Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Tunza Issa Malapo

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi mchana wa leo nami nichangie kidogo kwenye Wizara ya Kilimo.

Mheshimiwa Spika, kwenye suala la kilimo cha umwagiliaji hapa pana changamoto nyingi. Tunafahamu kilimo kinahitaji maji na siyo lazima yawe maji ya mvua ndiyo maana tunasisitiza kwamba kuwe na kilimo cha umwagiliaji. Ukiangalia eneo linalofaa kwa umwagiliaji ni asilimia ndogo sana inatumika. Hata ile inayotumika ufanisi wake bado ni mdogo.

Mheshimiwa Spika, nilikuwa kwenye Kamati ya Kilimo, tumepita kwenye miradi ya umwagiliaji, utasema nao kule kwenye miradi wanalima kwa kutegemea mvua. Binafsi nilikuwa nategemea kwamba tunapokwenda sehemu ambayo ina skimu ya umwagiliaji tukute shughuli za kilimo zinaendelea mwaka mzima lakini mambo yanayoendelea pale hayaridhishi. Unaambiwa pesa nyingi za Serikali ziko pale lakini kinachoendelea hakieleweki. Huko kwenye umwagiliaji miradi mingi pesa imepigwa, vyanzo vya mapato havieleweki ile miradi ambayo ipo…

T A A R I F A

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Kunti.

MHE. KUNTI Y. MAJALA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba nimuongezee tu Mheshimiwa Tunza kwamba vyanzo vya mapato vinavyotarajiwa kukusanywa mwaka huu wa fedha kupitia sekta ya umwagiliaji ni uuzaji wa nyumba pamoja na magari chakavu ambapo wanatarajia kukusanya shilingi milioni 15.

Mheshimiwa Spika, hiyo ndiyo sekta ya umwagiliaji. (Makofi)

SPIKA: Mheshimiwa Tunza, unaipokea hiyo taarifa?

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, naipokea kwa mikono miwili, inaonesha ni namna gani Serikali haiko serious kuwekeza kwenye umwagiliaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano ukija Mkoani kwetu Mtwara, Mkoa mzima wa Mtwara wameainisha kwenye hotuba yao kwamba eneo linalofaa kwa umwagiliaji ni hekta 24,317 lakini zinazotumika ni 3,729, ni asilimia 15 tu. Matatizo haya ya kutokuwekeza kwenye kilimo kingine tofauti na korosho ndiyo maana watu wa Mtwara korosho ikifanya vibaya utasema tuko msibani. Kama sasa hivi nenda Mtwara uikute hali yake, mimi nimetoka huko juzi. Kilimo cha mazao ya korosho, mpunga, mahindi hayaeleweki, kilimo cha umwagiliaji kiko asilimia 15 tu; nenda huko kwenye skimu kwenyewe hakuna kinachoeleweka.

Mheshimiwa Spika, hii Wizara inatakiwa iwe serious. Ukipita kwenye skimu zote za umwagiliaji zina migogoro. Kwa nini wanawekeza pesa sehemu ambazo hawajatatua migogoro? Watu wanashindwa kulima kwa sababu ya migogoro iliyopo pale; Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri ni mashahidi. Tatueni migogoro, wawezesheni watu walime ili tutoke hapa tulipo tusonge mbele. La sivyo, kila siku tutakuwa tunaimba lakini kile tulichokikusudia hakiwezi kuleta tija kwa sababu hatuweki misimamo iliyo sahihi na thabiti kukiendea kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niongelee korosho kidogo, wenzangu wameongea sana, mwenye masikio asikie. Sisi watu wa Mtwara hatutaki kuchanga ile pesa ya pembejeo; yaani huo ndiyo msimamo wetu, hatutaki. Hatutaki kuchanga kwa sababu gani? Mtu hauwezi kukataa bila kuwa na sababu. Sisi hatutaki kuchanga kwa sababu kuna export levy imekusanywa, ninyi mnajua, siyo chini ya bilioni 400.

SPIKA: Mheshimiwa Waziri, hawa Wamakonde wakikwambia kitu fulani hatutaki yaani wanamaanisha. Ukisikia hatutaki chichi hicho kitu yaani ujue hawataki. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Tunza, endelea. (Kicheko)

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru unatuelewa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, hawa watu wana hela zetu na wanajua wanazo, kwa nini leo wanatulazimisha tuchange? Zile hela zetu ambazo mnazo kule tangu msimu wa 2017/2018 mpaka leo mmezitumia kufanyia nini?

Mheshimiwa Spika, mimi nikiwa Mbunge ninayetokea Mkoa wa Mtwara, tunawaambia kabisa tafuteni namna sisi tupate pembejeo, watu walime tuvune korosho tuuze. Hizo habari za kutuzungukazunguka kutuambia sijui tukatwe shilingi 110 kutoka kwenye kila kilo ya korosho hatutaki kwa sababu hela zetu mnazo. Yaani ninyi msituzugezuge kutuona kama sisi hatuelewi, sisi tunaelewa vizuri sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la mwisho nalotaka kumalizia; mimi najiuliza sisi kama nchi hivi ni zao gani kabisa tunajivunia kwamba hili zao ndiyo tunalilima kwa kiasi kikubwa?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Tunza, dakika ndiyo hizo.

MHE. TUNZA I. MALAPO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. (Makofi)