Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Hon. Amb. Liberata Rutageruka Mulamula

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Nominated

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikushukuru tena kwa kunipatia nafasi hii ya kuweza kutoa na kufanya majumuisho ya mjadala uliokuwa unaendelea.

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru na kupitia kwako kumshukuru Mheshimiwa Spika kwa kuongoza na kusimamia mjadala wa bajeti yetu kwa umahiri sana. Nawashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kushiriki mjadala huu, maoni, michango na ushauri uliotolewa yataiwezesha na kuisaidia Wizara yangu kutekeleza majukumu yetu kwa ufanisi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee naomba kuishukuru tena Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama chini ya uongozi mahiri wa Mheshimiwa Mussa Azzan Zungu, Mbunge na Wajumbe wote wa Kamati kwa kuipatia wizara yetu ushirikiano mkubwa na kwa michango yao ambayo mizuri sana, ambayo wameitoa katika mjadala huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kwamba muda nilionao ni mfupi, lakini niwatambue sio kwa majina, lakini niwatambue na kuwashukuru kwa njia ya pekee Waheshimiwa Wabunge waliochangia hoja niliyoitoa leo asubuhi, jumla ya Waheshimiwa Wabunge 25 wamechangia kwa kuzungumza na pia Waheshimiwa Wabunge wengine wamewasilisha michango yao kwa maandishi, naomba niwashukuru sana, sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baadhi ya hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezitoa zimejibiwa kwa ufasaha muda mfupi uliopita na Naibu Waziri wangu Mheshimiwa Balozi Mbarouk Nassor Mbarouk, Mbunge, nichukue tu fursa hii kulihakikishia Bunge lako Tukufu kuwa hoja zote na maoni ya Waheshimiwa Wabunge zilizotolewa zitazingatiwa na zimepokelewa kwa moyo mkunjufu na zitazingatiwa na Wizara katika kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja ambazo hazitapata majibu ya kutosheleza katika hitimisho langu tutazijibu na tutaziwakilisha katika Ofisi ya Bunge kwa maandishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nijielekeze katika kutoa ufafanuzi wa baadhi ya hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wamezitoa; kwanza kabisa nitambue mchango wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nje, Ulinzi na Usalama. Maeneo waliyoyagusia ambayo mengi yao pia yamegusiwa na Wabunge, kubwa zaidi niseme ni suala la kuhusu majengo; kuhusu kuwekeza katika vitega uchumi katika kujenga ofisi za balozi zetu na makazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme napenda kulitaarifu Bunge lako Tukufu kwamba katika mwaka wa fedha 2021Wizara imetenga shilingi bilioni 20 kwa ajili ya kuendeleza viwanja na ukarabati wa majengo balozini. Hadi kufikia sasa Wizara ilitoa kazi ya usanifu na uandaaji wa mahitaji ya ukarabati wa majengo ya balozi mbalimbali kupitia kwa Mshauri Elekezi Chuo Kikuu cha Ardhi.

Mheshimiwa Naibu Spika, tayari mshauri elekezi ameshawasilisha mchoro na makisio ya gharama kwa ajili na ukarabati wa majengo wa Balozi zifuatazo; moja ambayo imekuwa inasemeka muda mrefu sana ni Ubalozi wetu Mascut - Oman. Ujenzi wa jengo la Ubalozi na makazi ya Balozi Mascut ambao utagharimu shilingi trilioni 3.6 zimeshatengwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Ubalozi wetu wa Nairobi ujenzi wa jengo la ubalozi shilingi trilioni 3.9 na pia Kinshasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, asubuhi hii Wabunge waliongelea kuhusu ujenzi wa jengo la ubalozi na kitega uchumi Kinshasa DRC; fedha tayari imeshatengwa na pia, Moroni - Comoro kuhusu ujenzi wa jengo la ubalozi tayari pia fedha imetengwa karibu shilingi trilioni 1.8.

Vilevile Wizara inafanya ukarabati wa jengo la ofisi ya Mambo ya Nje ya Zanzibar kama ilivyoelezwa, shilingi bilioni tatu badala ya trilioni tatu samahani nilikuwa namaanisha bilioni sio trilioni, shilingi bilioni tatu. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, iliongelewa kuhusu jengo la ofisi yetu Zanzibar ambayo Naibu wangu ameieleza, lakini napenda nilihakikishie Bunge kwamba, ukarabati wa jengo hilo umeanza. Pamoja na ukarabati wa jengo la Ubalozi wetu Washington DC ambalo ukarabati wa jengo hilo unategemea utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 5.8 na unatarajiwa kukamilika hivi karibuni.

Mheshimiwa Naibu Spika, nieleze tena pia, kuna Mpango wa mwaka 2018/2032 wa ujenzi, ununuzi na ukarabati wa majengo ya ofisi na makazi balozini ambapo Wizara inatenga fedha za maendeleo kwenye bajeti ya Wizara kila mwaka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, imeongelewa sana kwamba tumekuwa tunatenga hizi fedha kwenye bajeti, lakini hatupati, lakini napenda kushukuru Wizara ya Fedha imetuona. Wametenga karibu shilingi bilioni 20 ambazo zitatusaidia kuweza kukarabati hayo majengo na kujenga mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja kwamba, Serikali ikamilishe mchakato wa kuandaa sera ya mambo ya nje; kama alivyoeleza Naibu Waziri wangu, hii rasimu imekamilika, kinachosubiriwa sasa ni kuweza kuridhiwa na mamlaka katika mwaka huu tutakuwa tumeikamilisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, sera hii ina sehemu kubwa ya diaspora kwa hiyo, sera ya diaspora itakuwa sehemu ya Sera ya Mambo ya Nje. Nataka kuihakikishia Bunge Tukufu kwamba sera hii kwa kweli haitamaliza mwaka huu tutakuwa tumeimaliza. Hii ni kwa kutambua umuhimu wa diaspora katika kuchangia maendeleo ya nchi yetu, masuala ya diaspora kwa kweli yanapewa kipaumbele na kama alivyosema Mheshimiwa Kimei, mimi nilikuwa mdau sana, nimekuwa mdau sana wa masuala ya diaspora na nitahakikisha kwa kweli kama sikutunguliwa suala la diaspora kwa kweli nitaipa umuhimu wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na niseme pia kuhusu uraia pacha, hili ni suala lilishafanyiwa kazi kweli, iliyopo tu ni maamuzi ya kisera liweze kutekelezwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu hoja ya kwamba, Serikali iweke mpango mkakati wa kushughulikia changamoto ya muda mrefu ya uchakavu wa uhaba wa magari, hususani katika balozi zetu; naomba kukuhakikishia kwamba changamoto hii tayari tumeishughulikia Wizara imepata kibali kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kununua magari 67 katika mwaka huu wa fedha. Tayari fedha zimeshatumwa kwenye balozi zetu 18nje, kuweza kununua magari na bado tunaendelea kufuatilia magari mengine ambayo tumeagiza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara imeanza pia, kupeleka vituoni watumishi 137 katika kipindi hiki. Tumesikia kilio cha Waheshimiwa Wabunge kuhusu balozi zetu kwamba hazina watumishi.

Sasa mimi nitumie pia nafasi hii kuweza kuishukuru Wizara ya Fedha. Wizara ya Fedha imetuwezesha, tutapeleka watumishi 137 katika mabalozi zetu na tumezingatia weledi, tumezingatia uzoefu na tumezingatia ujuzi, kwa hiyo, sio kupeleka tu. Lakini kwa kweli tutakuwa tumeziimarisha balozi zetu na kila tunapopata rasilimali zaidi ya fedha, tutakuwa tunawaongezea uwezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, iliongelewa asubuhi hapa pia kwamba Wizara yetu iweze kufuatilia baadhi ya Wizara za kisekta, ambazo zikifanya kazi kwa juhudi na ufanisi zitaongeza pato la Taifa, kwa kusimamia uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo ambayo yana soko kubwa nje ya nchi kama vile, nyama ya mbuzi katika masoko ya nchi za Kiarabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niwaambie Wabunge kwamba, ushauri umepokelewa na unazingatiwa, lakini pia ulishaanza kufanyiwa kazi. Niwashukuru pia Mawaziri wenzangu kutoka hizi Wizara za kisekta, tumekuwa na ushirikiano wa karibu, tukiwa na ugeni tunakaa pamoja kimkakati na kuweza kuweka yale maslahi, ambayo kila sekta inaona inaupa kipaumbele, kwa hiyo, tunafanya kazi kwa karibu sana na sekta zote. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, pia katika ushirikiano huu Wizara ilifanikisha upatikanaji wa vibali kwa kampuni nane za Tanzania kuuza minofu ya samaki aina ya sangara katika nchi ya Saudi Arabia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuhusu Serikali kuzidisha juhudi kusimamia balozi zetu za nje, kutangaza fursa za kitalii na vivutio mbalimbali zilizopo nchini kwa kushirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii, tumepokea ushauri huu na kwamba utazingatiwa, lakini niwahakikishie kwamba tayari Balozi zetu kwa kweli zinafanya mambo mengi makubwa sana katika kuvutia utalii na kama mtakumbuka tulieleza hapa asubuhi kwamba mathalani balozi zetu zimepeleka sampuli za zao za korosho, lakini pia ubalozi wetu wa Malaysia umeweza kufanikisha kwamba ndege ya Malaysia inaweka matangazo ya utalii wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa na hoja mbalimbali kuhusu Wizara iendelee kuwapa viwanja mabalozi wa nje hapa Dodoma, kwa ajili ya kujenga ofisi na makazi ili balozi zihamie hapa. Napenda kukufahamisha kwamba Serikali tayari ilishatoa viwanja Jijini Dodoma kwa balozi zote na tayari ilishatoa hati kwa balozi zote zinazowakilishwa nchi zao hapa nchini. Kwa hiyo, sisi ni kuhamasisha kwamba wajenge ili waweze kuhamia makao makuu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, iliulizwa pia kwamba Wizara ihakikishe inapeleka taarifa za kutosha ubalozini kuhusu mazao na fursa za biashara ili kufanikisha utekelezaji wa diplomasia wa uchumi. Kama nilivyoeleza hapo awali kwamba Wizara imeendelea kushirikiana na Wizara za kisekta na taasisi za biashara za sekta binafsi nchini kutafuta masoko ya mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia imeshiriki pamoja na TANTRADE katika maonesho mbalimbali ya kibiashara. Kwa hiyo, balozi zetu zimepeleka sampuli za zao la korosho kwa ajili ya kuwasilisha katika nchi mbalimbali ikiwemo Vietnam, India na China. Aidha, balozi zetu zote zimeendelea kutangaza bidhaa za kimkakati zinazopatikana Tanzania. Vilevile Wizara imeendelea kuhamasisha taasisi za Serikali zinazohusika na biashara, kushirikiana na sekta binafsi kushiriki katika maonesho mbalimbali ya Kimataifa, ambayo yanatoa fursa kwa nchi kutangaza bidhaa zake.

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara pia, imeendelea kufungua of course Balozi mpya kama ilivyoelezwa na mwenzangu. Lakini nisisitize pia kwamba kwa kipindi hiki Wizara ipo katika hatua za mwisho kufungua consul kuu huko Guangzhou nchini China, niwahakikishie kwamba tuko katika hatua za mwisho. Pia Lubumbashi Jamhuri ya Demokrasia ya Congo baada ya kupata vibali kutoka katika nchi husika, maana yake katika kufungua hizi consul au balozi, lazima mpate pia kibali kutoka kwenye nchi zinazohusika. Hamuwezi kwenda mnaingia tu mnasema tumefika tunaanzisha na wenyewe inabidi watukubalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kama sisi kwa upande wetu tumeshamaliza mchakato huo, lakini tunasubiria hizo nchi husika na wenyewe waweze kuturuhusu wamalize mchakato wao, kusudi tuweze kufungua hizi balozi. Nina imani haitapita mwaka huu kabla hatujazifungua hasa Guangzhou na Lubumbashi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mambo mengine of course yameongelewa kuhusu kutangaza Kiswahili na kupeleka walimu na kufundisha lugha hiyo nje ya nchi, tayari mikakati hii imefanyika. Balozi zetu zimejipanga, tayari vyuo vikuu vya nchi za SADC karibu nyingi sana zimeanza mtaala/curriculum ya Kiswahili. Kwa hiyo, sasa iliyopo ni sisi huku wenyewe kujipanga na walimu wakaweza kwenda. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, maana nilikuwa juzi Afrika Kusini wameniambia Afrika Kusini tayari vyuo vyao vimeshaanzisha tayari curriculum ya Kiswahili. Botswana imeanza, Lesotho inaanza, lakini shida ni kwamba walimu wako wapi. Kwa hiyo, sisi tunaomba tushirikiane na sekta zote zinazohusika tuweze kuwapata walimu waende kufundisha Kiswahili kwenye hizo nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme kuhusu hili suala la Wizara kwamba iweke mkakati of course niliyosema ya kutangaza utalii nimeshaiongelea. Lakini niseme pia kwamba juhudi zinaendelea kwa mfano, Ubalozi Tanzania nchini Malaysia kama nilivyosema imeshawishi Kampuni ya Ndege ya Lion Group Air ya nchini Indonesia inayomiliki zaidi ya ndege 350 kuweka video kwenye ndege zao zinazoonesha utalii wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilimsikia Mbunge hapa nakumbuka mimi nilikuwa mmoja wa mwanachama wa Mozambique na Tanzania, kile chama kitafufuliwa Mheshimiwa Mbunge, maana mimi nilikuwa mjumbe, nilikuwa kwenye bodi lakini kwa uhusiano wetu wa Mozambique tena uko karibu sana na kutokea na yale yanayotokea Mozambique nadhani hiko chama kinahitajika sana, kutoa msukumo na kuweza kusimamia yanayoendelea katika nchi ya rafiki yetu hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba nikuhakikishie hayo ya DRC hatuna tatizo kabisa kama ninavyosema tunamalizia mchakato wa kufungua hiyo consul kuu nchini Lubumbashi kwa ajili ya kuendeleza mahusiano ya biashara, lakini najua tena kuna mambo mengi kati ya DRC na Kigoma. Kwa hiyo, tunayatambia na tuna consul kule ya DRC, kwa hiyo, wanataka nao kuanzisha mahusiano hayo. Kwa hiyo, kwa kweli tutaendeleza na kwa mchango wenu kwa kweli mimi naona kwamba kuna fursa nyingi sana ambazo saa nyingine wengi hawazifahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sijui nina muda gani, lakini naomba kwa hitimisho niruhusu kwamba baada ya maelezo hayo, ninaliomba Bunge lako Tukufu lipitishe na kuunga mkono bajeti ya Wizara yangu kwa mwaka 2021/2022 ili niweze kutekeleza yafuatayo:-

Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza, tunapende kutekeleza ipasavyo masuala yote yaliyoainishwa katika Sura ya Saba ya Ilani ya CCM yam waka 2020/2025 inayohusu mambo ya nje na ushirikiano wa kimataifa.

Pili, tuko tayari kutekeleza majukumu ya msingi ya Wizara kama ambavyo Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mkazo aliouweka katika hotuba yake hapa Bungeni tarehe 22 Aprili, 2021 ambapo ndio msingi wa mpango wa bajeti niliouwasilisha. Vipaumbele hivyo ni pamoja na kuimarisha na kukuza uhusiano na mataifa mengine pamoja na jumuiya za kikanda na taasisi za kimataifa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pili, tumejipanga kuimarisha utendaji kazi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na balozi zetu zote zilizoko nchi mbalimbali. Yale yote ambayo tumepata hapa leo kwa kweli itasaidia sana katika kujipanga na kuweza kuimarisha utendaji wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tatu, tutaendelea kushirikiana na Wizara za kisekta na sekta binafsi katika kutangaza vivutio vyetu vya utalii, kuvutia uwekezaji na kutafuta masoko ya bidhaa zetu nje.

Mheshimiwa Naibu Spika, nne, tutaendelea kushiriki kikamilifu kwenye shughuli za Kimataifa ikiwemo ushiriki wa Tanzania kwenye kulinda amani duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kwamba yale yote ambayo wameyasema tumeyachukua hasa yale ambayo wametaka kwa mfano, Zanzibar kwamba tuwe tunawapa taarifa mapema kuhusu ushiriki wao katika hii mikutano ya kikanda, lakini pia kuweza kuangalia nafasi za ajira watu wetu waweze kufanya na wenyewe kazi nje, lakini pia kuweza kuwapeleka watu wetu waweze kupata ujuzi na uzoefu kutoka katika nchi za nje hasa katika mahusiano yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mwisho, Wizara yangu imeongeza kasi ya kutekeleza majukumu yake kwa kufanya maboresho makubwa ili kufikia malengo yake pamoja na matarajio ya Watanzania. Hivyo kwa timu niliyonayo na kikosi nilichoongezewa na Mheshimiwa Rais, naomba Bunge lako lituunge mkono na kutupitishia bajeti niliyoiomba ili tukachape kazi, kazi iendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo naomba kutoa hoja. (Makofi)