Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Cecil David Mwambe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Ndanda

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. CECIL D. MWAMBE: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niweze kuchangia, maalum kabisa ninataka niongee na Mheshimiwa Waziri pamoja na Naibu wake hasa zaidi waweze kutusaidia sisi wakulima na kipekee kabisa niongee kuhusu wakulima wa korosho.

Mheshimiwa Spika, ukifika Mtwara maeneo yote ambayo utapita wananchi wa kule wanalima korosho, lakini kwa bahati mbaya kabisa ukilinganisha maisha yao halisi na sifa tunazopeana hapa ndani Bungeni kwamba wananchi wa Mtwara na Lindi pengine wa kusini kwa ujumla ni wakulima wa korosho wanaongeza pato kwenye mapato ya nchi yetu hawafanani kabisa na hicho tunachokisema. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, wanaonufaika ni wasimamizi au wa Ushirika au wasimamizi wa Bodi ya Korosho au Wasimamizi wa Vyama Vikuu vya wanaosimamia manunuzi, lakini wakulima kama wakulima hawanufaiki. Mheshimiwa Waziri nilimpa taarifa na nilipeleka mchango wangu pia kwenye maandishi na Mheshimiwa Naibu Waziri pia kwamba kuna ubadhirifu mkubwa sana umefanyika ndani ya Bodi ya Korosho, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Korosho ndiyo maana Wabunge wote hapa wanaotokea maeneo hayo wamelalamika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunaomba ukafanye ukaguzi pale ndani kuna pesa zaidi ya shilingi bilioni 1.5 zimetumika nje ya utaratibu kabisa na tunamwambia hapa Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anamaliza na ku-windup hapa atueleze hatua anazochukua dhidi ya Mkurugenzi huyu kwa haraka kwa sababu vinginevyo sisi tunakwenda nyumbani kufanya mikutano na wananchi wetu na tutakwenda kuwaeleza kwamba Waziri anamlinda na kumtetea Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho kwa sababu labda ana maslahi binafsi na yeye, lakini sisi hatusaidii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mtu mwingine ni Meneja wa Chama Kikuu cha Msingi cha Mtwara ambaye ni Meneja wa MAMKU Mheshimiwa Naibu Waziri anamfahamu naye ni mmoja wa watu wanaonufaika sana na zao la korosho bila kuwa na shamba hata nusu eka nyumbani kwake na wenyewe tunaomba kabisa na siku ya uchaguzi mkuu pale wakulima walimkataa, wakataka kabisa na kuandamana.

Mheshimiwa Spika, Mheshimiwa Waziri mwenyewe alihusika kupiga simu akawaambia jambo hili tutahakikisha tunapata suluhisho siku chache zijazo, sasa hivi mwezi mzima umepita hakuna hatua yoyote aliyochukua Mheshimiwa Bashe na yeye tunamuomba kama ana maslahi binafsi na huyu ndugu basi amuondoe Mtwara ampeleke kwao Tabora akasaidie kwenye mazao mengine kwenye Korosho hawezi kufanya kazi. (MakofI)

Mheshimiwa Spika, jambo jingine ni suala la, masuala ya stakabadhi ghalani, Mheshimiwa Mulugo hapa jana aliongea kwa uchungu mkubwa kabisa suala la stakabadhi ghalani akiomba Serikali iondoe mfumo huu. Mheshimiwa Bashe hapa alikuja akaongea mwenyewe ndani ya Bunge hili labda kama alikuwa ameamua kufanya utani na sisi Wabunge kwamba mazao ya maeneo ya Dodoma, Songwe, Katavi wasitumie huu mfumo kwa sababu hawajiandaa kutumia huu mfumo.

Mheshimiwa Spika, lakini sisi kwetu kwenye zao la Korosho mfumo wa stakabadhi ghalani ni sehemu ya ukombozi na uhai, tunachotaka sisi kikubwa mfumo huu uboreshwe na siyo kuondoa kwa sababu umekuwa ukiwasaidia wakulima. Lakini pia, urasimishwe ukipata stakabadhi yako ya ghalani kabla hujalipwa kwenye ghala lako uweze kutumia stakabadhi kwenda nayo hata hospitali na hospitali zikutambue kwa sababu tuna hospitali za Serikali uweze kupata matibabu tuachane na hivyo vitu vingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwenye hotuba yako pia uliyotuwasilishia hapa umeongea kuhusu skimu, lakini mimi naweza kukwambia umeleta utani mkubwa kwenye masuala ya skimu umeitaja skimu ya Ndemba halafu inaonyesha kwamba ina eka moja na hii ni skimu ya Serikali, umeitaja skimu ya Maparagwe yenye eka 450, lakini Kijiji chenyewe cha Maparagwe hakifikii hata eka 30. Mheshimiwa umetaja hapa skimu ya Liputu yenye eka 10 hizi ni skimu za Serikali, umetaja Skimu ya Chingurunguru eka tano ni uongo kwa sababu Chingurunguru hata shida ya maji ya kunywa kule ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, waambie watalaam waende hatuna hata maji ya kunywa tuanze sasa kutoa maji mengine ya kumwagilia hicho kitu hakuna. Umetaja skimu ya Ndanda yenye eka 350 eka zinazotumiwa pale hazizidi eka thelathini na wananchi wamekuwa na migogoro kila siku tunataka sasa tujue Serikali kama ilipeleka hapa pesa zimetumika namna gani kwa ajili ya watu hawa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuna suala hapa pia ambalo pia umelitaja na waheshiwa Wabunge wote wamelichangia kuhusiana na suala la pembejeo ambazo zinakwenda kugawiwa sasa na mfumo wa Serikali.

Waheshimiwa Wabunge wameshauri kwamba Serikali itafute pesa na ione namna sasa ya kulipa pembejeo hizi badala yakwenda tena kuwakata wakulima ambao wamekuwa wanakatwa kila wakati na sheria haiwezi kurudi nyuma.

Mheshimiwa Spika, kama mnataka kuanzisha huu utaratibu zile pesa ambazo zilikatwa shilingi bilioni 210 kabla sheria haijabadilishwa ziko wapi? Zilitumika kufanya jambo gani? Kwa nini hizi zisitumike wakati huu na sisi Serikali kuturudishia ili tuendelee kwenda mbele na tuweze kuongeza mavuno. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine hapa ni suala la TARI. Wananchi wanakatwa shilingi 25 kwa ajili ya Mfuko wa CBT lakini wananchi pia wanakatwa shilingi 25 kwa ajili ya kupeleka kwenye vyuo vya utafiti. Tunataka Serikali itueleze shilingi ngapi mpaka sasa zimepelekwa kwenye utafiti. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi hii, nasubiri majibu. (Makofi)