Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Boniphace Nyangindu Butondo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kishapu

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. BONIFACE N. BUTONDO: Mheshimiwa Spika, nami naomba nikushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu kabisa ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri Kalemani pamoja na Naibu Waziri wake, niwapongeze pia na watendaji wote katika Wizara hii. Sababu kubwa kwa nini nampongeza Mheshimiwa Kalemani ni kwa namna ambavyo amekuwa mfano wa kuigwa kwa Mawaziri na hasa katika jambo kubwa la kutusikiliza sisi lakini pia kufika kwa wakati katika majimbo yetu na kuona changamoto na matatizo yaliyopo katika maeneo yetu. Kweli wewe ni kiongozi wa kuigwa na Mawaziri wengine ningependa waige mfano na mwenendo wa Kalemani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Kishapu ina jumla ya vijiji ya 127 lakini vijiji 75 vina umeme na vijiji 52 bado vina tatizo kubwa la umeme. Hivi navyozungumza kata tano hazina kabisa umeme kati ya kata 29 hata Kata nakotoka ya Lagana. Kata hizo ni Lagana, Bunambiu, Mwasubi, Itilima na Masanga, hizi kata hazina kabisa umeme hata katika kijiji kimoja. Kwa hiyo, hili bado ni tatizo kubwa sana katika eneo langu. Naomba sana Wizara katika hii REA III Awamu ya Pili vijiji hivi vyote viweze kupata umeme.

Mheshimiwa Spika, namshukuru Mheshimiwa Waziri mwaka 2017 aliweza kufika katika Jimbo la langu katika Kata za Ukenyenge, Mwamashele na bahati nzuri aliahidi kwamba maeneo hayo yatapatiwa umeme. Kata ya Mwamashele nguzo zimefika lakini mpaka sasa hatujapata umeme, kwa hiyo, bado wananchi wanasubiri umeme. Mimi ninahakika kwa jinsi ambavyo Waziri ameahidi atakwenda kutekeleza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna changamoto kubwa ya kukatika umeme katika Mji wa Munze ambao ni Makao Makuu ya Wilaya yangu ya Kishapu, liko tatizo kubwa na kwa kweli jambo hili linasikitisha. Pengine wakati una-wind up naomba ueleze tatizo ni nini kwa sababu maelezo yako mengi. Kwa kutwa nzima umeme unapatikana kwa wastani wa asilimia 30 ama 40 asilimia 60 unakatika; kwa siku unaweza ukakatika mara tatu, mara nne ni tatizo kubwa sana. Tunaomba kujua tatizo ni ni linalosababisha kukatika kwa umeme katika maeneo haya.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo nataka nizungumzie ni masuala mazima ya watumishi. Wilaya ya Kishapu tuna watumishi 12 peke yake na Mheshimiwa Waziri anafahamu watumishi katika sekta hii muhimu ni kubwa. Pale inapotokea emergency, kwanza katika emergency gang inatakiwa watumishi 12 waende haraka kwa ajili ya kutatua tatizo sasa unapokuwa na watumishi wilaya nzima 12 panapotokea emergency unafanya nini pia kuna maeneo yanayotakiwa kutolewa huduma za kila wakati, kwa hiyo, hili ni tatizo kubwa.

Mheshimiwa Spika, pia nizungumzie suala zima la wakandarasi. Nchi nzima wakandarasi wametolewa katika kila wilaya, Wilaya ya yangu ya Kishapu haijapata mkandarasi, hili ni tatizo sijajua sababu ni nini. Wakati Mheshimiwa Waziri ana-wind up aeleze nini tatizo. Nimeendelea kufuatilia mchana huu Mkoa mzima wa Shinyanga hatujapata wakandarasi. Kwa hiyo, hili bado ni tatizo na pengine nataka nipate majibu tatizo ni nini. Juzi Waziri alisema atakapowaita hao wakandarasi pamoja na mameneja wa TANESCO kutoka katika kila wilaya atawapa maelekezo wawasiliane na Waheshimiwa Wabunge ili waweze kuona maeneo gani ambayo yana changamoto na ya kufanyia kazi kwa haraka, kwa hiyo, kwangu hili ni tatizo kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka nizungumzie pale panapotokea matatizo ya moto. Mwezi Machi palitokea tatizo la kuungua nyumba tatu katika Kata ya Mwaweja Wilayani kwangu Kishapu kutokana na short za umeme. Tumepata tatizo kubwa sana kuzima moto katika nyumba zile lakini pia hata TANESCO wenyewe kuwahi kufika ilikuwa ni tatizo kubwa. Tatizo hili limechangiwa pakubwa sana kutokana na kutokuwa na magari na watumishi wa kutosha. Kwa hiyo, naomba sana mjaribu kuitizama Kishapu na watusaidie ili tuondokane na tatizo hilo.

Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)