Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Dorothy George Kilave

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Temeke

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. DOROTHY G. KILAVE: Mheshimiwa Spika, nikushukuru sana kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Temeke pia niweze kuishukuru sana Serikali yangu kwa jinsi ambavyo inafanya kazi ni miaka mingi ambayo tukiwa tukilia kuhusiana na umeme lakini sasa nikiri kwamba wizara inafanya kazi vizuri sana. Lakini sio nyuma sana kuwapongeza katika hotuba yako Waziri hotuba nzuri ambayo imeleta matumaini kwetu sisi watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nizidi kuwapongeza jinsi gani mnafanya miradi ambayo miradi ya kimkakati hasa mradi ule wa bwawa la Julius Nyerere ambalo tuna matumaini nalo litakapoisha hakika hatutakuwa tena na kelele za umeme katika nchi yetu na hata tutakwenda kuuza Jirani. Niwapongeze bado kwa jinsi ambavyo wameweza kujenga sasa ujenzi wa njia ya kuendesha treni ya umeme ambayo tunaamini watanzania wote tuna matumaini ya kwenda kuiona na hata sisi wenyewe kuipanda kabla hata ya mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini naendelea kuipongeza Wizara ya Nishati kwa jinsi ambavyo mmeweza kuendelea kuipatia kipato TANESCO kwa jinsi ambavyo sasa naona hata mambo mengine yatakuwa yanakwenda kwa sababu mmekuwa mmechangamka na kipato sasa ni kikubwa, na tunaweza kuona kwamba miundombinu inaimarika. Lakini siyo tu niweze kuwapongeza pia kwa kuweza kuangalia madeni sugu na niwatie moyo tuendelee kutafuta madeni yale ili tuweze kuona kwamba sasa nishati inakwenda mahali pazuri.

Mheshimiwa Spika, ukweli ni kwamba napenda sana kuwapongeza kwa sababu kazi inaendelea na inaonekana niseme tu kwanza sasa kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sina mengi sana ya kusema lakini nimesimama kwa niaba ya wananchi wa Jimbo langu la Temeke TMK wenyewe tunajiita, ni jimbo lenye viwanda vingi sana naamini mnafahamu hilo. Lakini si viwanda peke yake lakini wananchi tulioko Temeke ni wananchi wengi sana ambao tunatumia nishati hii ya umeme. Lakini imekuwa ni tatizo sasa kwetu pamoja na hongera zote pongezi zote nilizowapa niseme tu kwamba wananchi wangu wa Temeke jimbo letu la Temeke hakika hata hapa niliposimama sasa hivi hakuna umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, imekuwa ni kila siku simu ni hizo imekuwa ni salamu za sisi kusalimiana umeme hakuna hiyo ndio inanishangaza lakini baada ya kufuatilia kwa muda mrefu na ninawashukuru sana mmekuwa mkinisaidia sana hasa naibu wako mara nyingi amekuwa akinisaidia mara kwa mara niseme nakushukuru sana Waziri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini baada ya kufuatilia hayo yote nimeona ya kwamba sisi tuna vituo viwili ambacho kimoja kinaitwa kingine TOL na kingine kule Tandika hivyo vyote vinatoa megawatt jumla 30 tu. Ambayo Tall wanatoa megawatt 15 na kule Tandika inatoa megawatts 12 ambazo ni 30. Lakini ukiangalia Jimbo la Temeke sisi wenyewe tunahitaji megawatt 117 ili umeme uwake kwa siku zote. Sasa lakini umeme huu hauwaki sijui ndio sababu ambayo hatupati umeme sina uhakika majibu mtaweza kutupa sisi leo wana Temeke. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile tunapata umeme kidogo sana hiyo iliyobaki megawatts 87 tunaambiwa tunapata kutoka Ilala Mkoa wa Ilala wa umeme sina uhakika sana lakini sisi wananchi karibu 125 tunaolipa deni tunaotumia LUKU na hatuna madeni kwa sababu sisi sote mmetufungia LUKU. Sasa niwaombe mtuangalie kwa jicho la kipekee kabisa Temeke, ni jimbo ambao lina watu wengi tunalipa kwa sababu wote mmetufungia LUKU hakuna deni sugu kama nilivyosema kwamba jamani endeleeni kutafuta madeni sugu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini sisi Temeke tunakiri kwamba hatuna madeni sugu hata kule viwandani mkumbuke kwamba ni jimbo ambalo lina viwanda vingi na sisi wenyewe kama jimbo kama halmashauri tunategemea sana kupata fedha kutoka katika yale makampuni au viwanda. Sasa wakikosa umeme siku moja siku mbili kila siku hata sisi makusanyo yetu yanapungua. Kwa hiyo, niombe sana mtuangalie kwa jicho la kipekee kabisa ili tuone kwamba tunaendelea kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia miundombinu ni chakavu sana mimi ninaamini Temeke ni ya siku nyingi sana na miundo mbinu yetu kule ni chakavu kwa sababu kila siku kama nilivyosema umeme unakatika. Yaani imekuwa ni salamu zetu ikifika tu asubuhi saa nne utapigiwa simu hata hapa naweza nikawaonyesha kwamba mama umeme huku hukuna. Ukiangalia jimbo zima tunakata kumi na 13 Kata ya Keko umeme hakuna sasa hivi Mibulani hakuna umeme Kurasini, hakuna umeme Azimio, Mtoni Makangalawe Sandari Buza Yombo Vituka, Kilakala Temeke 14, Chang’ombe na Tandika kote hakuna umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaombe sana ndugu zangu Temeke ni jimbo ambolo linaangaliwa watu wengi wanakuambia tunaenda TMK ndio kwenye uwanja wa michezo na hata juzi nimeomba kwamba hata ile Arena ije ijengwe Temeke sasa tukikosa umeme namna hii tutafanya kazi gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, niwaombe sana wizara mliangalie hili sio tu lakini vilevile miundombinu yetu ambayo iliwekwa zamani waya zile kupita juu sasa hivi malori mengi yanaingia na kutoka kwenye viwanda vile. Aidha yanachukuwa mizigo au yanapeleka vifaa vingine kwa ajili ya matengenezo sasa yale malori yanakuwa yanagonga zile nguzo au marefu sana yanakata zile waya hilo nalo ni jambo lingine ambalo linaonekana kabisa kwamba linatufanya tuwe tunakosa umeme mara kwa mara.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, kwa ushauri wangu tuunde mkakati wa makusudi wakuona kwamba sasa ile miundombinu iliyochakaa ifanyiwe kazi ninatamani sana kama fedha ipo na ninaamini fedha ipo kwamba miundombinu hii sasa ifanyiwe kazi na tuweze kuipitisha chini badala ya zile waya zinazopita juu kwa sababu nguzo ni za zamani sana ikiguswa kidogo tu imeanguka umeme hakuna.

Mheshimiwa Spika, na mpaka waje watengeneze inachukuwa muda kwa hiyo niombe sana mkakati huu tuujenge pamoja tuko tayari wana Temeke kusubiri kutoka kwenu na nyinyi muweze kutusaidia ili tuendelee kupata umeme. Kwa hiyo, niombe sana kwa ushauri mwingine wakati tunajipanga kupata miundombinu hii salama niombe sana kitengo cha emergence wasingoje wakaambiwa kuna tatizo la umeme mahali fulani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naamini kwa sababu ni waajiriwa wa TANESCO wana uwezo kabisa wa kufika ofisini bila kuambiwa kwamba kuna tatizo au kuna katizo la umeme wao wenyewe wapite kuhakiki, kutambua na kuainisha sehemu gani ina kasoro kwa kipindi kile kwa sababu wanazijua kila wakati kasoro zinatokea wapi. Kwa hiyo, niombe kabisa kitengo cha emergence sasa tufanye kazi kwa pamoja ili Temeke yetu sasa iwake na sio tena kusema kwamba umeme hakuna maana hizo ndio salamu zetu niwaombe sana ndugu zangu badala ya kusubiri simu za itilafu emergence sana ifanye kazi ya kila wakati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kwa kufanya hivyo ninaamini hiyo salamu yetu ya umeme hakuna Temeke itaisha. Kwa hiyo, niombe sana ndugu zangu na bado niwape hongera na ninaunga mkono hoja ahsante sana. (Makofi)