Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Dr. Florence George Samizi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Muhambwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. DKT. FLORENCE G. SAMIZI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana, kwa kunipa nafasi hii niweze kuchangia bajeti ya wizara hii muhimu sana ya Nishati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ikiwa ni mara ya kwanza kusimama kuongea katika Bunge hili lako Tukufu, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Mwenyezi Mungu aliyenipa neema na kibali cha kuwa Mbunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nikishukuru Chama changu Cha Mapinduzi kikiongozwa na Mwenyekiti wetu wa Chama mama yetu mama Samia Suluhu Hassan ambaye pia ni rahisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniamini na kuniteua kuweza kupeperusha Bendera ya Chama. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee niwashukuru wananchi wa Jimbo la Mhambwe ambao wamenipa ridhaa kwa kunipatia kura za kutosha ili niweze kuwatumikia, ninawaahidi wananchi wa Mhambwe kwamba sitawaangusha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niishukuru familia yangu kipekee mume wangu mpenZi Sadoki Mgendi, Watoto wangu Naomi, George, Georgette na Noah kwa uvumilivu, lakini na ushirikiano wao walionipa kipindi chote cha harakati hizi, Mwenyezi Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, napenda niwashukuru Wabunge wenzangu wa Chama Cha Mapinduzi, wakiongozwa na Wabunge wa Mkoa wa Kigoma kwa mchango wao wa hali na mali ulioniwezesha kuweza kufanikisha safari hii. Napenda niwashukuru ndugu jamaa na marafiki wote ambao walikuwa na mimi katika safari hii nzima, Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niungane na wenzangu waliokwisha kuongea kuendelea kumpongeza Waziri wa Nishati na Madini Mheshimiwa Dkt. Medard Kalemani, Naibu Waziri Stephen Byabato, lakini na Katibu Mkuu Mheshimiwa Leonard Masanja na viongozi wote wa Wizara hii, lakini na viongozi na wafanyakazi wote wa TANESCO kwa kazi kubwa, lakini kwa ripoti nzuri ambayo kwa ukweli imetujibu mambo mengi ambayo tulikuwa tukiyafikiria, mmetoa ripoti nzuri, mmefanya vizuri hongereni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitaanza kwa kuipongeza Serikali kwa jitihada kubwa sana inayofanya ya kutuunganishia umeme wananchi wake, umeme wa uhakika, lakini umeme wa bei rahisi, hii inajidhihirisha kwa miradi mbalimbali ambayo Waziri wetu wamewakilisha, lakini pia kwa miradi ile inayoendelea ule ukanda wangu wa Jimbo la Muhambwe ikiwemo ujenzi wa kituo cha kufua umeme katika maporomoko ya Rusumo megawatt 80.

Mheshimiwa Spika, lakini na ujenzi wa kituo cha kufua umeme katika Mto Malagarasi Megawatt 49.5. Hii ni dhahiri kwamba baada ya miradi hii kukamilika basi itatupunguzia mzigo wa kuendesha umeme kutumia generator ambayo ni gharama kubwa kutumia mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini vilevile itatusaidia tuweze kupata umeme wa uhakika, naipongeza sana Serikali kwa jitihada hizo tunaomba miradi hii isimamiwe vizuri ili iweze kuisha katika kipindi kilichopangwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na pongezi hizo bado pana changamoto hasa katika usambazaji wa umeme vijijini. Jimbo langu la Muhambwe lina vijiji 50, katika vijiji hivyo 50 umeme umeunganishwa katika vijiji 8 tu na uunganishaji huo ni ile tunaita katikati ya Kijiji tu. Haujafika kwenye nyumba nyingi za wananchi, lakini haujafika kwenye taasisi kama vile, shule, makanisa, misikiti na kadhalika, hospitalini na vituo vya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hii ilitokana na ucheleweshaji wa vifaa vya mkandarasi bandarini, ambavyo vifaa vile vilikaa zaidi ya miezi 12 vikidaiwa kodi. Nichukue nafasi hii kuishukuru Serikali ambayo iliingilia kati na kutusaidia kuvitoa vile vifaa, vifaa hivyo vimetoka wiki iliyopita. (Makofi)

Mheshimiwa Spia, sasa basi, nimuombe Waziri wa Nishati kutokana na ucheleweshaji huu, naomba sasa Jimbo langu la Muhambwe lipewe kipaumbele. Maana vijiji ambavyo havijapata umeme ni vingi, ikiwemo Kigaga, Kichananga, Rukaya, Magalama, Kumkuyu, Kibuye, Kukinama, Nyakilenda, Malolegwa na kadhalika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakuomba Mheshimiwa Waziri wa Nishati, kasi iongezeke, ili tuweze kusambaziwa umeme katika vijiji vyetu. Sambamba na hili, tunayo Kata ya Bitale, hii Kata iko takribani kilometa 2 kutoka Mji wa Kibondo kwa maana ni karibu sana. Lakini Kata hii bado imepata umeme katikati tu ya hiyo Kata, lakini vijiji vyake kama vile Kumuhama na Rubanga bado haijafikishiwa umeme.

Mheshimiwa Spika, naomba pia Kata hii ipewe kipaumbele, maana iko karibu mno kukosa umeme ni aibu kwa Jimbo langu la Muhambwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niishauri Serikali, kumekuwa na changamoto ya ucheleweshaji wa vifaa kufika eneo la utekelezaji kwa madai ya ucheleweshaji wa kodi au kwa ucheleweshaji wa kibali cha kusafirisha vifaa ambavyo vina uzito. Lakini naamini taasisi zote hizi ni za Serikali kwa maana kwamba, bandari, TANROADS zote ni mali ya Serikali na TANESCO ni Shirika la Serikali. Na TANESCO hii inatekeleza miradi ambayo ni mali ya Serikali, basi kuwepo na mazungumzo ndani ya taasisi hizi. Taasisi hizi ziweze kuongea kwa maana kwamba, ucheleweshaji huu usilete madhara kwa wananchi, wananchi wanahitaji kuona matokeo chanya. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo ikibidi basi kibali kitolewe cha kuruhusu vifaa hivi viweze kufika eneo la tukio huku kodi zikiendelea kulipwa. Hii itaharakisha mradi kutekelezeka, lakini pia, itatupunguzia gharama za kutekeleza mradi. Lakini pia, itatusaidia kwamba mradi uishe kwa wakati uliopangwa, ili Serikali iweze kulipa gharama ambazo ni sahihi kwa mlaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa kusema hayo, naomba kuunga hoja mkono. (Makofi)