Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Pauline Philipo Gekul

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Babati Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

NAIBU WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru sana kunipa nafasi na mimi nichangie machache katika Wizara yetu hii ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. (Makofi)

Awali ya yote nimshukuru sana Mwenyezi Mungu aliyetupa nafasi ya upendeleo ya kutupa afya njema sisi Wabunge wa Bunge lako Tukufu ili kuendelea na majukumu yetu ya kulitumikia Taifa Mwenyezi Mungu tunamshukuru sana. (Makofi)

Pia nimshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama yetu Samia Suluhu Hassan kwa kuniamini tena na kuniteua kuwa miongoni mwa wasaidizi katika Wizara hii ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kuwa naomba nimuahidi Mheshimiwa Rais kwamba nimepokea kwa mikono miwili kazi hii na nitaifanya kwa moyo wangu wote kumsaidia Mheshimiwa Waziri na kuisaidia Wizara hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Niwashukuru wana Babati kwa jinsi ambavyo wameniamini kuwa Mbunge wao wa Jimbo kwa awamu ya pili. Niwashukuru sana na niwaahidi kwamba nitaendelea kuwa mtumishi mwema kwao na msikivu ili tuweze kufikia yale malengo ambayo tumejiwekea ya maendeleo katika jimbo letu. (Makofi)

Kwa namna ya pekee nimshukuru Mheshimiwa Waziri, kaka yangu Innocent Bashungwa amekuwa akitupa ushirikiano katika Wizara yetu, lakini amekuwa akitupa maelekezo mbalimbali ili kutusaidia kufikia malengo ya Wizara yetu pamoja na malengo yaliyoanishwa katika ilani ya Chama cha Mapinduzi 2020 - 2025; Mheshimiwa Waziri nakushukuru. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, shukrani za dhati pia kwa Katibu Mkuu pamoja na timu yetu ya Wizara, Dkt. Hassan Abbas, Naibu Katibu Mkuu Ndugu Ally Possi pamoja na watendaji wetu wa Wizara na wadau wa Wizara hii wamekuwa msaada kwetu, lakini wamekuwa wakitupa ushirikiano mkubwa sana. (Makofi)

Niwashukuru wadau wote wa sekta hii tumekuwa tukishirikiana kwa karibu lakini pia niwashukuru viongozi wa dini ambao wamekuwa wakiendelea kuombea Taifa letu la Tanzania na kumuombea Mheshimiwa Rais wetu na Watanzania kwa ujumla; nchi yetu imeendelea kuwa salama na amani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa namna ya pekee niwashukuru wale wote wenye mapenzi mema, familia yangu, nawashukuru wanangu nawaona hapo juu Irene pamoja na wenzako kwa maombi ambayo mmekuwa mkituombea mama yenu pamoja na Tanzania na tunawashukuru kwa maombi hayo yaendelee. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Niwashukuru kwa namna ya pekee Wabunge wote wa Bunge hili waliochangia hoja ya Mheshimiwa Waziri kaka yangu Bashungwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na maoni mazuri ya Kamati ya Bunge lakini Wabunge walioongea humu ndani ni Wabunge 25, waliotuandikia kwa maandishi ni Wabungu wanne, jumla Wabunge 29 wameweza kuchangia hoja hii iliyoko mezani. Tunawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge.

Mheshimiwa Naibu Spika, michango ya Wabunge hawa sisi tumepokea kama Wizara na imekuwa michango ya afya sana kwetu kwa ajili ya kazi hii ambayo ipo mbele yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Wizara hii ni Wizara inayogusa ajira za watu, ni Wizara inayogusa hisia za watu, ni Wizara inayoelimisha lakini ni Wizara inayohabarisha Watanzania. Bila vyombo vya habari maana yake taifa letu tunakuwa kwenye giza. Wizara hii imekuwa ikihabarisha inafanya kazi kubwa ya kuunganisha Watanzania. Lakini Wizara hii kupitia michezo ni Wizara ambayo imekuwa ikisaidia Watanzania kujenga afya zetu lakini kuisaidia pia na Wizara zingine na Serikali kwa ujumla kuhakikisha kwamba Watanzania wanakuwa na afya njema na hata itasaidia pia kupunguza matumizi kwa upande wa Wizara ya Afya kwa bajeti ya dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tukuhakikishie kwamba maoni yao yote tumepokea na tutaendelea kuzingatia na kwa sababu ya muda kwa kuwa nina dakika 10 naomba nizungumzie hoja kadhaa ambazo zimewekwa mezani na nianze kuhusu hoja hii ya kukuza michezo katika nchi yetu.

Waheshimiwa Wabunge wamezungumza suala zima la kuhakikisha suala la michezo linapewa kipaumbele. Tunashukuru mnafahamu kazi kubwa inayofanywa na academy mbalimbali kwa ajili ya kukuza vipaji. Sisi kama Wizara tunaona kwamba hili ni la msingi na ndio maana ndugu zangu Waheshimiwa Wabunge Wizara yetu ikishirikiana na Wizara ya Elimu, Wizara ya TAMISEMI, tuliunda Kamati Maalum ambayo pia itapita huko kwenye ngazi za chini kuboresha michezo katika Halmashauri zetu na katika shule zetu za sekondari na za msingi ili vipaji vya Watanzania hawa ambao wanahitaji michezo hii vikuzwe kwa kuwapatia walimu bora, lakini pia mazingira mazuri ya viwanja pamoja na miundombinu ipatikane kwenye ngazi za chini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tuwahakikishieni kazi hii ambayo mmtupa na maoni ambayo mmetupa kuhakikisha michezo tunaboresha kuanzia ngazi za chini tumeshaanza kufanyia kazi na Kamati hii karibuni inakamilisha pia kupitia combinations mbalimbali ambazo zinafundishwa kwa shule za form five na form six kuhakikisha kwamba watoto wetu hawa ambao wanatoka huku chini, lakini wanafikia kidato cha tano na cha sita waweze pia kusoma masomo ya michezo ambayo tunaishukuru Wizara ya TAMISEMI na Wizara ya Elimu wameshafikia hitimisho kuhusu hili na kuanzia mwakani sasa udahili utafanyika ili hao watoto wetu waweze ku-specialized katika masomo hayo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hili Chuo chetu cha Malya pia Waheshimiwa Wabunge katika bajeti hii tunakwenda kukiboresha. Ukiangalia kwenye bajeti yetu ya mwaka huu ambao unaisha mwezi Juni tumetenga zaidi ya shilingi milioni 200 kwa ajili ya Chuo chetu cha Malya na maana yake fedha hizo zitakwenda kule zitaboresha. Lakini kwenye bajeti hiyo ambayo leo tunaomba ridhaa Waheshimiwa Wabunge kwenu Serikali kupitia Wizara hii tumetenga fedha shilingi bilioni 1.3 kwa ajili ya Chuo chetu cha Malya. Maana yake hao watoto wakianzia huku chini watakapofika kwenye chuo hiki na masomo ya juu wanakuwa wamebobea katika masuala ya michezo. (Makofi)

Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tuhakikishieni kazi hii tunaendelea kuifanya vizuri na kusimamia pia michezo kwa wanawake. Tunaomba mtuamini na hili tuendelee kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la pili ni kuhusu vijana wetu kupata mafunzo kule walipo, tumeshauri sana kuhusu taasisi yetu ya TaSuBa. Tumeshauri pia ndani ya Serikali tuendelee kushauriana na TAMISEMI, Wizara ya Elimu pia kuhakikisha mafunzo ya vijana wetu ya usanii yanapatikana kwa Wilaya zetu kupitia VETA, tunategemea kuanzisha ushirikiano pia na VETA ili vijana wetu wapate mafunzo hayo katika wilaya zao ambako VETA zipo. (Makofi)

Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge kwa hili pia itasaidia sana vijana wakipata elimu hawatakuwa wanafungiwa fungiwa maana tumeona pia sio kuwafungia fungia tu ndio kazi yetu, lazima tuhakikishe pia vijana wetu wanapata elimu. Kwa hili tupeane ushirikiano na mambo yatakwenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa haraka niende kwenye suala la TBC. Tunashukuru maoni yenu Waheshimiwa Wabunge kwa upande wa kuboresha TBC, lakini pia Wizara yetu inaishukuru Wizara ya Fedha kutupatia fedha za TBC zilitolewa zote kwa ajili ya kuimarisha usikivu katika maeneo mbalimbali ambako usikivu haujafika, ni TBC Television pamoja na redio zake. Nikuhakikishie kwamba Wizara yetu itaendelea kufanya kazi hii na katika bajeti hii pia tunaomba shilingi bilioni tano na tunahakikisha kwamba tutazimamia kwamba fedha hizi zifike kwenye mikoa na wilaya ambazo kwa kweli usikivu bado haujafika. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge kwenye hotuba yetu mmeona kwamba ni maeneo mbalimbali kama Kasulu, Tanga, Ngorongoro, Kahama, Bunda, Karagwe na maeneo mbalimbali usikivu bado tu. Tuwahakikishieni mpaka sasa tumeshafika Wilaya 102 lakini lengo letu ni kufikia Wilaya 119 kati ya 161 kupitia hizi shilingi bilioni tano ambazo mtatupatia Waheshimiwa Wabunge tuwahakikishie tutazimamia na usikivu utapatika kupitia redio pamoja television.

Mheshimiwa Naibu Spika, Lakini jingine ni suala la madeni ya TBC; Waheshimiwa Wabunge wameshauri kwamba TBC madeni yao yalipwe. Nikuhakikishie TBC wameshaanza kulipwa madeni yao 1.8 billions zimeshaanza kuingia na Wizara imeshawaandikia wale ambao tunawadai na kazi inaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni suala la TSN. Tumekaa kwa karibu sana TSN kuangalia kwanza kwa nini makusanyo yao yameanza kushuka. Kuna suala la UVIKO 19 lakini kuna suala pia la mitambo chakavu. Waheshimiwa Wabunge mmelizungumzia hili ndugu zangu, sisi Wizara yetu pamoja na Wizara ya Fedha tunashukuru fedha hizi ambazo TSN ilikuwa inadai zimeanza kulipwa na mmeshauri mtambo ununuliwe. Hili tumeshaanza kulifanyia kazi kwenye zile shilingi milioni 495 ambazo zimeshaingizwa kutoka Hazina tumeshaelekeza mchakato uanze wa ununuzi wa mtambo huu ili TSN sasa waweze kuchapisha magazeti ambayo yana ubora na yaweze kufika kwenye maeneo mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, huu mtambo utakaponunuliwa maana yake magazeti haya sasa yatakuwa na ubora, lakini pia yatafikia Watanzania kwa wakati. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tuwatoe wasiwasi, uhakiki wa madeni unaendelea lakini pia kupitia Wizara ya Fedha, tuishukuru Wizara ya Fedha wamehakiki madeni ya TSN na wameendelea kufuatilia na ndio maana walipohakiki waliamua kutupatia kiasi fulani. Kwa hiyo, niwatoe wasiwasi Waheshimiwa Wabunge kwamba kazi hii inaendele na TSN watanunua mtambo huu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ya muda niunge mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)