Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Boniphace Mwita Getere

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bunda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara ya Kilimo. Nikupongeze wewe mwenyewe kwa jinsi unavyoendesha Bunge hili toka mimi nimeingia humu hii term ya pili, unaendesha Bunge vizuri sana mimi kwa kweli naku- mind yaani unafanya kazi vizuri sana. Kuna hospitali inajengwa kule kwangu Unyali ambako ulikuwa unaishi inaitwa Ndugai, ikikamilika nadhani tutakupeleka ufungue sasa hapo ndiyo utaona maisha yanaendaje huko. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niishukuru Wizara ya Kilimo viongozi wake wako vizuri sana, Waziri, Naibu Waziri, viongozi wote wako vizuri, kinachozungumzwa hapa ni matatizo ya kilimo ya muda mrefu. Wabunge wakiwa wakali hapa Mheshimiwa Profesa Mkenda na Mheshimiwa Bashe msiseme wanawasema nyie, tunazungumza matukio ya kilimo toka uhuru yanaendaje, tatizo letu liko hapo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kabla sijaendelea, naomba unipe nafasi kidogo niseme jambo moja. Kwa nini tusiunde kamati hata kama ni ya watu watano professional ambao watakuwa wanaangalia hizi Wizara? Waangalie katika bajeti hii 2020/2021 tumesema nini, bajeti ya 2022/2023 waje watuambie hapa tulichokisema wakati uliopita ili watakapokuwa wanazungumza kwenye bajeti mpya tuwe tunaona wametenda nini na wamepatia wapi? Haiwezekani kuzungumza habari ya kilimo cha pamba, korosho, alizeti miaka nenda rudi hakuna kinachotatuliwa. Lazima tujifunze jambo moja tujue ni wapi tumekamilisha jambo limeenda vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jana ulikuwa unasema mambo ya tija, tunapozungumzia tija ni jambo kubwa sana. Tija ya mazao yote kwa mfano tija ya pamba, wenzetu wa Misri, Sudan, India heka moja ya pamba wanazalisha kilo 1,000 mpaka 1,200, Tanzania heka moja ni kilo 250 mpaka 300. Sasa fikiria tija ilivyo, ukizalisha 300 kwa heka moja ukauza kwa Sh.2,000/= ni Sh.600,000/=, ukizalisha 1,000 kwa heka moja ukiuza Sh.1,000/= ni Sh.1,000,000. Kwa hiyo, suala la tija hapa ni muhimu sana katika uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, sasa watu watuambie jamani mliyozungumza msimu uliopita sasa tumetekeleza. Kwa mfano Jimbo langu la Bunda, Tarafa ya Chamriho ndiyo wazalishaji wakubwa wa pamba Mkoa wa Mara, waje waseme pamba tumefikia kiwango hiki lakini sasa hivi kazi ni ile ile. Ukizungumza pamba, alizeti na ufuta tija hakuna. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mbaya zaidi sasa mkulima anaanza kutayarisha shamba mwenyewe, kulima na kupanda mwenyewe, anatafuta mbegu mwenyewe, analinda usiku wanyama wa pori wakali mwenyewe, ikifika kwenye kuuza Serikali imefika, akitaka kuuza kila mahali anazuiliwa, mambo ya ajabu haya duniani hapa. Kwa hiyo, nafikiri sasa ifike muda tumsaidie mkulima kwenye kuzalisha apate tija kubwa na sisi twende kuingia.

Mheshimiwa Spika, zao la pamba lilivyo kwa mikoa yote inayouza pamba, mkulima analima na kupanda mwenyewe, akienda kuuza anaenda kwenye ghala anakopwa. Siku ya kwanza anapeleka pamba AMCOS amekopwa, AMCOS wanachukua pamba wanapeleka kiwandani wamekopwa, kiwanda kinachukua fedha kinapeleka benki mkulima hajapata fedha, ni shida. Watafiti watuambie kwa nini mkulima wa pamba akipeleka pamba ghalani asipewe pesa pale pale, kuna hoja gani? Pamba ya mtu inakopwa kwa sababu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa huwa najiuliza maswali ya kiakili tu, hivi pamba imeenda ghalani, AMCOS haina hela, amekopa mkulima, hivi ghala likiungua analipa nani? Pamba imechukuliwa kwenye gari inapelekwa kiwandani sio ya kiwanda ni ya AMCOS hivi gari ikiungua atalipa nani? Kwa nini kama watu wana fedha wasiende kununua pamba kwenye maghala ili wakulima wapate fedha zao? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, AMCOS hawana hela, hivi kuna haja gani ya kuwa na AMCOS? Kama kweli Serikali inataka AMCOS iwepo, iwape fedha kama ilivyokuwa zamani, Ushirika zamani walikuwa wanapewa fedha wanaenda kununua pamba. Sasa tuna AMCOS haina fedha, ni mawakala tu, wanasubiri mkulima alete pamba waanze kumdhulumu. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, kilo moja mara 100, 200 …

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Getere.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, naunga mkono hoja lakini ndugu zangu rekebisheni yale mambo tunayozungumza humu ndani. (Makofi)