Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Zainabu Nuhu Mwamwindi

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. ZAINABU N. MWAMWINDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu inahitaji kwenda mbele kwa kasi. Ni jambo linalofahamika duniani kote kuwa tofauti muhimu ya nchi tajiri na masikini ni uzalishaji bidhaa za viwanda.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo kimetajwa kuwa ndiyo uti wa mgongo wa nchi yetu; kilimo hakiwezi kustawi bila ya viwanda. Wakati Serikali imelivalia njuga suala la viwanda hapa nchini, naomba kuishauri Serikali yangu sikivu ya Chama cha Mapinduzi kutazama nyuma wapi tulikwama kama Taifa na wapi tulipo na changamoto ipi tunazokabiliana nazo. Kwa mfano, mimi nimetoka Iringa ambako kuna kiwanda kikubwa cha karatasi kilichopo Mgololo Wilayani Mufindi. Namwomba Waziri wakati wa majumuisho anisaidie kuwaeleza Watanzania, ziko wapi karatasi za Mgololo katika soko? Kwanini zikipatikana bei yake huwa ghali kuliko karatasi zinazoagizwa kutoka nje ya nchi?
Mheshimiwa Mwenyekiti, kinu cha kusaga unga Iringa Mjini kilikuwa chanzo muhimu cha ajira na soko la uhakika la zao la mahindi Mkoani Iringa na mikoa jirani. Mheshimiwa Waziri pamoja na kuwa na ulinzi, kinu hicho kipo katika sekta pacha ya kilimo na viwanda, tunaiomba na kuishauri Serikali kuhakikisha kuwa kinu hicho kiwe katika asilimia mia moja ya uzalishaji ili kukuza ajira na uchumi wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake amebainisha kuwa Sekta ya Viwanda ni msingi wa maendeleo wa Sekta ya Kilimo umetueleza kuwa asilimia 99.15 ya viwanda vyote nchini ni viwanda vidogo sana na viwanda vidogo Iringa kama ilivyo baadhi ya Mikoa nchini kama vile Tanga, Morogoro na kwingineko, kuna uzalishaji mkubwa wa matunda ambayo mengi huishia kuoza mashambani kwa kukosekana kwa viwanda vidogo vya kati katika maeneo husika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri kuhusishwa kwa viwanda vidogo hasa katika maeneo ya uzalishaji ni ukombozi mkubwa kwa wakulima ambao wengi wao ni wanawake. Ufufuaji na uanzishaji wa viwanda utakuwa na maana endapo Wizara husika itaweka vipaumbele, kwani mwisho wa siku tunachotaraji ni kuwepo kwa viwanda vyenye tija. Tunapofufua kiwanda cha mbolea tutakuza ajira na kupunguza gharama za pembejeo kwa wakulima na kuongeza uzalishaji mkubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naiona ari na hamasa kubwa aliyonayo Mheshimiwa Waziri ya kuhakikisha kuwa Tanzania ya viwanda inawezekana. Wanawake wa Tanzania vazi lao ni khanga, naomba kushauri kwamba kifufuliwe Kiwanda cha Mutex na Urafiki.
Viwanda vilivyopo vimesababisha wanawake wengi sasa hawavai khanga kwa sababu ukubwa wa khanga kiurefu na upana ni mdogo sana. Namtakia kila la kheri Mheshimiwa Waziri na timu yake Wizarani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.