Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Dr. Angeline Sylvester Lubala Mabula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Ilemela

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kuchangia katika Wizara hii ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, nianze kwa kuwapongeza kwa kazi nzuri ambayo wameifanya na Wabunge wote ni mashahidi wameweza kuwapongeza. Nami nawapongeza kwa kazi kubwa waliyofanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika mazungumzo na uchangiaji wa Wabunge, kuna maeneo mawili mazuri na ni maeneo ya kimkakati kwa Taifa letu lakini Wabunge wengi hawakuyazungumzia sana, wamezungumzia masuala ya REA pamoja na vinasaba. Nataka nizungumzie maeneo mawili ya bomba la mafuta kutoka Hoima mpaka Chongoleani pamoja na Bwawa la Mwalimu Nyerere.

Mheshimiwa Spika, nianze na Bwawa la Mwalimu Nyerere. Kama unavyotambua, maeneo mengi tunapokuwa na miradi ya kimkakati usipofanya maandalizi ya awali migogoro ya ardhi inakuwa ni mingi. Napenda nilithibitishie Bunge hili kwamba katika Bwawa la Mwalimu Nyerere, pamoja na kazi zinazoendelea, Wizara pia imehakikisha inafanya kile inachotakiwa kufanya ili kuhakikisha kwamba tunalinda maeneo yale ya vyanzo vya maji, misitu na maeneo oevu.

Mheshimiwa Spika, kilichofanyika pale ni kuwaondoa wale waliokuwepo, kulikuwa na mahoteli kama matatu; Serena Luxury, Amara Camp pamoja na Retreat Safari Ltd. Hoteli hizi zimelipwa zaidi ya Sh.3,754,000,000 ili kupisha maeneo yale. Kazi inayoendelea pale ni kupanga matumizi kwenye Mji wa Mloka pamoja na Mji wa Kisasi.

Katika Mji wa Mloka urasimishaji utafanyika kwenye kaya kama 1,000 na katika ule Mji wa Kisasi michoro 19 yenye viwanja 4,043 imeandaliwa. Kwa maana hiyo tayari tutakuwa tumeweka mazingira mazuri ili mradi unapoendelea basi kusiwepo na changamoto au migogoro ya ardhi katika eneo hilo.

Mheshimiwa Spika, lakini upande wa bomba la mafuta, tayari eneo la Mkuza kutoka Hoima mpaka Chongoleani utambuzi wa maeneo yale ya Mkuza umeshafanyika na kuweza kujua kama kuna maeneo yanahitaji kulipwa fidia ni maeneo kiasi gani. Tayari maeneo 12 yametambuliwa katika eneo lile ambayo hasa yataanza na masuala mazima ya ujenzi wa kambi zile ambazo zitatumiwa na wale wajenzi wa bomba la mafuta.

Mheshimiwa Spika, lakini pia katika maeneo ambayo wananchi watakuwepo pale kunapangwa miji ambayo itarahisisha kusogeza huduma za jamii katika maeneo yale kwa sababu bomba lile la mafuta litakapopita ni wazi shughuli za kijamii zitakuwepo. Kwa hiyo, tayari Sh.20,457,965,000 zitalipwa kama fidia katika yale maeneo ambapo camp hizo zitajengwa. Katika maeneo hayo watakaonufaika kwa fidia hiyo kwenye ujenzi wapo watu wa Misenyi, Kiteto, Kondoa, Iramba, Nzega, Igunga, Bukombe, Chato, Muheza, Handeni na Kilindi. Tayari utambuzi umefanyika na kinachofuata sasa ni namna ya kuweza kuona ni jinsi gani hatua hizo zitafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumechukua hatua hiyo kama Wizara ili kwanza kuleta usalama kwenye lile bomba la mafuta kwa sababu usipofanya hatua hizo za kupanga matumizi kwenye eneo lile ndiyo mwanzo sasa wa kugombania pale, watu watakuwa wana-struggle kutaka kuongezeka pale. Wizara inashirikiana na Wizara ya Nishati kuhakikisha mpango mzuri unawekwa pale ili watu waweze kukaa kwa amani kwa sababu tayari pia ni fursa kwao kwa shughuli za kimaendeleo. Maana ile miji ikipangwa tayari na uwekezaji katika maeneo yale utakuwepo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hilo nilitaka nilithibitishie tu Bunge kwa sababu wengi hawakuchangia maeneo hayo, nikaona basi kama Wizara tuseme kile ambacho Serikali imefanya kuhakikisha hii miradi mikubwa ya kimkakati inalindwa ili kuepusha migogoro na wananchi. Pia usalama wa maeneo yale tunaweka maandalizi kuweza kujua ni jinsi gani ambavyo tunaweza kufanya.

Mheshimiwa Spika, pamoja na hayo pia kuna maeneo mengine 12 ya vituo vya kupozea, tayari wafidiwa 392 wametambuliwa. Jumla ya fidia yao ni shilingi 1,600,000,000.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Serikali tayari imeshafanya maandalizi yake na tunaendelea kuhakikisha kwamba kila kilichopangwa kwenye eneo lile kinafanyika vizuri. Tumefanya hivyo ili bomba linapojengwa basi pasiwepo tena na sintofahamu katika suala zima la umiliki wa maeneo, lakini pia na kuyapanga yaonekane kwamba yamekaa vizuri.

Mheshimiwa Spika, nilitaka kuchangia hilo ili kutoa taarifa kwa Bunge lako nini ambacho kimefanyika katika hii miradi ya kimkakati. Vivyo hivyo hii inafanyika pia kwenye ile miradi ya SGR, nako Wizara ya Ardhi tupo kuhakikisha kwamba tunaepusha changamoto zinazoweza kujitokeza kutokana na matumizi ya ardhi au kwa watumia ardhi.

Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi)