe taarifa mbele yenu Waheshimiwa Wabunge tumeanza majadiliano toka mwezi uliopita na majadiliano yatachukua takribani miezi sita kutoka wakati huo na baada ya hapo utaratibu wa utekelezaji unaendelea. Kwa hiyo, niwape matumaini wananchi wote wa Kusini na Watanzania kwa ujumla mradi wa LNG unaanza sasa kutekelezwa tena kwa speed kubwa. Kwa hiyo, niwaondoe wasiwasi ndugu zangu wananchi katika jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la msingi hapa kuna suala la mgawanyo na matumizi ya gesi. Ni kweli tumegundua gesi nyingi sana takribani futi za ujazo trilioni 57.54 lakini kiwango tunachokitumia kwa sasa pamoja na kutumia kwa kiwango kikubwa katika kuzalisha umeme takribani asilimia 67 ya umeme tunaotumia, pamoja na kupeleka majumbani zaidi ya wananchi 1,000, magari 700 na viwanda 58 na kadhalika bado tumetumia chini ya asilimia moja kwa maana ya trilioni tulizonazo, ni 0.57 tu ya gesi tuliyoitumia, kwa hiyo, bado tuna gesi nyingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpango wetu ni nini? Kwanza, ni kuhakikisha kwamba mradi huu wa LNG ambao utatumia takribani tani milioni 10 kila mwaka, kwa matumizi ya gesi kwenye kiwanda hiki gesi itatumika kwa kiasi kikubwa sana. Hadi kumaliza mpango wa utekelezaji wa mradi huu, tutakuwa tumetumia trilioni 3.9 kwenye rasilimali ya gesi. Hicho ni chanzo cha kwanza kuanza kuitumia gesi kwa kiwango kikubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tunaendelea kuzalisha umeme wa gesi, megawati 300 Mtwara, megawati 330 Somangafungu na Kinyerezi I na Kinyerezi II tumetumia gesi, tunakwenda kuanza tena Kinyerezi III megawati 600 tutatumia rasilimali ya gesi. Matumizi yetu yatapanda, kwa sasa tunatumia takribani futi za ujazo milioni 200 kwa siku lakini matarajio yetu zitapanda maradufu katika miaka miwili ijayo. Kwa hiyo, niwaondoe wasiwasi wananchi kuhusu utumiaji wa rasilimali ya gesi.

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la msingi tuna miradi mikubwa ya gesi, mradi wa kwanza tuna bomba la Uganda. Tunataka tutumie Mkuza huu wa bomba la kutoa mafuta Hoima kuja Tanga na sisi tutumie sehemu hiyo hiyo kupitisha gesi yetu kuwauzia majirani zetu Uganda. Vilevile, tunatarajia kujenga bomba lingine la kutoka Dar es Salaam kuelekea Tanga hadi Mombasa litakalotumika kupeleka gesi pia maeneo ya Mombasa nchini Kenya. Kwa hiyo, bado rasilimali yetu itatumika sana katika maeneo yote. Nimeona hili nilifafanue kwamba rasilimali ya gesi haitakaa idle itaendelea kutumika kwa ajili ya manufaa ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ni muhimu sana Watanzania kulielewa, katika mafanikio ambayo Awamu ya Tano na Awamu ya Sita imepata ni huu mradi wa treni ya mwendokasi ya kisasa ya kutumia umeme. Haya ni mafanikio makubwa sana. Nilieleza kwenye bajeti yetu kwamba hadi sasa tumeshajenga kilometa 160 kwa asilimia 100 hata ukitaka ulete leo treni ya mwendokasi ya kisasa ya kutumia umeme kama tunataka iishie Morogoro, inaweza ikaanza kukimbia hata wiki ijayo na ikafika mpaka Morogoro kwa sababu tumeshajenga na tumekamilisha kwa asilimia 100. Haya ni mafanikio makubwa sana, naipongeza sana Serikali yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mradi wa EACOP wa kusafirisha mafuta kutoka Hoima. Huu ni mradi wenye manufaa makubwa sana. Tumeeleza hivi karibuni takribani mikoa nane, wilaya 24, kata 134, vijiji 257 na vitongoji 527 vinapitiwa na mradi huu. Maana yake nini? Maeneo yote niliyoyataja yanakwenda kukua kiuchumi. Kwa hiyo, hii ni fursa kubwa sana kwa wananchi wetu kuchangamkia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitumie nafasi hii kuwaambia wananchi wote wanaopitiwa na miradi hii, waanze kujiandaa kuchukua fursa hizi ambazo kwa asilimia 80 ziko kwa Watanzania. Zaidi ya asilimia 80 ya mradi huu uko Tanzania maana yake ni kwamba sisi ndiyo wenye fursa ya kupata manufaa makubwa kutokana na mradi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nilieleza vituo vingapi vitajengwa, kwa haraka haraka tutajenga takribani vituo nane kwa ajili ya kusukuma mafuta lakini vituo 6 kati ya 8 vyote viko Tanzania na vitakuwa na makambi ya wafanyakazi. Tutakuwa na maeneo ya kufunga valve kwenye vituo 79 lakini maeneo 53 yako Tanzania, hizo ni fursa. Tutakuwa na maeneo ambako tutachemsha mafuta hayo kwa sababu ni ya kuchemsha, kati ya vituo 29 vituo 22 viko Tanzania, hizo ni fursa kwetu. Kwa hiyo, nitoe wito kwa Watanzania kutumia fursa hizi ili kuleta manufaa kwao. Mradi umeshaanza kutekelezwa, ni matumaini yetu ndani ya miaka mitatu mradi utakamilika na manufaa tutayaona zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kubwa zaidi katika Mkoa wetu wa Tanga hasa kule Chongeleani, bandari ya Tanga inakwenda kupanuka sana kwa sababu hapo ndiyo mafuta yatakapokwenda kusimama na kutakuwa na uwekezaji mkubwa zaidi ambapo uwekezaji wa nje tunatarajia kwa Serikali yetu kunufaika kwa asilimia takribani 55. Haya ni manufaa makubwa ambayo Watanzania ni vyema kujivunia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mradi wa REA. Pamoja na maelezo ya Mheshimiwa Naibu Waziri, napenda niwahakikishie Watanzania na Waheshimiwa Wabunge mradi huu wa REA III round II, tunakwenda kumaliza vijiji vyote na huu siyo utani, hii ni dhamira ya Serikali. Tumedhamiria ni lazima tumalize. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwapongeze sana Waheshimiwa Wabunge katika hili kwani wametupa ushirikiano wa kutosha katika kila hatua. Niwaombe, kama kuna Kijiji katika eneo lako kimesahaulika, ama kimerukwa kwa namna yoyote ile tukiwa hapa Bungeni tuletee kabla hatujaondoka ili twende tukakijumlishe na kifanyiwe kazi. Suala la umeme kwa sasa ndugu zangu sio la hiari ni jambo la lazima. Ni lazima tuelewane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ameeleza Naibu Waziri, tumejipanga vizuri leo tuko wa kwanza Barani Afrika kupeleka umeme vijijini lakini tunataka tusiishie hapo tuwe wa kwanza kupeleka umeme bora na wa uhakika, ndio lengo letu la msingi. Vijiji vilivyobaki tumepeleka wakandarasi, tumebakiza wakandarasi watano ni matumaini yetu kwamba wiki ijayo nao wanaweza kupatikana ili mikoa na maeneo yote wakandarasi wawe wameshafika site. Nitumie nafasi hii kutoa wito kwa wakandarasi, mkandarasi yeyote atakayelegalega hata kabla hajachelewesha mradi tukimbaini njiani, tunamuacha, tunamtelekeza, tunachukua mkandarasi mwingine, hiyo hatua tunayokwenda kuchukua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeeleza Watanzania Mradi wa Umeme Vijijini haubagui nyumba na hili nisisitize kwa watani wangu wa Dodoma. Zile nyumba zetu za tembe zote ni umeme, hatuchagui nyumba. Najua mmeshatoka huko lakini tunataka Watanzania wote waone hii ni fursa. Nazungumza huu si utani, leo nenda Kongwa kwa Mheshimiwa Spika, Bahi, Singida angalieni barabarani, nyumba za aina hiyo tunataka zikue zifanane na magorofa, wananchi wa-enjoy maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, katika mradi huu tumejipanga vizuri. Katika maeneo ambayo vitongoji vimebaki, tuna mradi wa vitongoji almaarufu densification. Huu mradi ni muhimu sana, tumetenga shilingi bilioni 366 kwa ajili ya kupeleka umeme kwenye vitongoji vyote, hiyo ndiyo dhamira ya Serikali. Pia tuna maeneo ambayo kimsingi sio vijiji yanaitwa mitaa lakini ukiyatazama kwa hali halisi na wala si mitaa kwenye macho ya Watanzania. Hasa maeneo katika Majiji, Manispaa, Halmashauri za Miji yako mengi, tumeanza kushughulika nao. Kwa sasa tumebaini maeneo 637, maeneo ya Dar es Salaam, yakiwemo ya huko Chanika, Bombambili, Dondwe, Msongole, Zingiziwa hayo yote tunawapelekea umeme. Hata kule kwa Naibu Spika kule Tonya, Ituhi, Nzoho, tunapeleka umeme kwa bei hiihii. Hata kwako Mheshimiwa Spika ulisema pale Mbande Kati na Mbande Kisimani tunapeleka kwa bei hii hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwahakikishie wananchi wa Majiji ya Mwanza, iwe Nyamanoro, Nyamadoke, Kishiri, Kabaha, Kalemela yote tunapeleka umeme kwa bei hiihii. Arusha, iwe Murieti, Olasiti, Moshono, Terati, bei ni hizi hizi. Dodoma, iwe Ntyuka, Nala, Vikonje tunapeleka kwa bei hiihii. Tumetenga shilingi bilioni 160 kwa ajili ya kupeleka umeme katika maeneo haya ambayo yanatuchanganya ni vijiji ama ni mitaa. Sisi kwenye macho ya Serikali tumedhamiria yote yawe shilingi 27,000. Kwa hiyo, Watanzania wote watapata umeme bila kuchelewa. Kazi hii si ndogo lakini Serikali tumejipanga, Wabunge mmejipanga najua leo mnatupitishia bajeti, mkishamaliza kupitisha bajeti sisi mtatuona vijijini hatutakaa ofisini, lengo tupeleke umeme kwenu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nikandamizie mbele ya Bunge lako Tukufu, umeme iwe kijijini anapeleka REA au mjini anapeleka TANESCO bei ni shilingi 27,000. Naomba nirudie, bei ya kupeleka umeme ukiondoa City pale Ilala Dar es Salaam ambapo hata kwa sasa hawahitaji wana umeme, maeneo yote nchini ni shilingi 27,000. (Makofi)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan, Oyeee. (Makofi)

WABUNGE FULANI: Oyeee. (Makofi)

WAZIRI WA NISHATI: Mheshimiwa Spika, naomba niwaelekeze TANESCO, atakayesuasua kutekeleza agizo hili, hajitaki na atakuwa hana kazi. Hayo ndiyo maelekezo ya Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la kuuziwa nguzo, naomba nirudie, Serikali imegharamia nguzo kwa asilimia 100 na nguzo zipo. Mahitaji yetu ya nguzo kwa mwaka ni nguzo milioni 2.8, nguzo tulizonazo ni milioni 4.9, kwa hiyo, nguzo zipo. Naomba nisisitize kwa mara nyingine wakandarasi, Mameneja wa TANESCO, wala msijiingize kwenye mtego wa kusema mwananchi anunue nguzo tutakushughulikia mapema usiku na mchana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, jipangeni, haiwezekani Watanzania wote waishi ndani ya mita 30 kutoka kwenye nguzo. Niwaombe sana TANESCO na wakandarasi mjipange katika hilo, lazima muwe wabunifu, mfanye kazi kwa kasi na uweledi wenye uaminifu. Sihitaji kurudia katika hilo, nadhani watendaji wetu wameelewa na hili linatekelezeka wala hatuna mashaka nalo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kuna suala la kucheleweshwa wananchi kuunganishiwa umeme. Ameeleza Mheshimiwa Naibu Waziri yako maeneo kuna sababu lakini pamoja na sababu nzuri tulizozitoa, tumeanza kuchukua hatua na tunawapima Mameneja wetu kwa vigezo viwili, ili apande cheo ni vigezo viwili vikubwa. La kwanza, kuunganishia umeme wateja kwa kasi, hilo ndilo lengo tunalowapimia. La pili, anavyohudumia wateja, hivyo ni vigezo vikubwa sana tunavyovizingatia. TANESCO inafanya biashara, kazi yake kubwa ni kuwajali wateja wetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nimeshaeleza na nimetoa miezi miwili kwa TANESCO Mameneja wote ambao wanadaiwa na wananchi wameshalipa pesa yao, hajawaunganishia umeme wakamilishe kufanya zoezi hilo ndani ya miezi miwili vinginevyo tutachukua hatua kwa Mameneja wanaohusika. Tumeanza kuchukua hatua, sio lengo letu kuwaonea, lakini tunataka wafanye kazi kwa umakini, kwa kasi na kwa kweli kwa ubunifu mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la msingi ambalo napenda kuzungumzia ni kuhusu kukatikakatika kwa umeme. Tumeeleza kwa kiasi kidogo, naomba nirudie tu kidogo. Yako kweli mazingira, nchi yetu ndugu zangu ni kubwa, unauzungumzia waya unatoka Mtwara mpaka Kagera, unatoka Mtwara katika Mtaa wa Mkunjanguo unakwenda mpaka Kyaka, mazingira haya ni marefu, yako maeneo kwa kweli hali halisi inatokea waya ukakatika, hilo nalo lipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, lazima tukubali bado tunatumia nguzo za miti kwa kiasi kikubwa, baada ya miaka miwili zinaoza, si kwamba hazina ubora ndiyo nature ya miti yetu haiwezi kukaa miaka mingi, hiyo changamoto nyingine. Sababu nyingine ni matumizi yetu sisi wananchi, mtu anaweza akagonga nguzo, akachoma moto na kadhalika. Hata hivyo, tumeweka bajeti tumeeleza hapa, mwaka huu tumetenga bajeti ya ndani ya TANESCO shilingi bilioni 85.8 kurekebisha dosari hizo ndogo ndogo ili umeme uwe imara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la msingi kabisa tumeeleza, baadhi ya maeneo kwa kweli njia ni ndefu, umeme unafika ukiwa kidogo. Tumetenga fedha nyingi sana mwaka huu zaidi ya shilingi bilioni 150 kwa ajili ya kujenga vituo vya kufua umeme katika maeneo hayo ili kuimarisha upatikanaji wa umeme. Tumefanya hivi Handeni, Kilindi, Simiyu, Ipole, Nguruka, Urambo na maeneo mengine tunaenda kufanya hivyo. Leo tumeanza kutekeleza mpango wa kujenga substation Mkuranga ili Mbagala ijitegemee na Mkuranga ipate umeme wake, lengo ni kuboresha njia hizo za umeme. Hatukusudii kuendelea kuwa na umeme unaokatika, tumejipanga vizuri na Wabunge mnatuunga mkono, ni matumaini yetu hili jambo tumelipa muda mfupi mbele ya safari tutakwenda vizuri. Tukikamilisha Mradi wa Julius Nyerere nataka niwaambie Watanzania hii nchi inakwenda kuwa Ulaya ya Afrika, hizi ni dosari za wakati huu tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na suala la kukatika kwa umeme Serikali inakwenda kupitia upya bei za ankara za umeme kwa Tanzania. Tunakwenda kuangalia bei kulingana na uzalishaji. Tulisema uzalishaji wa mradi huu unachukua mpaka unit 1 Sh.36 ukilinganisha na vyanzo vingine. Sitaki kutaja kila chanzo, lakini ndio chanzo cha gharama ya chini kabisa unapozalisha umeme, kwa hiyo, Serikali tutafikiria pia kufanya mapitio ya bei za ankara kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bei za visiwani, wazalishaji wadogo maeneo mengine wanaitwa Wananzengo wanawauzia wananchi umeme kwa bei kubwa Sh.3,500 wakati unit 1 kwa bei elekezi ya Serikali ni Sh.100 kwa Watanzania wa kawaida. Tulitoa maelekezo mwaka juzi, tumetoa maelekezo mara nne na leo narudia mara ya tano. Niwaombe na kuwaagiza wazalishaji wote wadogo wadogo, bei elekezi ya Serikali ya kuuza umeme kwa Watanzania ni Sh.100 kwa unit na si vinginevyo. Kwa hiyo, wazalishaji walioko visiwani, Mheshimiwa ameeleza hata kule Ukerewe kuna wazalishaji wa namna hiyo, wako Buchosa kule Maisome wanafanya hivyo, wako Nyantakara Biharamulo, wako Mafia, wako Njombe na Makete na maeneo mengine, tulishawapa muda warekebishe dosari. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nielekeze viongozi wenzetu wanaosimamia usalama wa wananchi kule, Wakuu wa Wilaya na Wakuu wa Mikoa watusaidie, tulishatoa maelekezo na hata kwenye kanuni na mikataba yao hiyo bei haimo wanafanya hivyo kurejesha faida. Hatuwezi tukakubali arejeshe faida kwa maumivu ya Watanzania, bei inaeleweka.

Kwa hiyo, ni marufuku wazalishaji wengine wowote wale, kuzalisha umeme sio shida, wahudumieni wananchi wetu lakini bei ya umeme lazima iwe linganifu shilingi 100 kwa unit na si vinginevyo. Hili narudia leo tusilisikie tena tutachukua hatua kali dhidi ya wazalishaji hao wadogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusiana na gridi Kigoma, Katavi na maeneo mengine. Kwanza niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wote wa Kigoma na Katavi mnajitahidi sana kutupa ushirikiano. Nataka niwahakikishie kwa Kigoma peke yake, kuna njia nne zote zinashambulia kupeleka gridi ya umeme Kigoma. Njia ya kwanza ni ile ya dharura ya kutoka Urambo, tunapitisha substation kutoka Urambo, Nguruka mpaka Kidahwe na mwakani tunakamilisha, hiyo ya kwanza. Ya pili ni kutoka Kigoma hadi Nyakanazi kilometa 283 kutoka Nyakanazi tunapeleka KV 220 Kigoma mpaka Kidahwe, hiyo ni ya pili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaanza kutekeleza Malagarasi, niipongeze sana Serikali wiki iliyopita tumepata dola milioni 140 kwa ajili ya kuanza kutekeleza mradi wa Malagarasi. Napo tunajenga mradi kutoka Malagarasi kilometa 53 mpaka tena Kidahwe, hiyo ni njia ya tatu. Ya nne ni kutoka Sumbawanga hadi Mpanda mpaka tena Kigoma jamani, wananchi wa Kigoma mtafurahi tu muda sio mrefu. Tunashukuru sana kwa ushirikiano wenu lakini Serikali imejipanga vizuri sana katika hilo. Tuvumilieni kidogo lakini Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan amejipanga vizuri, Makamu wa Rais yuko vizuri, Waziri Mkuu ndio usiseme anatuongoza vizuri tutawafikishia umeme wa gridi Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vivyo hivyo hata Mpanda tumeanza kutekeleza mradi mzuri wa kutoka Tabora kupitia Ipole, Inyonga mpaka Mpanda. Juzi akaeleza Mheshimiwa Mbunge mwingine tupitishe mpaka Nsimbo, tutapita Nsimbo kwa sababu gridi inapita maeneo yale yale. Kwa hiyo, tuna matumaini kwamba umeme wa gridi utafika maeneo yote. Kwa wakati huu tuna vifaa ambavyo vitakwenda kurekebisha tatizo kwa muda mfupi lakini suluhisho la muda mrefu kwa wananchi wa maeneo hayo linakuja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hata wananchi wa Simiyu, Simiyu ni Mkoa unaojenga viwanda, tumeanza kujenga gridi ya Taifa kutoka Ibadakule Shinyanga umbali wa kilometa 109 kwa kutumia fedha ya ndani, eneo la Imalilo tumeanza kutengeneza muda si mrefu. Kwa hiyo, ni matumaini yetu tutakamilisha vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, deni la ZECO na TANESCO. Kwanza niishukuru Serikali mwaka juzi kulikuwa na deni la VAT la shilingi bilioni 22. Kwa umakini wa Serikali yetu deni likaondolewa, tunawapongeza sana viongozi wetu. Limebaki deni la KVA charge, nitoe tu mrejesho kwamba linakwenda vizuri, technical team ya masuala ya Muungano, kwa taarifa nilizopewa leo imekaa mwezi uliopita na tarehe 8 na tarehe 9 mwezi huu itakaa kwa ajili ya kufanyia kazi jambo hili kwa sababu liko kwenye Serikali ya Muungano na litakamilishwa muda si mrefu. Kwa hiyo, wenzetu wa Zanzibar mtuvumilie kwa sababu najua kamati ile ya masuala ya Muungano inalifanyia kazi kwa kina sana Inshaalah najua matokeo yake yatakuwa mazuri zaidi kama ambavyo imekuwa siku za nyuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumze kidogo kuhusiana na vituo vya mafuta vijijini. Tunaposema kupeleka nishati vijijini naomba isitafsirike kwamba ni umeme peke yake. Nishati vijijiji ni pamoja na mafuta vijijini pamoja na gas ya mitungi vijijini. Tumeanza, katika mwaka uliopita tumepeleka takriban vituo vidogo 221 vijijini vya mkono mmoja walau wananchi wanaomiliki bodaboda na taksi waweze kupata mafuta kule vijijini. Hivi viroba vya mafuta kubebwa kwenye bodaboda tunataka yafike mwisho ili wananchi nao wapate huduma hii kulekule vijijini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, tumejipanga vizuri na wenzetu EWURA tuliwaambia wafanye mapitio upya pamoja na taasisi nyingine kuondoa mlolongo na ukiritimba na gharama kubwa ya uanzishwaji wa vituo hivi; ambavyo vinafanya Watanzania washindwe kuviendesha. Kwa hiyo, matumaini yetu tutakwenda vizuri katika eneo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, imeelezwa vizuri kuhusiana na deni la Mradi wa Bomba la Gesi Madimba. Serikali yetu inalipa na tunakwenda vizuri na mradi hauna mashaka. Deni lilikuwa ni Dola za Marekekani bilioni 1.2 tumeshalipa zaidi ya milioni 221 na tunakwenda kulilipa vizuri. Kwa trend ya kulilipa ni nzuri na wenzetu wa Hazina wanatupa ushirikiano mzuri tunakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bei ya mafuta ameeleza Mheshimiwa Mwijage ni mtaalam mzuri sana. Mheshimiwa Mwigaje nakupongeza sana kwani umenisaidia sana. Kwa kweli bei hupangwa na soko la dunia. Masuala haya ya mafuta na gesi kuna wakati bei kwenye soko la dunia kwa sababu mbalimbali inaweza ikashuka. Mkiona hapa tumeshusha bei maana yake na kule imeshuka. Sisi huwa tunatangaza bei inayopangwa pia kwenye soko la dunia. Bahati nzuri sana bei inapopanda kwenye soko la dunia na huku ikapanda huwa tunapiga kelele lakini ikishuka kule na huku ikishuka huwa sisikii watu wakipiga kelele. Hiyo ndiyo fluctuation ya soko la dunia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hili lazima tuelezane ukweli. Kwa hiyo, ndugu zangu kazi yetu ni kufuatilia, je, vyanzo vya bei hivi ni halisi? Niwaombe sana wenzetu Wakala wa Mafuta (EWURA) kuanza kufuatilia kisasa bei za soko la dunia katika mafuta ili Watanzania waweze kuelewa vizuri zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu ya muda ambao umenipa, naomba labda nirudie jambo moja tu katika mradi wa EACOP. Watanzania wanataka kujua kuhusu semina kuelezea manufaa ya mradi huu na ule wa LNG. Tumetaka kuwa na semina kwenye maeneo ambako miradi inapita kwa ajili ya kuwajengea uwezo na ufahamu wananchi namna ya kushiriki kwenye miradi hii ya kimkakati. Semina hizi tumezianza katika maeneo ya Nzega lakini Waheshimiwa Wabunge mnaotoka katika maeneo ya miradi ya Kagera, Geita, Shinyanga mpaka kufika Tanga tunategemea kuanzia wiki ijayo tunaanza semina. Tunapenda sana tuwashirikishe Wabunge wawasaidie wananchi ili miradi hii iwe na manufaa na wajiandae. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kuhusiana na kuwashirikisha katika kazi za bomba, tumeandaa kanzidata (database) kwa ajili ya makampuni yote. Makampuni yote ya ndani yameorodheshwa kupitia Kanzidata ya EWURA. Kwa hiyo, niombe kama kuna kampuni ya kizalendo, ya kitanzania na ina uwezo, sifa na nia ya kufanya kazi katika miradi hii ipeleke company profile yake EWURA ili kusudi wakati wa mchujo tuzingatie makampuni ya kitanzania siyo makampuni yaliyosajiliwa Tanzania. Hii ndiyo itakuwa jambo lenye manufaa kwetu kwa ajili ya kunufaika na miradi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa upande wa LNG tumeshalipa fidia ya shilingi bilioni 5.71. Tunachofanya sasa ni kufanya mapitio ya eneo ambako wananchi watanufaika. Yako maeneo ya Likong’o, Mtomkavu na Masasi ya Leo. Maeneo hayo yote tunataka wananchi washiriki ipasavyo katika mradi huu wa kimkakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu leo kazi kubwa ni kuomba fedha na naomba mnitume tukakimbie tuwapelekee umeme kwenye vijiji, nisitumie muda mrefu sana, niwaomba Waheshimiwa Wabunge mtupitishie fedha zetu, sisi tupo tayari kwenda kufanya kazi. Ahsanteni sana kwa ushirikiano wenu na mimi naunga mkono hoja kwa asilimia 100. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Spika, naafiki.