Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto

Sex

Male

Party

ACT

Constituent

Kigoma Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. KABWE Z. R. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna changamoto ya sukari; changamoto hii suluhisho lake ni uzalishaji. Tatizo ninaloliona ni kukosekana kwa utaratibu ndani ya Serikali. Hotuba ya Waziri ukurasa 140 ibara ya 191 inaeleza malengo ya kisekta ikiwemo viwanda. Hata hivyo, katika malengo tisa hakuna hata lengo moja kuhusu kuzalisha bidhaa zinazotumiwa zaidi na wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya bidhaa hizo ni sukari, nguo na mafuta ya kula. Hata hivyo, ukisoma hotuba ya Wizara ya Kilimo ukurasa wa 25 na ukurasa wa 44; Wizara hiyo imeelezea mikakati ya kulima miwa kwa ajili ya kuzalisha sukari. Ili miwa iwe sukari, tunahitaji viwanda. Wizara ya Viwanda na Biashara haina malengo haya. Je, Serikali haina uratibu? Serikali inasema sema tu bila uhakika isemalo?
Mheshimiwa Mwenyekiti, orodha ya miradi kwenye Wizara ya Kilimo inaweza kuzalisha tani 1.5m za sukari kwa mwaka. Kwa bei ya jana ya sukari na kupata $500m za Marekani kama forex. Hii ni robo ya lengo letu la mpango wa maendeleo kwa sekta nzima ya viwanda. Naomba mlete addendum ya hotuba ili tuweze kuwa na lengo la kuzalisha sukari na kuondokana kabisa na tatizo la sukari. Napendekeza muongeze lengo katika ibara ya 191 amendment ukurasa wa 140, ongezea (i) na rekebisha (i) iwe (ii) na kuendelea.
(i) Kuhamasisha kuanzisha na kuendeleza viwanda vya bidhaa zinazotumika zaidi na wananchi kama sukari na mafuta ya kula. Hii ni pamoja na kuhamasisha viwanda vidogo vya wakulima kwenye maeneo yanayolima miwa ya ziada kama Kilombero na Mtibwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia mapendekezo hayo hapo juu, naomba pia kusisitiza kuhusu viwanda vya kusindika mafuta ya kula. Tanzania ina mawese na alizeti ambapo iwapo tukiweka nguvu kubwa kwenye kuzalisha mawese na alizeti tutaweza kuwa na mafuta mengi zaidi na hata kuuza nje.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Kigoma tuna mpango/mradi wa kulima hekta 100,000 za michikichi kwa mpango wa hekta moja kwa familia moja. Iwapo tutafanikiwa tutaweza kuzalisha tani 200,000 za mafuta kutoka nje yenye thamani ya dola milioni 240 kwa mwaka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda inabidi ifanye kazi na Wizara ya Kilimo na Mkoa wa Kigoma ili kufanikisha jambo hili. Mkoa wa Kigoma na Mkoa wa Singida inaweza kuwa Mikoa ya kimkakati ya kumaliza kabisa uingizaji wa mafuta ya kula kutoka nje. Mipango iwekwe kwenye mikakati.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo litaondoa kabisa tatizo la ajira muhimu ni viwanda vya nguo (Textile Industries). Ukisoma hotuba ya Wizara ya Kilimo, unaona namna uzalishaji wa pamba umeshuka mwaka 2014/2015 kwa 47%.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo azma ya Wizara ya Viwanda lazima iendane na malengo ya Wizara ya Kilimo kuongeza uzalishaji wa pamba nchini. Kuna hatua za kuchukua sasa hivi ikiwemo udhibiti wa ukwepaji kodi unaofanywa na waagizaji wa nguo nchini. Viwanda vya ndani vya nguo vinapata shida kubwa sana kutokana na magendo ya nguo. Pambaneni na magendo ya nguo ili tulinde viwanda vya ndani vya nguo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda ifanye kazi na Wizara ya Kilimo ili kuongeza uzalishaji wa pamba nchini na tuongeze thamani ya pamba kwa kuzalisha nyuzi, vitambaa na nguo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kumalizia; viwanda vya sukari, mafuta ya kula na nguo viwe vipaumbele vya juu kabisa kuanzia mwaka 2016/2017. Tuwe focused, tuwe na sequence; narudia; nguo, mafuta ya kula na sukari.