Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Cosato David Chumi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafinga Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa kunipa nafasi na kwa haraka kabisa napenda kutumia nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama yetu Samia Suluhu Hassan alipokuja kulihutubia Bunge alieleza sasa nia ya Serikali kuanza kutenga fedha kidogo kidogo kugharamia timu zetu za Taifa na hata timu za wanawake napenda kutoa pongezi sana, lakini pia napenda kutoa pongezi kwa Azam kwa uwekezaji waliouweka ambao kwa kweli unasaidia tu sio sisi kuangalia mpira, lakini pia ni sehemu ya ajira. Ukienda huko kwa wananchi wetu kuna kitu kinaitwa vibanda umiza, unakuta mtu ana banda lake anaonesha mpira, anauza vinywaji, anapata kipato na maisha yanaendelea, kwa hiyo ninawapongeza sana.

Mheshimiwa Spika, lakini pia nitoe wito kwa vilabu wasibweteke tu na uwekezaji huu na wenyewe pia watafuta wadhamini wengine, lakini pia napenda kutoa pongezi wa wachambuzi wote wa michezo hususan zamani tulikuwa tumezoea vipindi vya michezo unasubiri jioni, lakini siku hizi kuna vipindi vya michezo hata katika stesheni za redio kama Wasafi, EFM TBC Fm unapata habari za michezo muda wowote, kwa hiyo nao napenda kuwapongeza sana.

Mheshimiwa Spika, sasa baada ya pongezi hizi watu wengi wamesema kuhusu michezo kweli michezo pamoja na kuwa ni burudani inatuondolea stress na kadhalika lakini kama ambavyo siku zote mimi nimesema michezo ni sehemu ya ajira ni mapato. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, michezo, sanaa na burudani ni kitu kikubwa katika uchumi wa nchi na hasa kwa kuendelea katika uchumi wa kutumia sayansi na teknolojia, digital economy michezo ina nafasi kubwa sana, lakini sasa michezo ili uweze kukupa hiyo tija sasa lazima kuwe na usimamizi bora, nitatoa mfano hapa tarehe 5 Mei, 2017 nilitoa mchango wangu hapa nikasema TFF ambao ni Tanzania Football Federation imegeuka sasa kuwa Tanzania Football fungia fungia kwa sababu ya kufungia fungia yaani jambo dogo tu unamfungia mtu, yawezekana kweli ni kanuni, mimi ninashauri, unajua unapomfungia mtu kama Mwakalebela ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa TFF ile ya Tenga ambayo ndio imejenga msingi wa mpira huu tulionao leo kwa kweli you have to think twice mimi kwa mawazo yangu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo yawezekana ni kanuni ni taratibu zao lakini wajaribu kuziangalia kuwe na adhabu ambao kidogo ni friendly ambao unaweza kumjengea mtu kurekebika kuliko kumfungia, unamfungia Mwakalebela miaka mitano, huyu mtu ambaye katika football, katika michezo ni mtu ambaye amekuwa na mchango mkubwa sana kwa hiyo ndio maana kunakuwa na lawama nyingi sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Leo hii sisi katika FIFA ranking Tanzania tupo wa 137 hata Libya ambao wako kwenye kupigana wako wa 119 sasa hata Mama alipokuja hapa kwenye Bunge alisema tumechoka na mimi nasema tumechoka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na kwa sababu tumechoka mimi ninashauri unawezekana ukawa ushauri sio mzuri na haitakuwa mara ya kwanza, sisi kwanza timu yetu ya Taifa kwanza ipumzike, tujipange, tujipange hata miaka mitano. Ghana wamefanya hivyo, Cameroon wamefanya hivyo, Comoro wamefanya hivyo, wamejipanga, leo hii tunajua Cameroon wako wapi, Ghana wako wapi, hata Comoro ambao vilabu vyao vilikuwa vikija hapa tunawafunga 12 kwa sifuri sasa hivi wameshatuacha katika list ya Afrika, yaani kama ile ambayo easy way of doing business sisi wa 141 katika East Africa Uganda ya 84; Kenya ya 102; Sudan ya 123; kwa kwa maana ya ile CECAFA Rwanda ya 129 yaani tuliowazidi sisi ni Burundi tu kwenye mazingira ya kufanya biashara pia tuliowazidi sisi ni Burundi tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo unaweza ukaangalia hivi vitu ni kama vile sijui kama vinashabihiana, sasa ukienda katika mpira wa Uingereza, Spain na Ujerumani wale wote ukienda Man U wawekezaji wametoka Amerika ukienda Chelsea - Abramovich ametoka Russia, ukienda Arsenal kwa nini wale watu wanakuja? Kwa sababu kuna mazingira bora ya kuwekeza katika mpira. Man City wanatoka Arabuni Leicester City wanatoka Singapore kwa sababu gani? Kwa sababu kuna mazingira bora ya nini ya kuwekeza, sasa mazingira bora yanatoka wapi, yanatoka kuanzia kwenye usimamizi wa watu wenye mpira ambao ni TFF.

Mheshimiwa Spika, sasa mimi huwa ninasema maisha ni ujanja, sio ujanja ujanja, lakini TFF inavyoendeshwa ni full ujanja ujanja ndio maana tunakosa nini uwekezaji, kweli leo hii wamekuja hao wa Azam, Azam wamewekeza pia nao kwa sababu watapata faida kwa kuuza ving’amuzi na kadhalika. Lakini kama tunataka serious watu wawafuate Azam ni lazima kwakweli mazingira ya uwekezaji kama yale tunayosema kwenye biashara katika mpira wetu yaboreshwe. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hapa watu wanazungumzia kujenga viwanja Serikali hii bajeti iliyokuja hapa bilioni 54, uwanja tu kama wa Abuja National Stadium bilioni 800 ambao unaweza kufanya mambo ya mpira na mambo hayo aliyokuwa anasema Mheshimiwa Babu Tale. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hiyo hapo Serikali haiwezi, Serikali iwe facilitator na vyombo vyake vya michezo, wawekezaji waje wawekeze. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitapenda kuzungumzia kuhusu COSOTA, BASATA na Bodi ya Filamu; hii mimi nimelisema miaka minne tunawashukuru wameviunganisha wamesema One Stop Centre. Ukienda EWURA ukienda NEMC hivi regulator authority unazikuta hadi ngazi ya kanda, ninashauri Serikali, ione uwezekano tuache kumsumbua msanii kutoka Kongwa, kutoka Itimbo Mafinga kutoka Tandahimba kuja Dar es Salaam akae siku tatu gharama za usafiri na kadhalika, haya siyo mazingira bora ya kuwawezesha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ninakuomba Mheshimiwa Waziri jaribu kama utaona ni gharama tumia Maafisa Utamaduni uwe japo na ngazi ya Kanda. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ninakuja Shirika la Magazeti ya Serikali; kama ambavyo tunasema tuwe na national career kwa maana lazima kama Taifa uwe na shirika la Ndege kama Taifa uwe na Shirika la Utangazaji, Shirika la Magazeti ya Serikali ni chombo muhimu sana katika dunia ya sasa.

Mheshimiwa Spika, magazeti yale ya Daily News, Habari Leo ndiyo chanzo kikuu ukitaka kusema cha taarifa za Serikali, lakini TSN mimi nimekaa newsroom, nimefanya kazi ya uandishi wa habari kwa miaka nane hali ya TSN siyo nzuri, wameomba bilioni 16 wanunue mtambo ambao utachapisha siyo magazeti yao tu, lakini utafanya uchapishaji mpaka kutoka watu wa Congo ita-generate income leo hii ukibeba gazeti la Daily News tunasema washindani, hawawezi kwasababu watu hawa hawana nguvu hiyo, hatujawawekezea. Sasa kama tumeweza kuweka nguvu kwenye Shirika la Ndege la Serikali, TBC mmeona kazi waliyofanya wakati wa mazishi ya Mheshimiwa JPM ni kwa sababu wamewezeshwa.

Mheshimiwa Spika, Leo hii TBC wamepewa shilingi bilioni tano; ninashauri tuiangalie sana Shirika la Magazeti ya Serikali ili liweze kushindana na akina The Guardian, liweze kushindana na akina Mwananchi, kwa sababu hiki ndiyo kisemeo cha Serikali. Tufumbe macho tuiwezeshe TSN ili kusudi hili gazeti la Daily News, diplomatic community kabla hajasoma chombo chochote cha habari anaanza kusoma Daily News, sasa Daily News haina uwezo tena wa kujichapisha kushindana na The Guardian matokeo yake hata mtangazaji anayepeleka matangazo hawezi kupeleka kwasababu halina mvuto. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo hawa watu TSN wanaidai Serikali nadhani almost shilingi bilioni 11 lakini na wao wanadaiwa na suppliers mbalimbali pesa nyingi tu. Kwa hiyo, mimi naomba Serikali na baadaye naweza nikashika shilingi inakuja na mkakati gani kuisaidia kitu ambacho ndiyo kisemeo cha Serikali, ili wasaidiane na TBC, wasaidiane na TBC Radio wasaidiane na vyombo vingine.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo kuhitimisha tu, mimi narudia tena, ili tuvutie wawekezaji katika sekta ya michezo, burudani na sanaa ni lazima tugeuke kuwa facilitators, wala tusiwaze sisi kama Serikali tutawekeza leo hii kama nilivyosema tulienda nakushukuru sana katika miaka mitano ulijitahidi sana Bunge Sports Club imeshiriki kwenye michezo ya Mabunge ya Afrika Mashariki tumeenda pale Burundi, tumekuta unaenda asubuhi uwanja wa mazoezi, kuna timu ina wachezaji 31 ni magoli kipa tu wana-train ugolikipa tu, na leo hii tunaona kuanzia Namungo kule golikipa ni Mrundi yule wako makipa wengi tu ni Warundi.

Mheshimiwa Spika, leo hii ligi yetu ina wachezaji kutoka Burundi wako wengi tu. Tumeenda pale Kampala watu wamewekeza sasa ili ukisimamia bora nitakwambia kwa kumalizia kitu kidogo tu, hata waamuzi sisi hapa hatupeleki waamuzi kwenye michezo, hawapati nafasi kwa sababu usimamizi siyo mzuri nitakwambia katika CHAN hii ambayo tulienda kushiriki hii katika waamuzi 47, 19 wa kati, wasaidizi walikuwa 20 na wale wa VAR (Video Assistant) walikuwa nane miongoni mwao wakiwepo akinamama wawili Lydia Abebe kutoka Ethiopia na Bernadeta Kwimbila kutoka Malawi. Sisi hapa kama hauna menejimenti nzuri ya mpira utakosa hata waamuzi.

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. COSATO D. CHUMI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana naunga mkono hoja. (Makofi)