Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Kwa kweli nilikuwa nimejiandaa kuchangia kesho lakini tuendelee. Ni heshima kubwa umenipa, ninashukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo moja ambalo nilitaka kuzungumza tumesema kwamba tunataka kuleta umeme wa vyanzo tofauti tofauti. Nilikwenda kumuona Waziri wakati fulani. Namshukuru, alinipokea. Kuna watu walikuwa wanataka kuweka mradi wa umeme kwenye Jimbo langu, mradi wa solar. Nilivyoongea na Waziri alinipokea vizuri lakini nikiangalia utekelezaji wake kwa watendaji wake naona kama iko polepole sana kwa sababu nimekuwa nikifuatilia sioni kama napata majibu vizuri.

Mheshimiwa Spika, nachotaka kusema ni nini? Kama mradi huu wa solar utaweza kujengwa kwenye Jimbo langu la Kalenga kwanza utausaidia Taifa kupata umeme kwa sababu hawa watu wanataka kuleta Megawatt 50 ambazo wataziingiza kwenye grid ya Taifa. Lakini pia kwenye Jimbo langu watu watapa ajira, pamoja na kuongeza uchumi katika maisha yao, hii ni muhimu. Nataka nikuambie Waziri hili jambo nitaendelea kulifuatilia na wewe unisaidie kuhakikisha kwamba huu mradi wa solar kwenye Jimbo la Kalenga unatekelezwa na huyu mtu ambaye ameonesha nia ya kutaka kuweka huu mradi apate hiyo fursa kwa sababu itatusaidia kufikia malengo ya Kitaifa ya kuhakikisha kwamba tunaongeza megawatt na kuwa na vyanzo tofauti tofauti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo ningependa kuishauri Wizara na TANESCO kwa ujumla, tunavyopeleka huu umeme wa REA III sasa kwenye vijiji tuhakikishe kwamba tunaangalia Taasisi. Of course, maagizo wewe Waziri umeshatoa lakini nataka kwa watendaji wako wafahamu hili ni suala muhimu sana taasisi kama shule, kama zahanati, hizo ni muhimu sana zipewe kipaumbele. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninapokea malalamiko hapa watu wananiambia umeme wa REA umepita lakini kwenye shule tumeambiwa kwamba tununue nguzo. Nafikiri hilo hapana. Kwmaba ni muhimu sana kuona kwamba tunapeleka umeme huko watoto wetu wasome lakini pia na kwenye zahanati watu waweze kupata huduma. Ninavyo vijiji kadhaa hapa ambavyo havina umeme na ninaomba kwamba katika mradi huu wa REA tunaokwenda nao sasa tuhakikishe kwamba vijiji ambavyo havijapata umeme tukiangalia kwenye Kata ya Wasa na vijiji kama Ulata lakini tukija kwenye Kata yangu ya Luhota kuna vijiji kama Wangama, Ikuvila ambavyo tayari kwa miaka mitatu watu wameshasuka umeme, wameshalipia lakini umeme haujawashwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nikushukuru Waziri kwa sababu Wizara yako kweli imefanya kazi hatuwezi kulalamika lakini ni muhimu kwa sababu kwamba kwa kadri tunavyoendelea kuongeza huduma na matamanio ya watu ndiyo yanakuwa makubwa. Kikubwa kingine ni kwamba kuna maeneo mengine tuna umeme mdogo.

Mheshimiwa Spika, kwa mfano, Kijiji nilichozaliwa mimi Kijiji cha Nyamihu kwamba tuna transformer iko mbali sana na wananchi wangu wamekuwa wakilalamika kwamba tunataka transformer isogee hapa kijijini ili sisi tuweze kuwa na umeme wenye phase tatu. Tuweke mashine za kukoboa, za kusaga. Kwa kufanya hivyo, tunavyoongezea hii huduma maana yake tunazalisha ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, rafiki yangu Gambo, siku moja alisema hapa kwamba anashangaa inakuwa kuwaje Serikali imesema itaajiri watu milioni nane. Hapana, Serikali inavyosogeza huduma karibu na wananchi kama umeme maana yake kama tunaweka mashine za kusagia maana yake tumezalisha ajira. Tunavyoweka viwanda vidogo vidogo maana yake ndivyo tunavyozalisha ajira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nikuombe sana kwamba taasisi tuzizingatie. Kwa mfano katika Kata yangu ya Kiwele nimekuwa nikilalamikiwa hapa kuna kitongoji kimoja cha Kipengele, yaani umeme umeruka lakini eneo hilo ndiyo lenye shule na eneo hilo ndilo lenye makanisa. Ndiyo maana tukasema kwamba focus iwe kwenye huduma za jamii zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia tuangalie vile vitongoji vilivyoko pembezoni, vile vilivyoko pembezoni tukianza navyo hivyo ni rahisi wakati mwingine kurudi katikati. Kwa hiyo, nikuombe sana kwa hayo machache tuone namna gani tunaweza tukapeleka umeme hasa kwenye jimbo langu. Lakini jambo ambalo pia nataka kusisitiza nikukumbushe tu Mheshimiwa Waziri Jimbo la Kalenga ndilo jimbo ambalo Spika wake hapa ndiyo amekaa muda mrefu kuliko mtu mwingine yeyote. Lakini ukiangalia pia Chifu wetu Mkwawa ndiye Chifu ambaye alitetea nchi hii kuona kwamba isitawaliwe na Wajerumani na wengine waliokuja. Kwa hiyo, ni Jimbo moja muhimu sana. Kwa hiyo mnavyofikiri akupeleka huduma lazima hizi facts zote mziangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Rais wakati anafanya uteuzi wa Wakuu wa Mikoa amewakumbuka waasisi wetu. Amechagua mtoto wa Nyerere, akachagua mtoto wa Sokoine. Maana yake amekumbuka michango ya hawa waasisi walichofanya. Lakini na Jimbo la Kalenga katika nchi hii lina mchango mkubwa sana. Kwa hiyo, wewe pamoja na Waziri mwingine wanavyofikiria kupeleka huduma, Jimbo la Kalenga lipewe kipaumbele kwa sababu ya mchango wake mkubwa sana kwenye Taifa hili la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa hayo machache. Naamini mambo mengine tutaendelea kuzungumza. Ahsante sana Spika kwa kunipa nafasi. (Makofi)