Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Iddi Kassim Iddi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Msalala

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. IDDI K. IDDI: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii. Kwa niaba ya wananchi wa Msalala naomba nichangie hotuba ya bajeti hii ya Wizara ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, moja kwa moja nianze kwa kumpongeza Mama yetu Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya katika Taifa letu hili la Tanzania. Nitakuwa mchoyo wa fadhila kama sitampongeza Mheshimiwa Waziri Kalemani kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya katika nchi hii ya Tanzania na Deputy wake kwa kazi kubwa anayoendelea kuifanya. Nitakuwa mchoyo wa fadhila bila kuwashukuru watumishi wote wa Wizara ya Nishati kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niende moja kwa moja kuchangia katika maeneo matatu. Nianze kuchangia katika suala nzima la REA. Mheshimiwa Waziri nikuombe suala la REA hili katka Jimbo langu la Msalala na Mheshimiwa Mbunge mwenzangu leo yule wa Zanzibar ametutania hapa kwamba mradi wa REA katika Jimbo langu la Msalala Mheshimiwa Waziri bado na wewe mwenyewe ni shahidi. Pia sijui ni kwa nini Jimbo langu la Msalala na Mkoa mzima wa Shinyanga tumekuwa na bahati mbaya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama alivyosema Mbunge mwenzangu hapa tuna vijiji 92 katika Jimbo la Msalala lakini vijiji 63 bado havijapatiwa umeme. Siyo hilo tu hata mradi wa umeme jazilishi kwa maana ya desentification katika baadhi ya maeneo bado haujasambaa kwa uhakika. Nimuombe Mheshimiwa Waziri baada ya Bunge hili tuweze kuambatana kwenda katika Jimbo la Msalala tuweze kuzindua miradi mbalimbali inayoendelea, lakini pia tufike katika maeneo yenye changamoto za umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu na maeneo mengine ya Mkoa wetu wa Shinyanga ukosekanaji wa umeme unapelekea kuhatarisha ndoa za kina mama. Akina mama wanajitahidi sana kupika wali na kuhakikisha umenyooka lakini unakuwa ni bokoboko kwa sababu wanatumia mbinu ya kutwanga badala ya mashine za kisasa za umeme ambazo zitachambua mchele vizuri na kuwapelekea kupika wali ambao utapelekea kudumisha mapenzi ndani ya ndoa. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri chondechonde fika Jimbo la Msalala tuone namna gani tunaenda kuanzisha umeme katika Kata za Jana, Mwalugulu, Mwakata na kata zingine zote zilizoko katika Jimbo la Msalala. Kwa kufanya hivi utanusuru ndoa za kina mama. Nikuombe baada hapa twende tukanusuru ndoa hizo za kina mama wa Jimbo la Msalala. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizungumzie changamoto ya umeme katika uwekezaji. Katika Jimbo la Msalala wengi wetu ni wawekezaji katika sekta ya madini, tunategemea umeme ili shughuli hizi za uchimbaji ziweze kufanikiwa. Waziri alitoa maelekezo kwamba katika Kata ya Lunguya, Kijiji cha Nyangarata maeneo yote yenye machimbo wapeleke umeme. Nashukuru Mheshimiwa Waziri tayari umeme unaelekea katika Kijiji cha Nyangarata, lakini bado Ntambarare umeme haujafika. Haya maelekezo unayatoa huku Mheshimiwa Waziri watendaji wako hebu jaribu kuyafatilia wanayapuuza, ulisema utakapotoka waanze kupeleka umeme mara moja katika Kijiji cha Ntambarare Segese katika Kata ya Segese. Mheshimiwa Waziri hebu tusaidie kwa sababu ukuaji wa sekta ya madini katika Jimbo langu la Msalala tunategemea nishati ya umeme.

Mheshimiwa Spika, lakini pia kumekuwa na changamoto ya gharama. Wawekezaji wengi wanalia kwa sababu ya changamoto ya gharama na gharama hiyo ni KVA charges kama penalty. Unapoenda kuwekeza hao wateja wakubwa kuna gharama ambayo huwa inatozwa kama penalty kwa wawekezaji hawa na gharama hiyo inapelekea kuleta changamoto kubwa katika uwekezaji. Leo hii mtu analipa gharama ya umeme mathalani shilingi milioni 40, lakini hapo anapigwa penalty kwa ajili ya matumizi ya umeme wa ziada ambao yeye hautumii. Niiombe Wizara hebu jaribuni kuona ni namna gani sasa mnaenda kutupunguzia charges hizi na ikiwezekana mziondoe ili ilete unafuu kwa wawekezaji wetu katika maeneo hayo ya migodi na viwanda vikubwa katika Jimbo la Msalala. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia ni namna gani mnaweza kuimarisha ugawaji wa transformer katika maeneo mbalimbali katika Jimbo langu la Msalala lakini pia katika maeneo mengi nchini kote. Nimekuletea concern za wafanyabiashara wengi ambao mpaka sasa viwanda vimesimama kwa sababu ya ukosefu wa transformer. Kwa hiyo, nikuombe Mheshimiwa Waziri bajeti hii itakapoenda kupita uone namna gani unaenda kuimarisha suala zima la usambazaji wa transformer kwa wafanyabishara wetu hawa katika maeneo yale ili na wao waweze kuendeleza viwanda vyao hivyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nikushukuru kwa nafasi hii, ahsante sana. (Makofi)