Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara

Hon. Exaud Silaoneka Kigahe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mufindi Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Viwanda Na Bishara

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia afya ya kufanya kazi ya kujadili na kupitisha Bajeti za Wizara mbalimbali hapa Bungeni. Lakini pia kwa namna ya pekee, naomba niwashukuru Mheshimiwa Spika, Naibu Spika, wewe Mwenyekiti na Wenyeviti wenzako wenza, Wabunge kwa namna ambavyo mnatuongoza katika Bunge hili kwa weledi mkubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba nianze kwa kuunga mkono hoja ya bajeti ya Wizara na Viwanda na Biashara iliyowasilishwa na Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Profesa Kitila Alexander Mkumbo, Mbunge wa Jimbo la Ubungo ambaye ndiye Waziri wa Viwanda na Biashara. (Makofi)

Naomba pia Wabunge wenzangu wote tuunga mkono bajeti hii ambayo imezingatia miongozo mikuu ya Kitaifa hususan Dira ya Taifa, Ilani ya Chama cha Mapinduzi na Mpango wa Tatu wa Maendeleo ya Taifa ya Miaka Mitano. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongelea baadhi ya hoja kidogo kulingana na muda. Lakini, hoja nyingine nitamuachia Mheshimiwa Waziri ambaye ndiye mwenye Wizara yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niongelee kuhusu ukaguzi wa bidhaa (destination inspection) hususan imeongelewa kuhusu magari hasa yaliyotumika. Utakumbuka kuwa ukaguzi huu sio mara ya kwanza sasa kufanyika katika nchi yetu, umeshakuwa unafanyika huku nyuma, lakini kutokana na baadhi ya changamoto ndiyo tulibadilisha baadaye kuanza kuwa na ile pre-verification of conformity to standards (PVOC) kwa maana ya kukagua nje bidhaa hizo kabla ya kuingia nchini na hasa magari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuona changamoto ambazo tumekuwa tukizipata na Waheshimiwa Wabunge wanajua, kwanza kulikuwa kuna ukosefu mkubwa sana wa ufanisi katika ukaguzi wa magari yao huko nje. Kwanza tozo iliyokuwa inatozwa kodi zile zilikuwa nyingi, muagizaji alikuwa anatakiwa kulipa takribani dola 150 kwa ajili ya ukaguzi ule. Lakini zaidi ya hapo, usumbufu zaidi anapotuma kule, walikuwa wanatuma hela zaidi ya dola 100 kwa hiyo, unatuma dola 150 ya ukaguzi lakini pia unatuma na dola 100 kwa ajili ya handling ya yale makampuni ambayo yanafanya kazi ya ukaguzi kule. Kwa hiyo, unakuta mtu anatuma dola 250 badala ya dola 150. Kwa hiyo, gharama kubwa ya ukaguzi na upimaji ilikuwa ni moja ya changamoto ambazo zilikuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mawakala wengi kutokuwa na ofisi na hivyo kuwa na changamoto kidogo kwenye ukaguzi huo. TBS sasa imeanza kukagua magari hapa nchini kuanzia mwezi Machi, 2021 na hakika kazi hii inaenda vizuri na nikutaarifu tu na Bunge lako kwamba kazi ya ukaguzi wa magari yaliyotumika nje unaenda vizuri na baadhi ya changamoto za kawaida ambazo ndizo tunategemea kwa mfano sasa tunapokagua pale baadhi ya magari ambayo hayakidhi viwango yanapewa muda wa kwenda kutengenezwa, halafu yanarudishwa kupata ile certificate ya TRA. Tumeshapata eneo la UDA pale ambapo magari yale ambayo yanahitaji kutengenezwa yanakaa pale yakishatengenezwa taarifa zile zinarudishwa TBS, TBS wanapeleka TRA wanapata ile certificate ya ukaguzi wanaendelea. Nina uhakika asilimia 80 ya magari yaliyokuja sasa yako vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na utaratibu uliokuwepo sasa hivi ni kwamba TBS wanashirikiana na wameshatoa maelekezo kwa kampuni yanayouza magari kule nje kuhakikisha kwamba wanaleta magari yenye ubora. Kwa hiyo, na sisi tunatoa rai kwa waagizaji wote wa magari kutoka nje watumie kampuni ambazo zinafahamika. Wasiagize kwenye kampuni ambazo hazifahamiki kwa sababu zile kampuni zimeshapewa maelekezo ya namna ya ubora ambao tunautaka sisi kama nchi kwenye magari ambayo yanaingizwa hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hili suala la ukaguzi wa magari au bidhaa za kutoka nje, lengo kubwa ni kuhakikisha tunakuwa na bidhaa zenye ubora na hivyo tukishamaliza hili tutajiimarisha tayari zaidi ya shilingi bilioni 60 zimeshatengewa kwa ajili ya kuweka mitambo ambayo itafanya ukaguzi wa magari lakini baadaye kukagua bidhaa nyingine ambazo zinaingizwa kutoka nje. Kwa hiyo, lengo ni kuona kwamba bidhaa nyingi zinakaguliwa sasa nchini ili kuepuka baadhi ya kampuni huko nje kutumia udanganyifu lakini pia na wafanyabiashara wengine kuingiza bidhaa ambazo hazina ubora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baadhi ya Waheshimiwa Wabunge wameongelea kuhusu Electronic Tax System. Huu ni mfumo ambao ulianzishwa kwa ajili ya kukusanya kodi kwa njia za kielektroniki. Lengo kubwa la mfumo huu lilikuwa ni kukusanya kodi ya Serikali. Makampuni au wafanyabiashara wengi hasa wenye viwanda walikuwa na questionable integrity. Ndiyo maana Serikali ikaona sasa ili kuondoka na tatizo hili la kutokuwa waadilifu kwa wafanyabisahara integrity kati ya Serikali na wafanyabiashara ilikuwa chini. Kwa hiyo, tukaanzisha mfumo hu una ufanisi wa mufumo huu umekuwa ni mkubwa ambao kimsingi umdhibiti udanganyifu uliokuwepo unafanywa na wafanyabiashara wasio waaminifu ambao walikuwa hawaripoti taarifa kamili ili waweze kulipa kodi stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, makusanyo kutokana na mfumo huu yameongezeka, lakini tukubali kwamba katika kufanya kazi yoyote au katika ufanyaji kazi huo kuna changamoto na changamoto kama ambavyo Waheshimiwa wameongelea ni kuhusiana na ile kampuni ambayo inafanya kazi hii kuchukua mapato mengi zaidi kuliko ambavyo Serikali inakusanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikutaarifu tu kwamba Serikali sasa inafanyia kazi hili na kwa sababu tulikuwa tumekubaliana, tumeingia mkataba na ile kampuni, kwa hiyo, cha muhimu tunaona namna gani tutakavyofanya ili kuhakikisha baada ya mkataba ule kuisha basi tuweze ku-review ile kampuni, lakini pia ikiwezekana tufanye sisi wenyewe hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na suala unyaufu wa korosho; niliongelee kidogo hili. Ni kweli kuna changamoto hiyo lakini tumeshakubaliana kwamba sasa tunaenda kufanya utafiti ambao utaangalia namna gani tuweze viwango vya unyaufu katika korosho. Utafiti huo utaongozwa na TARI kwa kushirikiana pia na shirika letu la Tanzania Bureau of Standards, lakini pia na Bodi ya Korosho na Chuo Kikuu cha Sokoine, lakini pia na wadau wengine kwa maana ya Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Vyama Vikuu, TAMISEMI lakini pia na waendesha maghala. Kwa hiyo, hilo pia tuanenda kuliangalia ili tuweze kuona namna gani sasa ya kutatua changamoto hii ya unyaufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee kidogo pia kuhusu vifaatiba na dawa za binadamu. Limeongelewa kuhusu viwanda vya vifaatiba na dawa; tuna viwanda zaidi ya 14 sasa; kati ya hivyo, viwanda 12 vinatengeza dawa za binadamu lakini viwanda viwili vinatengeneza vifaatiba na vingine viwili vinatengeneza dawa za kinga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Kamati ya Kitaifa ambayo inaendelea na upembuzi yakinifu kuhusiana na uanzishwaji wa kiwanda cha vifaatiba katika Mkoa wa Simiyu. Kamati hiyo, iko katika hatua mbalimbali za kuona namna gani ya kuanzisha kiwanda hicho ikiwemo maoni ya hawa Waheshimiwa Wabunge ambayo leo wameyatoa nayo yataingizwa kwenye Kamati hiyo ya Kitaifa ili tuweze kuwa na uhakika sasa wa kuanzisha kiwanda hicho katika Mkoa wa Simiyu. Kusudi ni lile lile kuhakikisha tunatumia malighafi zilizoko nchini kwa maana ya pamba angalau zianze sasa kutumika katika viwanda vyetu vya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba tena kuwasihi Waheshimiwa Wabunge kuunga mkono hoja bajeti hii iliyobeba ajenda kubwa ya Kitaifa na hasa ujenzi wa Tanzania ya viwanda. Hakika, kazi hii ni kubwa na sote tuunge mkono ili iweze kuendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja. (Makofi)