Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Martha Festo Mariki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu ya kilimo. Kwanza naanza kwa kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jinsi ambavyo wanaendelea kushughulikia matatizo yanayojitokeza katika Wizara hii ya Kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nitajikita moja kwa moja kwenye suala la masoko. Mkoa wangu wa Katavi, wananchi wa Mkoa wa Katavi kwa asilimia kubwa sana wamekuwa wakitegemea kilimo. Lakini wanazalisha mazao mengi, masoko yamekuwa ni tatizo na ukizingatia kwamba pembejeo zimekuwa na bei sana. Katika Mkoa wetu wa Katavi huwezi kuamini, gunia la kilo 100 linauzwa hadi shilingi… (Makofi)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge tusikilizane, tupunguze sauti. Tumsikilize Mbunge mwenzetu. Huyu anaitwa Mheshimiwa Martha Mariki na anafunga ndoa hivi karibuni sana, kwa hiyo… (Makofi/Vigelegele)

Zile kadi za michango Mheshimiwa hakikisha zinafika kote. Endelea kuchangia.

MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Spika, nilichokuwa nasema wananchi wa Mkoa wa Katavi hususan akina mama maana jambo lolote katika Taifa hili linapokuwa suala ni gumu sana sana lazima limguse mwanamke yeyote wa Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hivyo kwa maana kuwa, katika Mkoa wangu wa Katavi akina mama na akina baba wa Mkoa wa Katavi wamekuwa wakizalisha mahindi kwa wingi lakini masoko yamekuwa ni mtihani. Gunia la kilo 100 limekuwa likiuzwa mpaka shilingi 18,000. Hapo tunamuumiza sana mkulima huyo ukizingatia pembejeo zimekuwa zikiuzwa bei sana. Hivyo, niiombe sana Serikali kupitia Wizara yetu ya Kilimo waweze kumtamfutia mwananchi huyu masoko ya uhakika ili tuhakikishe mkulima huyu tunamkomboa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala langu la pili nitakalozungumzia ni suala la irrigation schemes. Katika Mkoa wetu wa Katavi tuna maeneo ambayo ni potential yakiwepo maeneo kama ya Mwamapuli, Mwamapuli tuna takriban hekta 13,600 ambazo zinaweza kukubali kilimo cha umwagiliaji. Hivyo, niiombe sana Serikali katika Mkoa wetu wa Katavi hususan eneo la Mwamapuli ambalo ni potential sana kwa kilimo cha mpunga, Mkoa wa Katavi umekuwa maarufu sana kwa kulima mpunga ambao ni first class ambao hata nchi za jirani zimekuwa zikija katika Mkoa wetu wa Katavi kuja kukusanya mpunga huo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo, niiombe sana Wizara ya Kilimo katika eneo la Mwamapuli tuweze kuwekeza kwenye irrigation schemes ili mwananchi wa mkoa huo aweze kulima, yani tufanye bandika bandua ili tuweze kumkomboa mwananchi na Taifa letu liweze kupata uzalishaji ulio bora. Wananchi wa Mkoa wa Katavi tunalima mpunga ambao ni first class na nikuambie tu Mkoa wetu wa Katavi mchele unaotoka pale ni mchele ambao ni first class, mchele wa kienyeji. Mchele ambao ukiupika lazima jirani asikie harufu kwamba ni mchele wa kienyeji uliopikwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo, niiombe sana Serikali tuwekeze eneo hili ili mwananchi yule aweze kulima na Taifa letu liweze kuingiza mapato kupitia kilimo. Niiombe sana Serikali yangu Sikivu na tukufu. Tukiwekeza katika kilimo tutakuwa tumemkomboa mwananchi kwani kilimo ni uti wa mgongo na wananchi wengi wa maeneo yale wanategemea sana kilimo hivyo tuwekeze hasa katika uchimbaji wa mabwawa makubwa ambayo tukiwekeza katika mabwawa makubwa yatasaidia katika kilimo hicho kikubwa na pia akina mama wa Mkoa wa Katavi watafanya kilimo cha mbogamboga na hivyo tutakuwa tumemgusa mwanamke wa Mkoa wa Katavi kwa kulima pia mbogamboga kwa kutumia umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo, niiombe sana Serikali, kwa kuwa muda ni mchache pia tuna maeneo mengine kama eneo la Kalema. Kalema ni eneo ambalo ni potential, hivyo niiombe Serikali tukiwekeza katika eneo hilo tutaweza kufanya kilimo chenye tija. Ukizingatia kwamba katika eneo la Kalema kumekuwa kuna miradi ya kimkakati ikiwepo ujenzi wa bandari ambao unaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa tukitumia kilimo tukazalisha kwa wingi na tukatumia bandari yetu ambayo tunajengewa na Serikali yetu Sikivu katika maeneo haya ya Kalema, tutaweza kwenda kufanya biashara na majirani zetu wa Kongo Kalemi kwa kupeleka mazao yetu kwa kutumia bandari hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, na Serikali imetuhakikishia kwamba tunaenda kujengewa meli za kusafirisha mizigo. Hivyo, niiombe sana Serikali tukiwekeza katika kilimo tutakwenda kumkomboa mwananchi na Serikali yetu itaingiza mapato na Taifa letu litaenda kusonga mbele. Pia, tutakuwa tumemsaidia kijana wa Kitanzania kwa kuweza kupata ajira nyingi sana zitakazotokana na kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hivyo kwa unyenyekevu mkubwa ninaiomba sana Serikali kupitia Waziri wa Kilimo aweze kutusaidia wananchi wa Mkoa wa Katavi kwa kufanya uwekezaji katika maeneo ambayo ni potential ili Serikali yetu iweze kumsaidia mwananchi kujikomboa. Wananchi wa Mkoa wa Katavi wanaipongeza sana Serikali kwa juhudi zao wanazoendelea kupambana ili kuhakikisha kwamba tunatatua matatizo ya wananchi. Hivyo, wananchi wa Mkoa wa Katavi tunaamini Serikali yetu Sikivu itatusaidia kwa kuweza kuwekeza katika maeneo hayo ambayo ni potential.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana. Naunga mkono hoja. (Makofi)