Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Ramadhan Suleiman Ramadhan

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chake Chake

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, ahsante na mimi kuwa miongoni mwa wachangiaji kwenye hoja ya Mheshimiwa Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo. Kwa niaba ya watu wa Chakechake na mimi ninaunga mkono hoja hii kutoka mwanzo wa uwasilishaji wangu, lakini nitakuwa na ushauri kidogo kwa Wizara hii kwenye mchango wangu.

Mheshimiwa Spika, kabla sijaanza kwenye ushauri wangu binafsi nichukue nafasi hii kwanza kutoa pongezi kwa bondia Hassan Mwakinyo kutokana na ushindi alioupata juzi baada ya kumpiga bondia Muangola kwa KO. Anaipeperusha bendera ya Tanzania vizuri, Watanzania tuko nyuma yake na tunamuunga mkono. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pili nitoe pongezi kwa msanii wa kizazi kipya wa Tanzania, Nasib Abdul a.k.a. Diamond Platnumz kwa kuwekwa kwenye nomination ya Best International Act kwenye tuzo za BET. Nayo ni hatua kubwa na ya kupigiwa mfano. Na mimi niahidi kwamba nitampigia kura na kuwashauri Wabunge wenzangu tuungane kwa pamoja na Watanzania wote tumpigie kura. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, simpigii kura kwa sababu ni msanini tu, Diamond ni icon inayoamsha dreams za vijana wengi walioko nje ya muziki; ndio definition ya hard working, vijana wengi wanapotaka kujifunza kuhusu hard working na commitment kwenye tasnia au fani zao wanaweza wakamuangalia Diamond kama mfano. Kwa hiyo, hiyo inanipa mimi hiyo hamu ya kutaka kupiga kura kumpigia kura, ili apate kushinda imtie moyo kuendelea zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la tatu natoa shukrani kwa uongozi mzima wa GSM jinsi unavyoendelea kuishika Yanga na kutushika mkono kwenye kipindi hiki cha mpito, tunaelekea kwenye mabadiliko ya uongozi wa klabu wameendelea kutu- support kwa kiasi kikubwa. Kwa hiyo, pongezi pia ziende kwa Mr. Ghalib Salim Said na uongozi mzima wa GSM, Mungu awajalie. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, shukrani zangu za nne ziende kwa Azam Media Limited, wameuheshimisha mpira wa Tanzania. Mkataba wa shilingi bilioni 225.6 unaenda kuongeza thamani ya ligi kuu ya Tanzania. Unaenda kuvitendea haki vilabu vyote vinavyoshiriki ligi ya Tanzania, vilabu 16, sio tu timu kubwa za Simba na Yanga. Vilabu vyote vinavyoshiriki ligi ya Tanzania sasa kutokana na mkataba huu vitakuwa vina uwezo wa kupokea shilingi milioni 500 kabla ya msimu, hizi ni nyingi na zitawasaidia vilabu vidogo hasa ambavyo vipato vyao bado viko chini kuweza kujikimu na kuondokana na umasikini wa vilabu vyetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia wameutendea haki mpira wa Tanzania kwa sababu kwa mujibu wa mkataba huu coverage ya uoneshaji wa mpira inaenda kuwa asilimia 99 sasa. Kwa hiyo, tunaenda kuungalia mpira wa Tanzania kwa asilimia 99, hii ni heshima kubwa sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na niipongeze TFF kwa kukubali hiyo tender na mkataba huu kuingia na Azam ni media ya nyumbani, kodi inarudi nyumbani kwa hiyo, ni heshima kubwa sana kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi nataka mchango wangu nijikite kwenye mpira wa miguu. sisi wengine kileo chetu, hatuna starehe nyingine, kileo chetu ni mpira, aidha tucheze au tuangalie, tuzungumzie, yaani kitu chochote kinachohusiana na mpira, kwa hiyo mpira umekuwa ni sehemu ya maisha yetu tunavyotoka mpaka tulipo sasa. Moja katika kitu kinachotusononesha sana ukikaa ni kuangalia timu yetu ya Taifa, kwa kweli hatufanyi vizuri kwenye football, lakini nakusudia, hatufanyi vizuri. Tunapata progress, lakini haiendi kwa kasi tunayoitarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa ushauri wangu ili tupate maendeleo kwenye mpira ni lazima tukubali kuwekeza kwenye mpira, nakusudia investment kwenye mpira. Hatujawa serious kwenye kufanya investment kubwa kwenye mpira. Wenzetu wa Burundi na Mauritius wanapiga maendeleo makubwa kwenye soka, wanaleta revolution kubwa kwenye soka. Baada ya miaka mitano mbele tutakuja kushangaa watakapofikia na yote ni investment. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mpira ni profession, ni fani kama u-engineer, kama udaktari, kama ualimu, tusipowekeza tutakuwa tunajidanganya. Kama tuna uwezo wa kuchukua madaktari wetu kuwapeleka Urusi wakakae miaka mitano tunawalipia kwa pesa za Bodi ya Mikopo, kama tuna uwezo wa kuchukua ma-engineer kuwapeleka Japan, China, kuchukua madaktari kuwapeleka India wakakae miaka mitano ili tuje tubadilishe fani ya udaktari tuwe na ma- professional kwenye fani, the same ina-apply kwenye mpira. Hakuna ubabaishaji, tukitaka shortcut ndio tunapoharibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wenzetu wa Burundi wanachukua watoto wa miaka 11, wameingia mkataba na nchi za Scandnavia pamoja na Algeria, wanachukua watoto wao wenye talents, vipaji vya mpira wenye umri wa miaka 11 mpaka 14 wanapelekwa Algeria na Scandnavia, wanakaa huko kucheza, wako academy huko na federations ndio zinalipia gharama za kuwaweka huko. Tunalilia hatuna academy, hatujajenga academy, lakini wako duniani watu wanazo academy, tuwachukue hawa vijana wetu tuwapeleke kwenye hizo academy zilizoko duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukichukua vijana watano ukawapeleka academy PSG - Ufaransa, watano wenye umri wa kati ya miaka 14, 15, 16, baada ya miaka mitano unapata watoto wasiopungua 30 wacheza mpira professional ambao watakuja kuipa nguvu timu yetu ya Taifa. Na sisi ifike wakati tuwe na timu ya Taifa ukikaa nyumbani kutizama timu ya Tanzania inacheza, una soda, unakunywa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini sasahivi moyo, sisi wengine tuna maradhi ya moyo. Sisi wengine tuna maradhi ya moyo, yaani hatutabiriki, mara unapata maradhi. Leo tunacheza vizuri, kesho pasua kichwa. Maana yake sisi tunataka kuziba ma-gap kwa kuweka viraka viraka, mpira ni uwekezaji, ni professional, hakuna shortcut. Ni lazima tuweke strategy za muda mrefu, bora tuumie miaka mitano hii, lakini baada ya miaka kumi tuje kustarehe…(Makofi)

SPIKA: Poleni sana Yanga, ugonjwa wa moyo jamani. (Kicheko/Makofi)

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, baada ya miaka kumi tuje tukae tukistarehe tukiiangalia timu yetu ya Taifa. Sasa hivi mpira unachezwa na vijana wenye umri mdogo ndio wenye market. Ukisema mpira duniani sasa hivi unazungumzia uchumi. Wachezaji unalipwa kwa wiki pound laki moja, ni fedha nyingi. Watu ni fulltime job. Soka imekuwa fulltime job za watu hawafanyi kazi nyingine yoyote, ni mpira tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo nikiiuliza Wizara wanajua nini kuhusiana na Kevin John? Wanaweza wasiwe na majibu.

Mheshimiwa Spika, Kevin John kapelekwa Genk, alipofika Genk wameshindwa kuingia nae senior contract kwa sababu ya umri. Wamemchukua wenyewe Genk wamempeleka Uingereza, Leicester School, akae Leicester, asome lugha na vitu vingine ajue, apate ile general knowledge, halafu muda ukifika wa kuingia contract atarudi Genk. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunapolalamika kwenye mifumo na sera zetu za elimu, baadhi ya wakati na ajira za vijana wetu tunaweza tukaweka academy, sio lazima tusome chemistry, tuwalazimishe watoto wasome physics, wasome, unaweza ukawaweka academy ukawapa general knowledge ya kuyainua maisha tu na lugha. Yaani wakawa wamebobea mtu anajua lugha tano, sita, ikamtosha yeye kuwa aki-fail kwenye mpira anarudi huku kumsaidia kwenye maisha yake ya kawaida hizo lugha sio lazima tung’ang’anie vijana wetu lazima… (Makofi)

SPIKA: Ahsante Mheshimiwa Ramadhan Suleiman.

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Spika, naomba kuunga mkono hoja. (Makofi)