Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Maimuna Ahmad Pathan

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ili nichangie katika Wizara hii nyeti sana ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, kwanza, napenda kutoa shukrani zangu za dhati na pongezi nyingi sana kwa Kamati ya Nishati na Madini kwa kazi yao nzuri ambayo wameifanya kupitia kwa Mwenyekiti wake na wajumbe wote kwa kuishauri vizuri Wizara hii ya Nishati na mpaka inaendelea kufanya vizuri kwa sasa. Pia napenda kumpa pongezi nyingi sana Mheshimiwa Kalemani, Msaidizi wake na Katibu Mkuu na watendaji wote kwa kazi nzuri wanayoifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Kalemani kwa kweli ni mtu ambaye ni msikivu, anajitahidi sana kutusikiliza. Mimi nimemsumbua mara nyingi sana lakini namshukuru Mungu kila napomuendea kwa suala linalohusu TANESCO na mambo mengine ya Wizara yake, huwa ananijali na huwa tunampigia simu Meneja wa TANESCO na matatizo yote tunayaongelea vizuri. Kwa kweli, Mungu akubariki Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Wizara ya Nishati kwenye eneo la umeme ni Wizara nyeti sana. Umeme ni kitu cha msingi sana kwenye maendeleo kwenye nchi yoyote. Tunashukuru mmeweka umeme wa REA sehemu nyingi sana kwenye vijiji vyetu. Ombi langu ambalo bado liko kwenu umeme wa Mkoa wa Lindi haueleweki au hauaminiki kwani unakatika sana mara kwa mara. Ndani ya dakika 20 au 10 umeme lazima ukatike, hauwezi ukanunua vitu ukaweka kwenye friji vikakaa salama, itakuwa ni uongo vile vitu vinaharibika. Kwenye Mpango wa Maendeleo wa Taifa mmesema kukuza ushiriki wa sekta binafsi kwenye maendeleo ya kiuchumi kwa kweli tunatakiwa tujitahidi kwa sababu kuna watu wengi wamejiajiri kupitia kazi hizi za umeme lakini wanashindwa kufanya kazi zao vizuri kwa kuwa umeme huu hauko stable. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru Mheshimiwa Kalemani amesaidia sana kwenye Mkoa wa Lindi hususani Wilaya ya Liwale, Nachingwea na Ruangwa. Inaonekana kweli kuna mafanikio lakini naomba uongeze nguvu kwa sababu ile kasi ya kuzimika sana imepungua lakini bado unaendelea kuzimikazimika. Naomba Waziri atusaidie ili wananchi wale waweze kufaidi huduma hii ya umeme na wao wajisikie vizuri waone kama vile walivyo watu wa Dodoma wanavyofaidi umeme wao. Sisi wananchi wa Lindi tungefurahi sana tupate umeme kama huu wa Dodoma ili tuweze kujisikia vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo napenda kulichangia kwenye Wizara ya Nishati ni kuhusu gesi asilia. Gesi asilia ni muhimu sana kwa sisi wananchi wa Tanzania hasa wenye kipato cha chini ili iweze kutusaidia. Tunaomba sana hii gesi asilia ingeanza kutumika vizuri na pia isambazwe sehemu zote vizuri sana ili iweze kusaidia. Matumizi ya gesi asilia ukiangalia gharama zake ni nafuu sana kuliko vitu vingine.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, kuna magari yanayotumia gesi asilia sasa hivi, matumizi ya yale magari nimejaribu kuongea na wale wataalam yako chini sana karibu nusu ya gharama ya mafuta ya petroli tunayotumia sasa hivi. Kilo moja ya gesi asilia ni Sh.1500 ambayo inaweza kutumika kwa zaidi ya kilomita, samahani kidogo nimesahau lakini gharama yake ni chini zaidi ukilinganisha na petroli lita moja. Tunaomba Wizara hii ya Nishati ijitahidi sana kusambaza hizo gesi asilia na pia iweze kutoa elimu kuhusu matumizi ya gesi asilia ili Watanzania tuweze kufaidika na gesi yetu ambayo iko katika nchi yetu ya Tanzania zaidi Mikoa ya Kusini. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa karibuni kulitokea tatizo la LUKU kwenye ununuzi wa umeme. Tunashukuru Waziri wetu alifanya jitihada na tuliona juhudi alizokuwa amefanya hali ikarejea. Hata hivyo, siku mbili, tatu za juzi mpaka jana ile hali imerudi tena kwa Mkoa wa Dodoma. Watu wengi wamejaribu kununua umeme wameshindwa lakini sasa hivi kuna watu nimewasiliana nao wanasema sasa hivi ile hali imeanza kurudi umeme umeanza kupatikana lakini kulikuwa na kama siku mbili tatizo lilirudia tena. Tunaomba Waziri wetu ambaye anajituma sana Mheshimiwa Kalemani ajaribu kuliangalia tena tatizo hili ili wananchi wako tuweze kuwa vizuri. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante.

MHE. MAIMUNA A. PATHAN: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja. (Makofi)