Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Noah Lemburis Saputi Mollel

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Arumeru-Magharibi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. NOAH L. S. MOLLEL: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Spika, nitakuwa mwizi wa fadhili nisipompongeza sana Waziri na timu yake nzima kwa maana ya Naibu wake pamoja na Wizara yake kwa ujumla ikiongozwa na Katibu Mkuu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda pia kusema kwamba katika usambazaji wa nishati kwa maana ya umeme Tanzania kwa kweli tumepiga hatua kubwa sana. Ukipita kwenye mapori na maeneo mbalimbali ukiona jinsi ambavyo nguzo zinapita utaona jinsi gani Serikali ya Chama cha Mapinduzi imejitahidi kwa kiwango kikubwa mno. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika hali hiyo ya Serikali ya Chama cha Mapinduzi kutekeleza Ilani ya usambazaji wa umeme bado tunaendelea kusema tunakwenda kusonga mbele na kuikumbusha Serikali kuendelea kumalizia maeneo ambayo bado. Katika usambazaji wa umeme wakandarasi ambao walikuwa wamepewa kazi hii wengine wamekuwa siyo wazuri sana, siyo wote lakini siyo wazuri sana. Hivyo, Wizara ni vizuri ikaangalia kwa makini sana wakandarasi hawa ambao wamekuwa hawafanyi kazi vizuri.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano kwenye Jimbo langu la Arumeru Magharibi mkandarasi aliyepewa kazi pale amechimba mashimo kwenye maeneo mengine hajaweka nguzo, amesimamisha nguzo hajaweka waya, maeneo mengine hayajakamilisha miradi kwenye vijiji na na kadhalika. Uchimbaji wa mashimo umewafanya wananchi, ng’ombe na mbuzi kuvunjika miguu. Naomba Wizara chini ya Waziri wetu Mheshimiwa Kalemani (mchapakazi) afike kwenye Jimbo la Arumeru Magharibi ili kuweka msukumo katika usambazaji wa umeme kwenye Kata za Bwawani, Nduruma, Kisongo, Musa, Mwandeti, Lingijale, Lemanyata, Kimyaq, Sambasha, Ikiding’a, Oljuroto, Tarakwa, Oturumet, Matebesi, Naroi na Oljoro. (Makofi)

Mheshimiwa Sjpika, kama unavyofahamu Jimbo la Arumeru Magharibi ni jimbo ambalo limeweka Jiji la Arusha katikati, kwa hiyo sisi tumezunguka Jiji la Arusha kama yai, wananchi wale wanahamu sana ya umeme. Kwa hiyo, nimuombe sana Mheshimiwa Kalemani aweze kutembelea na kuweka msukumo wa usambazaji wa umeme kwenye jimbo hilo.

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ni kuhusu suala la bei ya nguzo. Suala hili limekuwa kizungumkuti kwa sababu Mheshimiwa Waziri amekuwa akijitahidi sana kutumia nguvu kubwa kueleza kwenye mihadhara mbalimbali kwamba usambazaji ni shilingi 27,000 lakini jambo hili TANESCO wanapolitelekeza linakuwa kinyume chake. Sasa inawezekana tunailaumu TANESCO lakini kuna nini huko ndani? Naomba Mheshimiwa Waziri aweze kufafanua zaidi kupitia waraka maalumu, kama ameandika sijui, lakini kama hajaandika atoe waraka TANESCO kwa maana ya TANESCO mikoa yote Tanzania, umeme wa REA ni shilingi 27,000, je, miradi ya TANESCO yenyewe ni shilingi ngapi, ni shilingi 177,000 au kuna tofauti ili mwisho wa siku wananchi waweze kuelewa gharama hii ya shilingi 27,000 na shilingi 177,000. Suala hili ni kizungumkuti katika utekelezaji, Waziri anatamka lakini utekelezaji unakuwa mgumu labda kuna kitu ndani. Hilo nalo Mheshimiwa Waziri aweze kuliangalia na kulitolea ufafanuzi zaidi.

Mheshimiwa Spika, suala la upandaji wa gesi. Ujio wa gesi umepunguza sana uharibifu wa mazingira na huko vijijini gesi hizi ndogondogo kwa mfano hii ya kilo sita imepanda kutoka shilingi 16,000 hadi shilingi 20,000. Sasa hali hiyo inaenda kutusababishia uharibifu wa mazingira, wananchi watarudi tena kwenye kukata miti na kuharibu mazingira. Naomba pia hili Mheshimiwa Waziri aliangalie kwa nini gesi ile ya kilo sita ipande kutoka shilingi 16,000 mpaka shilingi 20,000? Hili nalo ni jambo ambalo Wizara inatakiwa iliangalie kwa makini kwa sababu gesi imesaidia sana katika kutunza mazingira.

Mheshimiwa Spika, suala lingine ni kukatikakatika kwa umeme. Kumekuwepo na tatizo la kukatika kwa umeme, hatukatai kwa sababu mitambo ni mitambo tu lakini pale ambapo umeme unakatika ghafla basi tunaomba Wizara isimamie TANESCO iweze kutoa taarifa kwa wananchi kwamba umeme umekatika kwa muda huu na tunategemea uwake kwa muda fulani au siku tatu au nne. Kukaa kimya au kutowaeleza wananchi umeme umekatika kwa sababu gani na ni kwa nini inaleta wasiwasi na hofu na kurudisha pia maendeleo nyuma. Kuna watu umeme ukikatika dakika moja tu wanapata hasara kubwa sana katika kuendesha maisha yao.

Mheshimiwa Spika, umeme ni nishati ambayo inahitajika sana kwa Watanzania kwa ajili ya kuleta maendeleo tena maendeleo endelevu. Kwa hiyo, niombe kukatika kwa umeme tuwape taarifa wananchi ili waweze kukaa tayari kujua kwamba kuna nini na baadaye watapata kwa wakati gani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nakushuru sana kwa kunipa nafasi hii, naunga mkono hoja. (Makofi)