Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Jacqueline Kandidus Ngonyani (Msongozi)

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, nakushuru sana, na ninaomba Mwenyezi Mungu aniongoze katika mchango wangu.

Mheshimiwa Spika, naanza na Chama cha Msingi cha UMANA katika Kata ya Lisimunji, Wilaya ya Namtumbo. Kwenye hiki chama kuna mgogoro mkubwa sana Mwenyekiti na viongozi wengine wa chama hiki wametumia fedha za chama hiki vibaya. Kwa hiyo, wananchi ambao ni wanachama wameamua kumkataa huyu Mwenyekiti, lakini kilichojitokeza sasa wakati wa zile vurugu za kumkataa yule Mwenyekiti Diwani alijitokeza akaenda kushirikiana na wale wananchi kwa ajili ya kutaka kujua hatma ya suala zima la chama hiki juu ya huyo mwenyekiti na viongozi wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini viongozi kutoka wilayani kwa maana ya Serikali wakaenda wakamchukua yule Diwani wakamweka ndani, jambo ambalo si sawa, Diwani alikuwa anatetea haki za wananchi wake, lakini amewekwa ndani hii si sawa na niombe Serikali yangu, niiombe Serikali ishughulikie suala hili kupitia waziri mwenye dhamana aende akachunguze kule kulikuwa na tatizo gani na ikiwezekana huyu Diwani alipwe fidia kwa kufedheheshwa na kuwekwa ndani wakati akitetea maslahi ya wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo jingine ni kuhusu na suala la ushirika, ushirika kupitia AMCOS na UNION mimi nadhani kwamba hawa watu hawajajipanga vizuri, hawako sawa, kupitia AMCOS na UNION hawa watu hawana wanachokifanya cha kuwasaidia wanachama badala yake wameweka kama ni sehemu yao ya kujinufaisha wao wenyewe migogoro imekuwa mingi na wananchi hawasaidiwi kwa namna yoyote ile na ndiyo maana kumekuwa na kelele nyingi kuhusiana na suala la stakabadhi ghalani. Wananchi hawahitaji stakabadhi ghalani inayohusiana na mazao madogo madogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, stakabadhi ghalani imeletwa na Serikali kwa maana nzuri kabisa ili iweze kuleta tija na imefanya vizuri sana kwenye mazao makubwa kama korosho, pamba lakini kwenye ufuta, soya na mazao mengine madogo madogo ambayo yanakwenda kumsaidia mkulima haijafanya vizuri. Mkulima mdogo amelima ufuta maana ni zao ambalo linamsaidia auze aweze kujikimu kwa mambo madogo madogo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa Serikali inavyoingilia kati na kusema kwamba mwananchi huyu apeleke zao hili kwenye stakabadhi ghalani maana yake ingekuwa ina tija kwa wananchi hawa wasingekuwa na kelele.

Mheshimiaw Spika, nitoe ushauri kwa Serikali hii, irudi ikajipange upya iondoe suala la stakabadhi ghalani kwenye mazao haya madogo madogo iache kwenye mazao makubwa kama korosho na mazao mengine lakini siyo ufuta. (Makofi)

T A A R I F A

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Mheshimiwa Msongozi unapewa taarifa.

MHE. TWAHA A. MPEMBENWE: Mheshimiwa Spika, napenda tu kumpa taarifa mzungumzaji, anayoyazungumza ni ya msingi zaidi na hii ndiyo sababu unaona Mkoa wa Dodoma leo hii hawalimi zao la ufuta. Ahsante sana. (Makofi)

SPIKA: Nakushukuru sana, Mheshimiwa Msongozi endelea.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, sasa mtani wangu wewe umechangia asubuhi halafu unanipotezea muda.

Mheshimiwa Spika, namba choroko, soya, ufuta hivi havina haja ya stakabadhi ghalani. Kwa mfano, wanawake wa Mkoa wa Ruvuma unapolima mahindi, korosho, tangawizi unaweka shamba dogo la mama kama kuna UPATU, VICOBA, kumpeleka mtoto zahanati na mambo mengine kadha wa kadha ndio ule ufuta unasaidia. Ukimwambia mwanamke achukue ule ufuta debe mbili apeleke huko akasubiri, mnamtakia nini huyu mwanamke wa Mkoa wa Ruvuma? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala hili haliwezekani asilani abadani. Mimi niwaombe Waziri na Naibu Waziri waje na majibu mazuri wakati wa wind-up waondoe suala hili la stakabadhi ghalani kwenye mazao madogo madogo. Mazao madogo madogo haya ni aibu jamani kwani ndiyo yanamsaidia mwananchi. Siku moja Mheshimiwa Flatei alisema ataruka sarakasi mimi kuhusiana na suala hili nauliza nipande juu ya meza? (Makofi)

SPIKA: Hapana.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Nipande juu ya meza kama Kanuni inaruhusu?

SPIKA: Mheshimiwa Msongozi usipande juu ya meza.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, kwa kweli kwa Mkoa wa Ruvuma hatukubali. Naomba suala hili liondolewe na Wizara ikajipange upya hata mwakani waje wakati wametoa elimu kwa wananchi lakini pia…

SPIKA: Mheshimiwa Msongozi usipande juu ya meza leo hapa kitaeleweka kuhusu stakabadhi ghalani. Waziri yuko hapa, leo hapa leo hapa, malizia Mheshimiwa Msongozi nilitaka tu usipande juu ya meza. (Makofi/Kicheko)

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa sababu mimi nilisema leo labda ningepanda juu ya meza dunia ijue na Tanzania nzima waone kwamba hatuhitaji suala hili.

Mheshimiwa Spika, nikushawishi uniongezee dakika moja niendelee kuongelea suala hili. Wako vijana wetu wamemaliza vyuo, wametoka JKT wamefanya mafunzo lakini wamerudishwa nyumbani ajira hakuna. Hawa vijana wamejikita kulima mazao ambayo yanaweza kuwaletea pesa kwa haraka ikiwemo ufuta, soya na vitu vingine lakini wanakatishwa tamaa. Hili zao la ufuta sasa limekuwa kama vile mtu unalima bangi, ukishavuna debe mbili za ufuta basi unafuatwa unazingirwa. Hata mambo mengine ndani ya nyumba hayawezi kuendelea vizuri kwa sababu unafuatiliwa huko yaani muda wowote unagongewa kuulizwa zile debe mbili ziko wapi? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana.

MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI: Mheshimiwa Spika, vijana wetu hawa watakuwa majambazi sasa kwa sababu wanataka wawekeze kwenye ufuta lakini Serikali inawapiga danadana.